Monday, May 6, 2013

Kampuni kubwa nchini zatajwa kuwa muhimu katika kuimarisha sekta binafsi


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Muda wa kuunganisha nguvu na kuwa sauti moja ya sekta binafsi ili kuleta maendeleo endelevu ya kiuchumi na kijamii ni sasa.

Akiongea kwa niaba ya Mwenyekiti wa taasisi ya sekta binafsi Tanzania, Bw. Arnold Kileo amesema ni muda muafaka sasa kwa sekta binafsi kuungana na kuwa na sauti moja hasa katika kipindi hiki ambapo panagundulika raslimali nyingi hapa nchini.

Bw. Kileo ambae pia ni mjumbe wa bodi ya TPSF alisema hayo katika kikao kilichofanyika jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki na kujadili jinsi ya kutekeleza maoni ya kuunda bodi mpya ya TPSF chini ya mfumo wa kongano pamoja na kuangalia jinsi ya kuchagua wawakilishi katika bodi hiyo.

Kikao hicho kilihusisha wadau toka makampuni makubwa nchini ambayo pia yatakua na uwakilishi katika bodi hiyo mpya.

Bw. Kileo alisema kuhusishwa kikamilifu kwa sekta binafsi katika maendeleo ya nchi kwa sasa ni muhimu sana hasa kipindi hiki ambapo watu wengi wanaangalia raslimali za Tanzania kwa karibu wakitaka kuzichuma na kuondoka zao.

“Lazima tuhakikishe kuwa raslimali za nchi zinafaidisha nchi na watu wake kwa utaratibu unaokubalika huku pia wawekezaji wakifaidika kulingana na makubaliano yanayoeleweka,” alisema.

Aliongeza kuwa sekta binafsi ina nafasi nzuri na kubwa kuishauri serikali jinsi bora ya kufanya nchi ifaidike na raslimali za madini, gesi na mafuta ambazo zinaendelea kugundulika kwa wingi hapa nchini.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye alisema utaratibu mpya wa kongano unataka kuhakikisha kuwa sekta binafsi inakua yenye nguvu na kutoa mchango mkubwa zaidi katika maendeleo.

Alisema kuhusisha kampuni kubwa kubwa katika mfumo huu mpya ni muhimu sana kwa kuwa kampuni hizo zina mchango mkubwa katika maendeleo ya sekta binafsi na nchi kwa ujumla.

“Ni lazima kampuni hizi ziwe na uwakilishi katika mfumo huu mpya wa uongozi,” alisema Bw. Simbeye.

Kwa mujibu wa mfumo huo mpya, wajumbe watapatikana katika kongano kumi. 

Kongano hizo ni pamoja na kilimo, uzalishaji, sekta ya madini, viwanda na nishati, utalii na maliasili, benki na huduma za kifedha, huduma, biashara, sekta binafsi za Zanzibar, vyama vya biashara mikoani na wajasiriamali wanawake.

Hata hivyo makongano haya yanaweza kubadilika kadiri uchumi wa nchi unavyobadilika.
Kwa mujibu wa mapendekezo, wawakilishi wa makongano haya kumi ndio wataunda bodi ya TPSF, nafasi moja ikiwekwa kwa Mwenyekiti anaemaliza muda wake.

Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, makundi maalum kama wanawake, vijana na walemavu watapewa upendeleo maalum katika muundo mpya wa TPSF.

Mwisho 

No comments: