Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Hafla ya chakula cha hisani ya kuchangia
fedha kwa ajili ya kujenga vyoo vya umma katika barabara kuu za Tanzania sasa
itafanyika mwishoni mwa mwezi ujao, Novemba.
Rais Jakaya Kikwete anatarajiwa kuwa mgeni
rasmi katika hafla hiyo.
Mwenyekiti Mtendaji wa Shirika la
Mazingira Mufindi (MUET), Bw. Godifrey Mosha aliwaambia waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam kuwa chakula hicho kinalenga kuchangisha fedha kwa
ajili ya ujenzi wa vyoo hivyo katika barabara kuu tatu ziendazo mikoani.
“Tunatarajia kujenga vyoo hivyo katika
barabaraza zetu kuu ziendazo mikoani,” alisema,”alisema Bw. Mosha.
Alisema kwa sasa mazingira ya abiria
kupata falagha ya kujisaidia barabarani siyo nzuri kwani watu huchimba dawa
porini jambo ambalo siyo nzuri kiusalama na husabisha uharibifu wa mazingira.
Barabara zitakazo jengewa vyoo hivyo ni
pamoja na Dar es Salaam-Songea; Mwanza-Dar es Salaam; na Mtwara-Dar
es Salaam ambapo awamu ya kwanza itaanza na barabra ya Songea kwenda Dar es
Salaam ikiwa na vituo vitano.
Alisema michoro yake imekamilika na
inaonyesha umbali wa choo kimoja kwenda kingine na kila choo kitakuwa na
matundu hamsini, wanawake 25 na wanaume 25 na cha walemavu na pia sehemu za
kuvutia sigara na kutupa takataka.
Awali, chakula hicho cha hisani kilikuwa
kifanyike kesho, Alhamis. Hafla hiyo imesogezwa mbele ili kuleta
ufanisi zaidi.
Alitoa wito kwa wadau wote wa mazingira
wakiwemo wasafirishaji na watu mbalimbalimbali wazidi kuchangia ili kuzidi
kukamilisha shughuli hiyo muhimu kwa maendeleo.
“Vituo hivi vina maana sana kwa abiria na
kwa wananchi wa vijiji vya karibu,” alisema na kuongeza kuwa ajira zitazalishwa
na kufanya biashara kujiongezea vipato vyao kuendesha maisha yao.
Aliongeza kusema kuwa maendeleo yanakuja
kwa wananchi kuwa wabunifu na kushirikiana katika maswala mbalimbali ya
kijamii.
Alisisitiza kwamba mwasisi wa taifa hili,
Mwalimu Julius Nyerere aliliandaa taifa vizuri na kuliacha likiwa na hali
nzuri, hivyo ni vyema sasa kufanya kila liwezekanalo kuzidi kuliendeleza.
Chakula hicho cha hisani kitaandaliwa na
MUET kwa kushirikiana na wadu mbalimbali.
Wachangiaji watapatiwa vyeti vya
kutambuliwa.
Mwisho.