Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye akisisitiza jambo wakati wa
semina ya mafunzo ya maswala ya ubunifu na ushindani wa biashara yanayoendeshwa
na program ya Fanikiwa Kibiashara chini ya TPSF mjini Morogoro jana. Wengine katika picha ni mmoja wa wawezeshaji,
Mhandisi Peter Chisawillo (kushoto) na Meneja wa Programu ya BDG, Bw. Sosthenes
Sambua (kulia)
Na Mwandishi wetu, Morogoro
Moyo na tabia ya ubunifu na ushindani vimetajwa
kuwa vitu muhimu si tu kwa wafanyabiashara bali kwa mafanikio ya watu wote na
maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Wito huu umetolewa na Mkurugenzi Mtendaji wa
Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye alipokua
akizungumza katika semina ya mafunzo ya maswala ya ubunifu na ushindani wa
biashara yanayoendeshwa na program ya Fanikiwa Kibiashara chini ya TPSF mjini
Morogoro jana.
Bw. Simbeye alisema kwamba kama taifa linataka
kupata maendeleo endelevu mambo hayo mawili yanatakiwa kutochukuliwa kama
maswala ya wafanyabiashara pekee kwa kuwa kila mtu anatakiwa kuwa mbunifu na
mshindani bila kuangalia anafanya kazi ya aina gani.
“Hata watendaji serikalini wanatakiwa kuwa wabunifu
na washindani,” alisema na kuongeza kuwa hata dira ya taifa ya maendeleo
inasisitiza maswala hayo ili kufikia mafanikio.
Alisema ni ubunifu na ushindani vitakavyoifanya
Tanzania kutoka hapa ilipo na kuendelea zaidi na kusisitiza kwamba mataifa
yenye nguvu za uchumi zinazingatia sana vitu hivyo viwili.
Alisema nia ya mafunzo hayo ni kuimarisha sekta
binafsi Tanzania na kwamba TPSF inaamini kwamba sekta hiyo kwa kushirikiana na
ile ya umma inaweza kuwa injini kubwa ya maendeleo ya uchumi hapa nchini.
Alifafanua kwamba program ya BDG ni moja ya
iliyofanikiwa sana TPSF ikiwa imeshatoa mafunzo kwa wajasiriamali zaidi ya
8,000 nchi nzima katika miaka minne iliyopita.
Alisema ili kuhakikisha juhudi za BDG hazifi,
tayari TPSF kwa kushirikiana na Baraza la Uwezeshaji Wananchi Kiuchumi na Tume
ya Sayansi na Teknolojia wanabadili mradi huo kuwa taasisi ya kudumu
itakayoitwa Tanzania Entrepreneurship and Competitive Centre (TECC).
“Taasisi hii imeshasajiliwa,” alisema.
Alishukuru serikali kupitia Ofisi ya Waziri Mkuu
pamoja na serikali za Uingereza, Denmark na Sweden kwa utayari wao kusaidia
kukua kwa sekta binafsi Tanzania.
“Tutahakikisha sekta binafsi Tanzania inakua yenye
nguvu na shindani hata nje ya nchi,” alisema.
Kwa upande wake, mmoja wa wawezeshaji, Mhandisi
Peter Chisawillo alisema kuna umuhimu wa kuwa na maono ya aina moja ili kufikia
malengo ya maendeleo.
Alisema ni lazima watanzania kuwa washindani na
wabunifu katika maisha yao ya kila siku ili kufanikiwa.
“Haya ni mambo yatakayofanya nchi yetu kupata
maendeleo na kufanya nchi yetu kuwa na nguvu,” alisema na kuongeza kwamba
takwimu mbalimbali zinaonyesha kuwa bado Tanzania iko nyuma katika maswala hayo
ya ubunifu na ushindani, kitu alichosema kinatakiwa kufanyiwa kazi kwa haraka.
Mafunzo hayo ya wiki nzima yanahudhuriwa na
wajasiriamali zaidi ya 40 na pia wawakilishi mbalimbali toka serikalini.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment