Monday, March 31, 2014

EPZA yatoa leseni kwa kampuni mpya 13 za uwekezaji

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru (kulia) akimkabidhi leseni ya uwekezaji Mkurugenzi wa Rungwe Avocado Co. Limited, Bw. Joseph Mungai wakati wa hafla ya kukabidhi leseni za uwekezaji kwa kampuni mpya 13 mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA), Dkt. Adelhelm Meru (kulia) akimkabidhi leseni ya uwekezaji Meneja wa Fedha wa kampuni ya Fides Tanzania Limited, Bw. Wilhard Mlay wakati wa hafla ya kukabidhi leseni za uwekezaji kwa kampuni mpya 13 mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Katika juhudi za kuvutia uwekezaji Tanzania, Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) imetoa leseni za uwekezaji kwa kampuni mpya 13 ambazo zimewekeza katika sekta mbalimbali katika maeneo maalum ya mamlaka hiyo.

Hatua hii inakuja baada ya takribani miezi mitano ambapo chombo hicho kilitoa leseni kama hiyo kwa kampuni nyingine sita.

Maafisa wa EPZA wanasema hatua hiyo itasaidia kuimarisha viwanda nchini, kuongeza ajira na kuimarisha uchumi kwa ujumla.

Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka hiyo, Dkt. Adelhelm Meru aliwaambia waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam wakati wa hafla fupi ya kutoa leseni hizo kuwa bado Tanzania inahitaji wawekezaji ili kufikia malengo ya maendeleo iliyojiwekea na kuwa mamlaka yake itaendeleza juhudi za kuvutia wawekezaji hao.

“Tutaendeleza juhudi hizi kwa faida ya nchi yetu, nchi nyingi ambazo zimeendelea zimetumia njia hii kufikia maendeleo,” alisema.

Kwa mujibu wa Dk. Meru, kampuni hizo mpya zinatarajia kwa pamoja kuwekeza mtaji wa dola za Kimarekani milioni 62.2 na kutoa ajira takribani 3,500 kwa watanzania.  Pia kampuni hizo zinatarajia kuuza nje bidhaa zenye thamani ya dola milioni 61.86 kwa mwaka.

Alifafanua kuwa uwekezaji huo ni mkubwa na utachangia kujenga uchumi wa nchi kwa kiasi kikubwa.

Alisema kuwa katika juhudi za kuhamasisha uwekezaji katika kipindi cha miezi mitatu ya Januari hadi Machi mwaka huu wameweza kusajili makampuni hayo yakiwa yanatokea katika nchi mbalimbali na Tanzania ikiwa mojawapo.

“Leo katika jambo la kufurahisha kampuni sita zilizosajiliwa na kupatiwa leseni zinamilikiwa na watanzania jambo ambalo ni nzuri kiuchumi,” alisema.

Kampuni nyingine mbili ni za ubia kati ya watanzania na wageni wa nchi za Uturuki na Sweden na nyingine ni za wageni kutoka nchi za China, India, Uturuki, Uholanzi, Pakistan na Oman.

Alitaja kampuni zinazomilikiwa na watanzania kuwa ni  Rungwe Avocado Co. Limited, Basaliyu Textiles Limited, Polytex Africa Limited, Great African Food Company Limited, METL Motors Limited, and METL processing Limited.

Kampuni nyingine pamoja na nchi wamiliki ni pamoja na Amama Farms Limited (Sweden/Tanzania); Alkafil Company limited (Oman); Fides Tanzania Limited (Netherlands) na Tansan Investment Limited (Turkey/Tanzania).

Nyingine ni Wuzhou Investment Limited (China); Diamond Peal Company Limited (Pakistan); na Super Power Soap Industries (India).

Dk. Meru  alielezea kufurahishwa  na hatua ya watanzania kuamka na kuchangamkia fursa za  uwekezaji na kuongeza kusema kuwa hiyo itasaidia kuzidi kukuza uchumi wa nchi.

“Tunahitajika kuzidi kuwahamasisha wawekezaji wazalendo kuchukua nafasi zao katika jambo hili,” alisema.

Alisema kati ya kampuni alizozipatia leseni, saba ni za kusindika mazao ya kilimo na kuyaongezea thamani na kuwa hiyo ni moja ya hatua muhimu.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Rungwe Avocado Co. Limited, Bw. Joseph Mungai ambaye aliwahi kuwa Waziri alisema kupatiwa leseni hiyo ni hatua muhimu sana kwa kampuni yake.

“Tuna imani kubwa na mamlaka hii, tutafanya kazi kwa juhudi ili kutimiza lengo letu kama kampuni na nchi kwa ujumla,” alisema.

Naye Meneja wa Fedha wa kampuni ya Fides Tanzania Limited, Bw. Wilhard Mlay alisema kuwa wana matumaini ya kufanya vyema baada ya kupatiwa leseni hiyo.

“Hii ni hatua muhimu kwetu…tuna furaha,” alisema.

Mwisho


Wamiliki wa daladala watakiwa kujiandikisha DART

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka Dar es Salaam (DART) umewataka wamiliki wote wa mabasi ya abiria maarufu kama daladala ambao mabasi yao yanapita katika barabara ya Morogoro au kukatiza katika njia hiyo kufika katika ofisi zake kujiandikisha.

Mhandisi wa Wakala huo, Bw. John Shauri aliwaambia waandishi wa habari  jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuwa wamiliki hao wa daladala wanatakiwa kufika katika ofisi za DART zilizopo jengo la Ubungo Plaza barabara ya Morogoro eneo la Ubungo kuanzia tarehe 31 mwezi huu hadi tarehe 21 mwezi April mwaka huu kwa ajili ya kujiandikisha kama moja ya matayarisho ya kupisha mradi huo.

Kwa sasa wakala huo uko kwenye mchakato wa kuwezesha upatikanaji wa watoa huduma kwenye mfumo mpya wa mabasi yaendayo haraka awamu ya kwanza ambayo inajumuisha barabara ya Morogoro, Kawawa na mtaa wa Msimbazi kwa njia kuu na nyingine za kiungo. 
Alisema kulingana na mpango wa uendeshaji wa mfumo wa DART, barabara zinazohusika zitapaswa kutumiwa na mabasi ya mfumo huo pekee.
“Wakala umemwajiri mtaalamu mshauri ili kuwawezesha wamiliki wa daladala kuuelewa vizuri mfumo na kujipanga kuwa washiriki kwenye mfumo huu mpya,” alisema.
Kwa mujibu wa Bw. Shauri, jumla ya njia 64 zitakoma kutumika kutokana na kuanza kwa mradi huo.

Alitaja baadhi ya njia zitakazoguswa na zoezi hilo kuwa ni pamoja na Mbagala Rangi 3 kwenda Masaki, Vingunguti kwenda Makumbusho, Kunduchi Kwenda Mwenge, na Msata kwenda Ubungo.

Njia nyingine ni Kariakoo kwenda Makumbusho, Buguruni kwenda Kawe, Kivukoni kwenda Mburahati, Mbagala kuu kwenda Mwenge, na Mkata kwenda Ubungo.

Njia nyingine ni Mburahati kwenda Muhimbili, Segerea kwenda Mwenge, Vingunguti kwenda Kawe, Vingunguti kwenda Mbezi, Kunduchi kwenda Posta, na Kunduchi kwenda Makumbusho.

Pia alizitaja Temeke kwenda Masaki, Kivukoni kwenda Mabibo, Muhimbili kwenda Mabibo, Posta kwenda Ubungo, Posta kwenda Mabibo, Kawe kwenda Kimara, Kivukoni kwenda Mbezi, Mwenge kwenda Mbezi, Posta kwenda Mbezi, Mbezi kwenda Tegeta na Bunju kwenda Makumbusho.

Alisema wamiliki hao wa daladala wanahitaji kwenda na nakala ya leseni ya SUMATRA, nakala ya usajili wa gari, na nakala za rangi za leseni za madereva wao.

Uandikishaji utakuwa unafanyika kuanzia Jumatatu hadi Ijumaa asubuhi saa tatu mpaka saa 11 jioni.  Kwa siku za Jumamosi na Jumapili uandikishaji utakuwa unafanyika kuanzia saa tatu asubuhi mpaka saa nane na nusu mchana.

Naye Mshauri Elekezi wa Wakala huo, Bw. Felix Mlaki alisisitiza wamiliki hao kufika ofisi za DART kujisajiri na kufafanua kuwa daladala hazitasajiliwa tena na SUMATRA katika eneo la mradi huo.

“Tunawahitaji wajisajili na pia watoe mawazo yao juu ya kuanza kwa awamu ya kwanza ya mradi huu wa mabasi yaendayo haraka,”alisema Bw. Mlaki.

Alisema mradi huu ni wa kisasa na una manufaa makubwa kwa wananchi.

Alisema mfumo huo unatoa utaratibu mzuri wa ukataji tiketi na utoaji taarifa sahihi kwa abiria.


Mwisho

Tuesday, March 25, 2014

Watanzania washauriwa kujenga utamaduni wa kusoma, kuandika vitabu

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Watanzania wameshauriwa kujenga utamaduni wa kusoma vitabu ili kuchota maarifa mbalimbali na kuwasaidia katika kufanya shughuli mbalimbali za maendeleo.

Wito huo ulitolewa na mwandishi wa vitabu, Bw. Evodius Katare ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Utawa na Fedha wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo haraka (DART) akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam.

“Watanzania wakijenga utamaduni huu wa kusoma vitabu itawasaidia sana kimaisha,” alisema na kuongeza kuwa kusoma vitabu ni kuchota maarifa mbalimbali kutoka kwa waandishi.

Akitoa mfano alisema watu wakipenda kusoma vitabu pia watapenda kuandika vitabu ili wengine waweze kusoma.
Alisema yeye anapenda kusoma vitabu na utamaduni huo umemsaidia pia kuwa na tabia ya kuandika vitabu.

“Tabia ya kusoma vitabu imenisaidia kuwa mwandishi wa vitabu japo taaluma yangu siyo mwandishi,” alisema.

Kitabu chake kipya kinaitwa “Julius Nyerere, Falsafa zake na dhana ya Utakatifu.”

Alisema ameandika kitabu hicho kutokana na Kanisa Katoliki kutangaza mchakato wa kumfanya Baba wa taifa, Mwalimu Nyerere kuwa mtakatifu na uelewa mdogo wa jamii hasa vijana kuhusu mchango wake kwa taifa hili.
Anaungana na kanisa hilo kwa kutaka kumpatia zawadi hiyo kubwa Nyerere na kwamba anastahili kuipata kutokana na matendo yake ya uongozi aliyoifanyia nchi hii.

“Mwalimu Nyerere alikuwa mwanasiasa na kiongozi aliyeifanya jamii ya watanzania kuwa sehemu ya familia yake na hiyo ikawa tunu kwenu ya uwepo wa amani na utulivu,”alisema Bw.Katare.

Alisema katika kipindi chote cha uhai wake alitumia muda wake kuwatumikia watanzania, aliongoza harakati za kuikomboa nchi na pia aliliongoza taifa kwa uadilifu baada ya uhuru.

Alisema kitabu hicho kitaiwezesha jamii hasa vijana ambao hawakuishi kipindi cha Mwalimu kumfahamu ili wawe na fursa nzuri wanapotaka kumfananisha na wanasiasa wanaojitokeza leo ambao wengi wanajali familia na maslahi yao tu.

Alieleza kuwa watu wasome kitabu chake hicho ili  waweze kumfahamu zaidi mwalimu Nyerere na mchango wake kwa taifa hili.

“Kitabu hiki kitasaidia pia vizazi vijavyo kufahamu historia nzuri juu ya Mwalimu Nyerere,”alisema Bw.Katare

Alisisistiza kwamba tabia ya kusoma na kuandika vitabu hujengwa tangu awali vijana wakiwa wadogo katika mashule.

Alisema kuna kila sababu ya Tanzania kujenga maktaba shule zote za msingi na sekondari na kuwa na walimu wa kuhamasisha wanafunzi kusoma vitabu ili kuwa na jamii bora zaidi.


Mwisho.