Rais
wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Jakaya Mrisho Kikwete ( wa pili kulia)
akisikiliza maelezo kutoka kwa mkurugenzi wa Mamlaka ya maji Mkoani Arusha ( AUWSA)
mhandisi Ruth Koya wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa
maji safi na salama katika mji wa Karatu mkoani Arusha hivi karibuni, mwisho
kulia ni Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe, wengine katika picha ni mkuu
wa mkoa wa Arusha Bw. Magesa Mulongo wa tatu kulia.
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia)
akimtwisha ndoo ya maji Joan Israel, muda mfupi mara baada ya kuzindua hatua ya
kwanza ya mradi wa upatikanaji wa maji safi na salama katika mji wa Karatu
mkoani Arusha hivi karibuni, anaeshuhudia ni Waziri wa maji Profesa Jumanne
Maghembe.
Rais
wa Jmahuri ya Muungano wa Tanzania DKT. Jakaya Mrisho Kikwete (kulia)
akifurahia jambo na Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe mara baada ya
kufungua maji wakati wa sherehe fupi za uzinduzi wa hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa
maji safi na salama katika mji wa Karatu mkoani Arusha hivi karibuni, katikati
ni Mkurugenzi wa Mamlaka ya maji mkani Arusha ( AUWSA) mhandisi Ruth Koya.
Na Mwandishi Wetu, Karatu.
Hatua ya kwanza ya mradi wa upatikanaji wa
maji katika mji wa Karatu jijini Arusha umefikia asilimia 34, huku
shilingi milioni 310 zikihitajika kukamilisha hatua hatua hiyo, ambapo mradi
mzima ukitarajia kugharimu sh.mil 620.7.
Waziri wa maji Profesa Jumanne Maghembe
aliyasema hayo Wilayani Karatu, jijini Arusha wakati alipokuwa akizungumza na
mwandishi wa gazeti hili juu ya mpango wa ukamilishaji wa miradi ya maji katika
baadhi ya maeneo ya miji midogo na mikubwa hapa nchini.
“Fedha hizo kwa ajili ya kukamilisha awamu ya
kwanza ya mradi huo, tutazitoa kabla ya mwaka huu wa fedha haujaisha ili
kumaliza awamu hiyo,” alisema Waziri wa maji.
Alisema kuanzia mwaka wa fedha unaokuja 2014
– 2015 wizara itahakikisha kwamba mradi unapanuliwa kufikia upande wote wa
magharibi wa mji huo.
Aliongeza kuwa hadi kufikia mwakani mwezi wa
4 mji wa Karatu na maeneo ya jirani hakutakuwa na shida ya maji kama mwaka
2013.
“ Nawahakikishia wananchi wa Karatu kuwa
ifikapo mwaka 2015 mwezi kama huu hawatakuwa na upungufu wa maji tena”
aliongeza.
Mji huo wenye wakazi 42, 000 unahitaji
takribani lita 4,000, 000 kwa siku ambapo kwa sasa upatikanaji wa maji ni lita
850, 000 ambazo hazitoshelezi mahitaji ya wananchi wa mji huo.
Alisema baada ya kuchimbwa kwa visima viwili
katika mji huo kutapunguza adha hiyo kwa kiasi kikubwa kwa wananchi wa Karatu.
Alisema uendelezaji wa awamu ya pili ya mradi
huo ni kuongeza uchimbaji wa visima pamoja na kujenga matenki kwa ajili ya
kuhifadhia maji katika maeneo ya Karatu magharibi na eneo la G. lambo.
“Katika awamu hii ya pili zaidi ya shilingi
mil.700 zitahitajika ili kufanikisha kukamilisha awamu hii,” alisema.
Baadhi ya wakazi wa mji wa Karatu wamesifu
hatua hiyo ya serikali kupitia wizara ya maji kuwa wananchi wa Karatu sasa
watakua wamekombolewa katika adha kubwa iliyokuwepo awali.
“Hii ni kama neema kwetu kwa kweli serikali
imetujali sana ,” alisema Joseph Macha.
Aliongeza kuwa kwa muda mrefu wamekuwa katika
tabu, wakina mama walikuwa wakifuata maji umbali mrefu, hivyo kuzorotesha shughuli
nyingine za kimaendeleo.
Nae Joan Israel alisema wakina mama wa Karatu
sasa watakuwa na nafuu ya kuamka asubuhi kutafuta maji, kwani kilichofanywa na
wizara ni kitendo kinachoonyesha kuwa serikali inawajali wananchi wake.
“ mimi niseme tu kwamba, Mungu awabariki hawa
viongozi wetu, Rais Kikwete pamoja na waziri wa maji Jumanne Maghembe wamefanya
kazi kubwa kuwaokoa kina mama wa Karatu,” alisema.
Mwisho.