Thursday, February 27, 2014

TPA yazihamasisha nchi jirani kuzidi kutumia bandari ya Dar es Salaam

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Bandari Tanzania (TPA) imezihamasisha nchi jirani kuzidi kutumia bandari ya Dar es Salaam kwani sasa huduma zake zinaimarika kutokana na maboresho makubwa yanayoendelea kufanywa.

Kaimu Meneja Mawasiliano wa TPA, Bi. Janeth Luzangi amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa sasa ufanisi wa bandari hiyo unazidi kuwa wa kisasa na haraka.

“Maboresho yanayofanywa na mamlaka yanazaa matunda hivyo nchi jirani zizidi kutumia bandari yetu ili wapate thamani halisi ya pesa yao,” alisema.

Akielezea zaidi alisema bandari ya Dar es Salaam katika mwaka 2012/13 ilihudumia shehena ya jumla ya tani milioni 12.5 ukilinganisha na tani million 10.9 zilizohudumiwa mwaka 2011/12, ikiwa ni ongezeko la asilimia 15.0.

Katika shehena yote iliyohudumiwa mwaka 2012/13, shehena ya nchi zitumiazo bandari  ilikuwa tani million 4, ambayo ni asilimia 32 ya shehena yote.

Jitihada zinazoendelea kufanywa na Mamlaka pamoja, wadau wa bandari  na serikali katika kuimarisha njia kuuza usafirishaji za reli, na barabara na kupunguza vikwazo vya biashara.

“Hii itasaidia sana kuimarisha huduma ya ndani na nchi jirani,” alisema na kuongeza kuwa jitihada za kimasoko zinafanywa na Mamlaka na wadau wengine kuvutia wateja ikiwa ni pamoja na kuboresha utendaji kazi wa bandari.

Akitoa takwimu zaidi, Bi. Luzangi alisema shehena yote ya mizigo ya nchi 6 zitumiazo bandari ya Dar es salaam, (yaani Zambia, D R Congo, Burundi, Rwanda, Malawi na Uganda) imeongezeka kutoka tani millioni 3.55 mwaka 2011/12 hadi kufikia tani millioni 4.05 mwaka 2102/13, hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 14.2.

“Ongezeko hilo ni kutokana na kuendelea kukua kwa uchumi wa nchi hizo na vile vile mazingira mazuri ya biashara humu nchini Tanzania na uboreshaji wa huduma katika bandari ya Dar es Salaam,” alisema.

Akizungumzia ushindani, alisema bandari ya Dar es Salaam iko katika nafasi nzuri zaidi ya ushindani kulinganisha na bandari nyingine katika eneo hili la Afrika kutokana na eneo zuri kijiografia na kuwa nchi inafanya kila kinachotakiwa ili kufanya vizuri.

Katika miaka ya hivi karibuni pamekuwepo na mikakati mbalimbali inayofanywa na serikali kupitia Wizara ya Uchukuzi, TPA pamoja na wadau wengine kuhakikisha kuwa bandari ya Dar es Salaam inatoa huduma bora kwa wateja wa hapa nchini pamoja na wale wan chi jirani.

Kutokana na mikakati hiyo pamekuwepo na ongezeko la shehena, tija katika kuhudumia shehena na meli zinazotumia bandari hiyo, na kupungua kwa msongamano wa meli.

Pia kumekuwepo na punguzo kubwa la mrundikano wa mizigo na kufanikiwa kukomesha vitendo vya upotevu wa mizigo na wizi kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano, kwa upande wa mapato, mwaka 2012/13 wastani wa Tshs bilioni 371.7 zilikusanywa, sawa na ongezeko la asilimia 14.3 ukilinganisha na Tsh. bilioni 325.3 mwaka 2011/12.

Katika mapato hayo, bandari bila ya makusanyo ya TICTS, ilikusanya Tsh.bilioni 324.5 mwaka 2012/13, ikiwa ni ongezeko la asilimia 18.9, ikilinganishwa na mapato ya Tsh.bilioni 272.9 mwaka 2011/12.

Kwa mujibu wa afisa huyo, matukio ya uhalifu na wizi yamepungua sana kutoka matukio 21 mwaka 2011 hadi matukio 7 mwaka 2012, na kufikia matukio 3 mwaka 2013.

Alisema hali hiyo imetokana na mikakati mbalimbali inayochukuliwa na mamlaka ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kisasa katika udhibiti wa uingiaji bandarini, uboreshaji wa miundombinu, mafunzo kwa askari na dhana ya ulinzi shirikishi kwa wafanyakazi na wateja.


Mwisho

EPZA: Bagamoyo kuwa jiji kubwa la kisasa la viwanda na biashara

Mkurugenzi wa Uhamasishaji na huduma  wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Bi.Zawadia Nanyaro  akitoa mada juu ya eneo maalumu la uwekezaji la mamlaka hiyo lililopo katika mji wa Bagamoyo wakati wa mkutano na wafanyabiashara wa mji wa Vallejo uliopo Jimbo la California nchini Marekani na wale wa mji wa Bagamoyo jana.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Huduma wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Bi.Zawadia Nanyaro (kulia) akimkaribisha Meya wa Mji wa Vallejo uliopo Jimbo la California nchini Marekani, Bw. Osby Davis, wakati alipofanya ziara ya kutembelea eneo maalumu la uwekezaji la mamlaka hiyo lilolopo katika mji wa Bagamoyo jana.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Huduma wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Bi.Zawadia Nanyaro (kushoto) akimmwonyesha eneo maalumu la Uwekezaji la mamlaka hilo lililopo Bagamoyo Meya wa Mji wa Vallejo uliopo Jimbo la California nchini Marekani, Bw. Osby Davis (kati) na  Rais na Ofisa Mkuu Mtendaji wa Globetrend Group kutoka mji huo Bw.Edem Elvis Akpokli  (kulia)jana.
Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Huduma  wa Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji nchini (EPZA), Bi.Zawadia Nanyaro kati akiwafafanulia jambo wafanyabiashara wa Mji wa Vallejo uliopo Jimno la California nchini Marekani wakati walipofanya ziara ya kutembelea eneo maalumu ya mamlaka hiyo lililopo katika mji wa Bagamoyo jana.
Na Mwandishi wetu, Bagamoyo
Mamlaka ya Ukanda Maalumu ya Uwekezaji (EPZA) imesema mradi wa uendelezaji wa maeneo maalumu ya uwekezaji katika mji wa Bagamoyo ukikamilika utasaidia mji huo kuwa jiji kubwa la viwanda na biashara na kuchangia shughuli za maendeleo ya nchi.

Mkurugenzi wa Uhamasishaji na Huduma wa Mamlaka hiyo, Bi. Zawadia Nanyaro, aliuambia  ujumbe wa wafanyabiashara  kutoka mji wa Vallejo uliopo Jimbo la California nchini Marekani ambao ulifanya ziara kwenda kujionea fursa mbalimbali za kibiashara katika eneo hilo  kuwa mji wa bagamoyo utakuwa wa viwanda na biashara.

“Serikali imetenga eneo la hekali 22,000 sawa na heka 9,000 katika eneo hili maalumu la uwekezaji hapa Bagamoyo na tunahamasisha wawekezaji kama wa mji wa Vallejo kuja kuwekeza hapa,” aliuambia ujumbe huo ambao umeongozwa na Meya wa Vallejo, Bw.Osby Davis.

Bi. Nanyaro alisema kwa sasa serikali inayomipango ya kujenga miundombinu mbalimbali kwa kushirikiana na sekta binafs, hivyo wafanyabiashara hawanabudi kuchangamkia fursa hiyo kwa kuanzisha viwanda na biashara na huduma mbalimbali.

“ Mji wa Bagamoyo kutokana na eneo maalumu la  uwekezaji kutajengwa bandari kubwa ya kisasa kupita zote nchini ili kuunganisha na maeneo mengine ya nchi na nje ya nchi,” alisema mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa  Bagamoyo itakuwa ni kiungo kikubwa kwa biashara nchini.

Alisema kuna  mradi pia wa kujenga uwanja wa ndege wa kisasa na reli itakayounganishwa na reli ya kati na Tazara na miundombinu yote hiyo inalenga kuweka mazingira bora ya kibiashara na uwekezaji.

Ugeni huo wa  wafanyabiashara hao kutoka mji wa Vallejo walitembelea maeneo hayo ya uwekezaji likiwemo eneo la heka 300 la Kamal Industrial Estate linalomilikiwa na mtu binafsi.

“ Ujumbe wa wafanyabiashara hawa wengi wao walionyesha kufurahishwa na serikali ya Tanzania ya kutenga maeneo kama hayo kwa ajili ya viwanda na biashara,” aliongeza mkurugenzi huyo na kuongeza kuwa  wako tayari kuja nchini  ili kuitumia fursa waliyoiona Bagamoyo kwa ajili ya maendeleo ya nchi hizi mbili.

Naye Mwenyekiti wa Black Chamber of Commerce na Mkurugenzi Mtendaji wa chamber hiyo ya Mji wa Vallejo,Bw. Carl Davis, Jr  alisema wao wanahitaji kufanya biashara katika mji  wa Bagamoyo kwa faida ya miji hiyo miwili.

“Hii ni fursa kwetu kuja kufanyabiashara hapa Bagamoyo iwe ya ushirikiano kati yetu sisi zote au kuja kuwekeza mojakwamoja sisi wenyewe,” alisema Bw. Davis, Jr na kuongeza  kuwa shughuli za biashara zikiimarishwa zitasaidia sana mji wa Bagamoyo.

Alisema ujio wao umelenga kuona fursa zilizopo katika mji wa Bagamoyo na pia wanapenda kuwekeza katika sekta mbalimbali ikiwemo ya kilimo.
Bw. Davis, Jr alisema wafanyabiashara wa mji wao wanamahusiano mazuri ya kibiashara na nchi za Afrika na tayari wanafanya biashara katika nchi ya Ghana, Kenya na Misri na matarajio yao kuingia Bagamoyo.

“Sisi tumejidhatiti kufanya biashara hapa na ziara yetu imetuunganisha na nyie na tutaenda kuwa mabalozi wazuri juu ya fursa za Bagamoyo na tutarudi tena kibiashara zaidi,” alisisitiza.

Alisema pia mji wao wa Vallejo na Bagamoyo ni miji dada na mahusiano yaliyopo yanalenga kuendeleza mahusiano hayo na  kuingia zaidi katika biashara.

Mwisho .