Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wawekezaji kutoka nchini China wameshawishiwa kuwekeza
katika maeneo ya Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA) ambayo
yameshatengwa kwa ajili hiyo katika mikoa mbalimbali.
Mkurugenzi Mkuu wa EPZA, Dr. Adelhelm
Meru alitoa wito huo wakati alipokuwa akitoa mada kuhusu maeneo maalum ya
uwekezaji Tanzania na mamlaka yake wakati wa kongamano la pili la biashara kati
ya Tanzania na China lililofanyika jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
“Tunawakaribisha muwekeze katika maeneo huru ya
uwekezaji Tanzania,” alisema.
Akitoa mfano, Dk. Meru alisema kuwa serikali tayari
imetenga jumla ya hekta 22,000 katika eneo la uwekezaji Bagamoyo na kuwa
anawahimiza wawekezaji toka nchi hiyo kuja kuwekeza katika eneo hilo.
“Tunataka eneo hili kuwa la viwanda na kituo cha
biashara,” alisema.
Alisema kuwa serikali kwa kushirikiana na sekta
binafsi iko mbioni kuendeleza miundombinu katika eneo hilo na kuwa sasa ni
wakati muafaka kwa wawekezaji kuja na kutekeleza adhma yao.
Alisema kuwa bandari kubwa nchini itajengwa katika eneo
hilo na kuwa itabadilisha kwa kiwango kikubwa muonekano wa Bagamoyo.
Katika mpango pia ni kiwanja cha ndege cha kisasa na
reli itakayounganishwa na ile ya kati na TAZARA.
EPZA imetenga maeneo huru na maalumu ya uwekezaji katika
mikoa 20 yakiwa na ukubwa wa hekari 500-9,000 kila moja.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Maendeleo ya Viwanda wa
muungano wa wafanyabiashara, viwanda na kilimo (TCCIA) Mr.Adam Zuku alisema
kuwa watanzania wananatakiwa kuzidisha ujuzi na taaluma ili kuweza kushirikiana
kati ya nchi hizo mbili.
“Elimu na ujuzi mbalimbali utatuwezesha kushirikiana
vyema na wawekezaji kutoka nje na kufaidika,” alisema.
Hivi karibuni, EPZA ilisaini makubaliano na Benki ya
Maendeleo Tanzania (TIB) kwa ajili ya kupata mikopo ya kujenga miundombinu
itakayovutia wawekezaji kuanzisha viwanda katika maeneo yake maalumu.
Makubaliano hayo yalilenga kuendeleza maeneo ya
mamlaka hiyo yaliyosambaa pote nchini.
Kupitia makubaliano hayo maeneo maalumu ya uwekezaji
kama Bagamoyo, Mtwara, Kigoma, Tanga na mengine yote yaliyo katika mikoa 20
yatapata miundombinu itakayovutia wawekezaji wa ndani na nje.
Kongamano hilo lilishirikisha kampuni zaidi ya 100
kutoka China na kampuni zaidi ya 120 za kitanzania.
Hadi sasa China imesajili miradi 522 TIC yenye thamani
ya dola za Kimarekani bilioni 2.4 ambayo inatarajiwa kuzalisha ajira 77,335.
Kongamano hilo la siku tatu liliandaliwa na TIC kwa
kushirikiana na Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa na Baraza la
Biashara China Afrika (CABC) na kudhaminiwa na Stanbic Bank Tanzania.
Mwisho