Wednesday, March 5, 2014

DART yawatoa hofu watu wanaotaka kuomba zabuni za kutoa huduma

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART Agency) umewataka watu wanaotaka kuomba tenda za kutoa huduma katika mradi huo wa mabasi kuondoa wasiwasi kwa kuwa zabuni hizo zitatangazwa kwa uwazi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Bi. Asteria Mlambo aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa watu waondoe wasiwasi kwa vile zabuni hizo zitatangazwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Huduma zinazotarajiwa kutangazwa ni pamoja na watu wenye uwezo  wa kuwekeza katika mabasi, uwezo wa kukatisha tiketi, kukusanya nauli, na nyingine,”alisema Bi. Mlambo.
Alisema huduma hizo hazijatangazwa hivyo watu waondoe wasiwasi kwa vile zabuni zitawekwa wazi na kila mmoja mwenye sifa ataomba.
Pia alisema hadi sasa hakuna mtu ambaye tayari ameshateuliwa, hivyo watu waondoe dhana hiyo kwa vile taratibu zote zitafanyika kwa uwazi na bila kificho.
“Kuna baadhi ya watu wanawasiwasi hasa wamiliki wa daladala kuwa wamewekwa pembeni...hii si kweli,” alisema.
Alisema katika kufanikisha hilo, mwezi Mei mwaka huu wakala unatarajia kufanya mkutano kuwawezesha watanzania na watu kutoka mataifa mbalimbali kujionea fursa zilizopo kutokana na mradi huo.
Alisema tayari wakala umeshapata mtaalamu ambaye ni Kampuni ya Rebel Group  ambaye atafanya mchakato wote wa kupata watoa huduma hao katika mfumo huo mpya wa mabasi.
Mtaalamu huyo alisaini mkataba na wakala Januari 15 mwaka huu na wamesha andaa utaratibu wa namna ya kupata watoa huduma hao.
Kwa mujibi wa afisa huyo, mfumo wa mabasi haya unatarajia kukamilika mwaka 2015 na kuanza kutoa huduma zake kama ilivyopangwa.
Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanafuata sheria katika matumizi ya miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuchangia shughuli za maendeleo.
Vilevile wakala unahitaji ushirikiano kutoka mamlaka za Serikali za mitaa za jiji la Dar es Salaam hasa katika suala zima la utunzaji miundombinu vikiwemo vituo katika eneo la mradi.
Kwa muda mrefu pamekuwa na msongamano mkubwa wa magari na serikali inategemea kuwa mradi huo utasaidia kupunguza msongamano na foleni hizo.


Mwisho  

No comments: