Friday, May 10, 2013

Mfumo wa kongano bunifu suluhisho la maendeleo Tanzania, Afrika



Meneja wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (BDG) Bw. Sosthenes Sambua (katikati) akiongea na Mhandisi Peter Chisawillo (kulia) na mkuu wa wilaya ya Nkasi, Bw. Iddi Kimanta (kushoto) wakati wa mafunzo ya kuwezesha kongano mbalimbali hapa nchini kujenga ubunifu na ushindani mjini Morogoro jana.  Mafunzo hayo yanaendeshwa na Scandnavian Institute for Competitiveness and Development (SICD), Pan African Competitiveness Forum (PACF) na BDG, programu iliyo chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).


Na Mwandishi wetu, Morogoro
Mfumo wa kongano bunifu umetajwa kama mkombozi utakaoleta maendeleo endelevu Tanzania kama utazingatiwa na wadau mbalimbali hapa nchini.
Kauli hiyo imetolewa na Meneja wa Programu ya Fanikiwa Kibiashara (BDG) ambayo inafanya kazi chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Sosthenes Sambua wakati wa mafunzo ya kuwezesha kongano mbalimbali hapa nchini kujenga ubunifu na ushindani mjini Morogoro jana.
Mafunzo hayo ya siku nne yanayoendelea mjini Morogoro yanaendeshwa na Scandnavian Institute for Competitiveness and Development (SICD) pamoja na Pan African Competitiveness Forum (PACF) kwa kushirikiana na BDG, program inayoendeshwa chini ya Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).
Kongano ni mkusanyiko wa makampuni au vikundi vya kiuchumi kuwa pamoja katika eneo moja la kijiografia, vikishirikiana au kushabihiana katika kitu maalum na zikiwa na mahusiano ya karibu na ushirikiano ambao unasaidia kujenga ushindani wao kwa pamoja.
Bw. Sambua ambaye alikua mmoja wa wakufunzi katika mafunzo hayo amewaambia waandishi wa habari kuwa mfumo wa kongano una nafasi kubwa ya kuleta hali bora ya maisha kwa watanzania kwa kuwa unashirikisha nguzo tatu muhimu katika uundwaji wake ambazo ni serikali, wanataaluma au watafiti na wazalishaji katika jamii husika.
Alisema ni katika ushirikiano huo ambapo kongano huja na ubunifu na njia mpya za uzalishaji na kujenga ushindani sit u wa ndani bali pia nje ya nchi na hivyo kuleta maendeleo.
“Nchi nyingi zimefanikiwa kupitia mfumo huu…ni muhimu na sisi tukaupa uzito unaotakiwa,” alisema.
Akitoa mfano wa mataifa mengine alisema nchi kama Sweden, Ujerumani, Italia, Hispania, na Uholanzi zimekua zikitumia mfumo huu wa kongano kwa zaidi ya miaka 20 na kuwa bado wanaendelea kuwekeza katika mfumo huo maana wameona kuwa una manufaa makubwa kiuchumi na kijamii.
Alisema jumuia ya ulaya imetenga pesa kiasi cha Euro 200 bilioni kwa ajili ya nchi wanachama kuomba ruzuku kwa ajili ya kuendeleza kongano bunifu katika nchi zao.
Alitaja nchi nyingine zilizofanikiwa katika mfumo huu wa kongano kama Pakistan, Bolivia, Marekani, India, Canada na Brazil.
Alisema kuwa rasilimali, mawazo na mbinu tofauti havitoshi kuifanya nchi kufikia malengo ya maendeleo bali kinachotakiwa zaidi ya hapo ni ushirikiano wa karibu wa serikali, wataalamu au watafiti pamoja na wazalishaji.
Alitoa wito kwa serikali kuzingatia mifumo bora inayoweza kuleta tija zaidi kama ya kongano ili raslimali zilizopo Tanzania ziweze kuwa na faida zaidi.
“Wanataaluma pia hapa nchini wanatakiwa kufanya tafiti zitakazoimarisha mfumo huu wa kongano maana umeonyesha kuzaa matunda,” alisema.
Alitoa wito kwa wazalishaji kujitahidi kuwa wabunifu na kualika taasisi za utafiti katika kongano zao ili kazi zao ziweze kuboreshwa na kupatiwa ushauri zaidi wa kitaalamu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi ya washiriki katika mafunzo hayo walitoa shukrani kwa waandaaji wa mafunzo hayo na kuahidi kufanyia kazi ujuzi watakaopata kuimarisha kongano zao.
Bw. Godfrey Nyembele anaetoka katika kongano linalijishughulisha na usindikaji wa mafuta ya alizeti wilayani Ileje mkoani Mbeya alisema ataenda kuhamasisha wenzake kuhusiana na njia bora za kuondokana na umaskini baada ya mafunzo hayo.
Bw. Ramadhani Sigareti anaetoka katika kongano linalojishughulisha na kilimo cha mboga na matunda mkoani Dodoma alisema anategemea kuwajengea uwezo wenzake mara tu baada ya mafunzo hayo.
Mafunzo hayo yanayoendelea hadi ijumaa hii yanashirikisha zaidi ya washiriki 60 toka maeneo mbalimbali nchini.
PACF inayojitahidi kupigana na umaskini na kufikia maendeleo ya kijamii na kiuchumi kupitia mfumo huu wa kongano inafanya kazi katika kanda zote za bara la Afrika na kwa sasa sekretarieti yake inaendeshwa nchini Tanzania katika Tume ya Sayansi na Teknolojia Tanzania (COSTECH).
Mwisho 

No comments: