Monday, August 13, 2012

Benki ya Afrika Tanzania yaongeza faida


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Benki ya Afrika Tanzania imeongeza faida yake mara mbili kufikia nusu ya mwaka huu 2012 kulinganisha na kipindi hicho kwa mwaka 2011.
Taarifa ya fedha ya iliyotolewa hivi karibuni benki hiyo imepata Tshs 551 milioni katika robo ya mwaka inayoishia mwezi Juni 2012 kulinganisha na kiasi cha Tshs 273 milioni kilichorekodiwa katika kipindi hicho mwaka jana.
Kwa mujibu wa Mkuu wa Idara ya Fedha wa benki hiyo, Bw. Mussa Mwachaga faida iliyopatikana kutokana na riba ni Tshs 4 bilioni katika robo ya mwaka inayoishia mwezi Juni 2012 kulinganisha na kiasi cha Tshs 3 bilioni kilichorekodiwa katika kipindi hicho mwaka jana. 
Amesema benki imerekodi faida inayotokana na riba ya Tshs 8.2 bilioni katika kipindi kinachoishia Juni mwaka huu ukilinganisha na Tshs 5.7 bilioni zilizorekodiwa katika kipindi kama hicho mwaka jana.
Benki ya Afrika Tanzania imekuwa ikijitahidi kujitanua na kuimarisha huduma zake katika miaka ya hivi karibuni.
Tangu ianzishwe hapa nchini mwaka 2007, imeshafanikiwa kufungua matawi kumi mkoani Dar es Salaam na sita nje ya mkoa huo yakiwepo ya Morogoro, Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya and Arusha.
Benki hii ni moja ya mtandao wa kibenki unaofanya kazi katika nchi 15 ambazo ni pamoja na Benin, Burkina Faso, Ghana, Ivory Coast, Mali, Niger na Senegal.  Nyingine ni Burundi, Djibouti, Kenya, Madagascar, Tanzania na Uganda.

Pia ina tawi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.

Mwisho

No comments: