Monday, August 13, 2012

Serikali yatakiwa kulinda tamaduni za makundi ya watu waishio kiasili


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Serikali  imeshauriwa kulinda tamaduni za makundi ya watu wanaoishi kiasili wa makabila ya wafugaji, wawindaji na wakusanyaji matunda na kuwafikishia huduma za maendeleo katika maeneo yao.

Ushauri huo umetolewa na Mdhamini Mtendaji (Executive Trustee) wa Flame Tree Media Trust, Bw.Mwanzo Millinga katika maonyesho ya picha yaliyolenga kuonyesha utamaduni wa kabila la wamasai katika maadhimisho ya siku ya watu waishio kiasili duniani mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.

“Nchi yetu inatakiwa kutambua umuhimu wa utamaduni wa wamasai na makabila mengine yanayoishi kiasili na kuthamini mila na desturi zao katika mavazi, chakula na maisha ya kuhamahama kulingana na shughuli zao,”alisema Bw. Millinga.

Alisema Umoja wa Mataifa na Umoja wa Afrika unatambua uwepo wao na kuamua kutenga siku yao hivyo kuna kila sababu Tanzania kuwapatia haki zao na kuwathamini kwa kuwafikishia huduma za msingi za maendeleo.

Alisema utamaduni wa wamasai na makabila kama ya Wabarbaig, na wahadzabe unatofautiana na makundi ya makabila mengine yaliyopo nchini lakini thamani yake ni kubwa kitaifa hivyo ni wajibu wa serikali kulinda haki zao.

Alisema katika mazingira ya sasa makabila hayo yanakabiliwa na tatizo la ardhi kwa ajili ya malisho ya mifugo, uwindaji na utafutaji matunda kutokana na kushamiri kwa uwekezaji ambapo ardhi yao huchukuliwa bila kujali mahitaji.

Alisema maonyesho hayo yamefanyika kupitia picha ambazo waliwapiga wamasai wakiwa katika utamaduni wao ambao ni kivutio kikubwa kwa watu mbalimbali wa ndani na nje ya nchi walioshiriki katika maadhimisho ya siku ya watu waishio kiasili duniani hapa nchini.

Balozi wa Uholanzi hapa nchini Dkt.Ad Kaekkoek alisema tamko la Umoja wa Mataifa la haki za watu ashio kiasili (UNDRIP) linazitaka nchi mbalimbali duniani kusherehekea siku hiyo muhimu kwa ajili ya kulinda haki zao.

Alisema ubalozi wa Uholanzi nchini Tanzania na Umoja wa Nchi za Ulaya wameshirikiana na mpigapicha wa kimataifa Bw. Millinga kuonyesha utamaduni wa kundi la watu waishio kiasili ili kusaidia kuleta msukumo wa kulinda haki zao na utamaduni wao.

Picha hizo zinaonyesha vijana wa Kimasai wa maeneo mbalimbali yakiwemo ya Simanjiro na Manyara katika utamaduni wao wa vyakula, nyumba, na pia changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Tanzania ilipigia kura tamko la Umoja wa Mataifa la haki za watu waishio kiasili mwaka 2007 lakini bado haina sera au sheria inayowalinda kupata haki zao zikiwemo za kupata ardhi ya kutosha na kufaidika na rasilimali zao.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mtandao wa Mashirika ya Wafugaji, Wawindaji na Wakusanyaji Matunda,Bw.Edward Porokwa alisema kundi la watu wa kabila la Wamasai linatambuliwa na jumuiya za kimataifa kuwa ni moja ya makundi ya pembezoni.

Alisema makundi ya watu wa Kimasai,Wahadzabe Wabarbaig ni makundi yaliyo nyuma kimaendeleo kuanzia kipindi cha ukoloni na sasa wakati umefika kwa ajili ya kuwapatia haki na kutotengwa na rasilimali zao.

Tanzania ina makabila kati ya 125 hadi 130 yaliyogawanyika katika makundi manne ya wabantu,Wakushite,Wanile-Hamiti na Wasan.

Maonyesho hayo yaliandaliwa na Flame Tree Media Trust kwa msaada wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Ubalozi wa Uholanzi nchini na Umoja wa watu wanaozungumza Lugha ya Kifaransa Dar es Salaam (Alliance Francaise Dar es Salaam).

Mwisho

No comments: