Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Baada ya kufanya vizuri kitaifa katika
maonesho ya wakulima Nanenane, Asasi ya kusaidia uwekezaji katika kilimo nchini
(PASS) imesema ushindi huo utakua chachu kwao kuendelea kujiimarisha zaidi ili
kuwafikia wananchi wengi.
Katika maonyesho ya
mwaka huu, Asasi hiyo ilishiriki katika mikoa mitatu ya Dodoma, Mbeya na
Morogoro na kushinda katika mikoa yote .
Wakati katika mkoa wa Dodoma PASS ilishika nafasi ya pili
katika kipengele cha asasi zisizo za kiserikali; mkoani Morogoro ilishika
nafasi ya kwanza katika kipengele cha huduma za kifedha na kushika nafasi ya
pili katika huduma za kilimo mkoani Mbeya.
Akiongea na waandishi wa habari mwishoni
mwa wiki mjini Dodoma, Mkurugenzi Mtendaji wa PASS, Bw.Iddy Lujina alisema hatua
hiyo inakusudia kuwakomboa wananchi kupitia kilimo ikiwa pia ni njia
mojawapo ya kukuza uchumi wa nchi na kuongeza pato la taifa kupitia sekta hiyo.
“Tumedhamiria kuwafikia wakulima wengi
zaidi ifikapo mwishoni mwa mwaka huu, hii ikiwa ni pamoja na kuendelea kufungua
matawi katika mikoa
mbalimbali hapa nchini ili kuwaendeleza wakulima wengi zaidi,” alisema Lujina.
Aliongeza kuwa ushindi walioupata utakuwa
chachu ya wao kuendelea kujitanua zaidi na kuongeza kasi ya kuendelea
kuwasaidia wakulima wengi nchini ili waweze kuendana na mkakati wa serikali wa
Kilimo Kwanza na ule wa ukuaji wa kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania
(SAGCOT).
“Siku zote tumekuwa katika mikakati
madhubuti ya kuhakikisha kilimo katika nchi hii kinakuwa na kuimarika zaidi,
tutaendelea na juhudi hizi kwa faida ya wakulima na nchi nzima kwa ujumla,”
aliongeza.
Akielezea zaidi alisema siku zote PASS
imekuwa ikifanya kazi kwa karibu na serikali yetu katika kuendeleza kilimo
katika nchi hii hasa katika kupeana ushauri wa kitaalamu wa kuwafikia wakulima
katika maeneo yao na kufanya nao kazi.
Kwa upande wake, mmoja wa waliofaidika na
PASS, Bw. Papian Emmanuel ameishukuru kwa kuwajali wakuliama wa nchi hii, huku
akizitaka taasisi zinazohusika na utoaji wa mikopo kwa ajili ya kilimo kukiona
kilimo kama eneo linalofaa kufanya nalo kazi.
“Taasisi nyingine zinatakiwa kuiga mfano wa
PASS katika juhudi zao wanazofanya kuwafikia wakulima wengi hapa nchini, kutoa
ushauri na kusaidia wakulima wadogo wadogo kupata mikopo,” alisema Bw.
Emmanuel.
Asasi hii ilianzishwa mwaka 2000 ili
kuwawezesha wakulima wapate huduma za mabenki. Mpaka sasa imeshaidia wakulima 60,000
kupata mikopo yenye thamani ya Tshs 100 bilioni.
Kwa mujibu wa Bw. Lujina mwaka 2011
wakulima 11,000 pamoja na vikundi 524 waliwezeshwa
kupata mikopo ya Tshs 28 bilioni.
Pamoja na mpango wa upanuzi wa asasi hiyo
katika mikoa ya Kilimanjaro na Mtwara mwaka huu, asasi hiyo inatarajia
kuwezesha wakulima wapate mikopo zaidi ya Tshs 300 bilioni kwenye miaka minne
ijayo.
Kwasasa asasi hiyo ina ofisi katika mikoa
ya Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya na Mwanza.
Ends
No comments:
Post a Comment