Tuesday, March 25, 2014

Tanzania, DRC zaimarisha uhusiano kiuchumi

Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe akiagana na Waziri Justine Mwanangongo Kalumba mara baada ya mkutano wa pamoja. Kulia mstari wa mbele ni Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini (DRC), Mheshimiwa Marcellin Chishambo na kushoto ni Balozi wa Tanzania nchini DRC, Balozi Anthony Cheche.
Waziri wa uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe (kulia) akiwa katika mazungumzo ya pamoja na Waziri wa Uchukuzi wa DRC Mhe. Justine Kalumba mwenye miwani wa pili kushoto.
Waziri wa Uchukuzi  Dkt. Harrison Mwakyembe akizungumza na waandishi wa habari mara baada
Kukutana na Gavana wa Jimbo la Kivu Kusini (DRC), Mheshimiwa Marcellin Chishambo mwenye kofia. Wa kwanza kulia ni Balozi wa Tanzania DRC Mhe. Anthony Cheche.
Na Mwandishi wetu, Kinshasa
Serikali ya Tanzania na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo zimekubaliana kushirikiana kuondoa vikwazo vya usafirishaji wa bidhaa kati ya nchi hizo mbili ili kurahisisha usafirishaji wa shehena ya Kongo inayopitia bandari ya Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Kaimu Meneja wa Mawasiliano, Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), Bi. Janeth Ruzangi, makubaliano hayo yalifikiwa hivi karibuni wakati Mawaziri wa Uchukuzi wa nchi hizo mbili walipokutana mjini  Kinshasa, Kongo.

Katika kikao hicho, Waziri wa Uchukuzi Dkt. Harrison Mwakyembe alimweleza Waziri wa uchukuzi wa Kongo, Bw. Justine Kalumba kwamba Tanzania imedhamiria kuondoa changamoto mbalimbali zinazowakabili wafanyabiashara wa Kongo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam ili kuondoa ucheleweshaji na kuongeza ufanisi wa huduma za uchukuzi wa shehena hiyo.

Dk. Mwakyembe alisema uhusiano mzuri uliopo baina ya nchi hizo mbili lazima uwe wa manufaa kwa wananchi wake na kwamba wakati ulikuwa umefika wa kuondoa vikwazo vinavyokwamisha biashara kati ya nchi hizo mbili.

Waziri Mwakyembe alisema Serikali ya Tanzania inaendelea kuboresha huduma za uchukuzi kwa njia  ya reli, barabara, bandari na usafiri wa anga ili kuhakikisha inatumia fursa yake ya kijiografia kikamilifu.

“TPA hivi karibuni itafungua ofisi zake mjini Lubumbashi ambako wafanyabiashara hawatalazimika kusafiri mpaka Dar es Salaam kwa ajili ya kushughulikia utoaji wa mizigo yao,” alisema.

Pia aliitaka serikali ya nchi hiyo kuanzisha Kituo cha mizigo kitakachokuwa maalum kwa ajili ya shehena ya Kongo na kuongeza kwamba TPA tayari ilikuwa na eneo la ekari 110 jijini Dar es Salaam na ardhi katika bandari ya Kigoma ambazo Serikali hiyo inaweza kuomba kiasi itakachohitaji.

Akizungumzia usafiri katika Ziwa Tanganyika ambalo pia linatumiwa na nchi za Kongo na Burundi, Dk. Mwakyembe alisema njia rahisi ya kumaliza tatizo la usafiri katika Ziwa hilo ni kuanzisha Kampuni ya meli ya pamoja kati ya nchi hizo ambayo itamiliki na kuendesha meli ya abiria na mizigo na hivyo kurahisisha uchukuzi kupitia bandari za Kigoma na Kasanga.

Alisema Shirika la Reli Tanzania linatarajia kuanzisha huduma maalum ya usafirishaji shehena (Block Train) kati ya Dar es Salaam na Kigoma ambapo TPA itanunua vichwa vya treni na mabehewa kwa ajili ya huduma hiyo maalum ya reli.

“Wataalam kutoka pande zote mbili watakutana pamoja na kuweka mpango na ratiba ya utekezaji wa makubaliano yaliyofikiwa,” alisema.

Akizungumza katika kikao hicho, Waziri Kalumba alisema Serikali yake inathamini uhusiano mzuri uliopo kati ya nchi hizo mbili na kusema kwamba Wizara yake itahakikisha makubaliano yaliyofikiwa kati ya pande hizo yanafanyiwa kazi haraka iwezekanavyo.

“Hii ni fursa ya pekee kukuza biashara kati ya nchi zetu, tutafanya kila linalowezekana ili hili lifanikiwe,” alisema. 

Akiwa Lubumbashi waziri Mwakyembe alikutana na wafanyabiashara wa nchi hiyo wanaotumia bandari ya Dar es Salaam na kupokea maoni na malalamiko mbalimbali kutoka kwao.

Waziri aliwahakikishia wafanyabiashara hao kwamba atahakikisha kuwa dukuduku zao zinashughulikiwa ipasavyo na taasisi husika na kutaka Umoja wa Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA) kuhakikisha wanatoa matangazo ya orodha ya mawakala waliothibitishwa kuwa na uwezo wakufanya kazi hiyo kwenye tovuti na televisheni ili wafahamike kwa wafanyabiashara hao.

Katika ziara hiyo Waziri Dk. Mwakyembe aliongozana na viongozi na wawakilishi wa taasisi zilizo chini ya Wizara ya Uchukuzi pamoja na wawakilishi wa sekta binafsi ya uchukuzi.


Mwisho.

No comments: