The Tanzania Private Sector
Foundation (TPSF) Executive Director, Mr. Godfrey Simbeye (left) speaking
during a meeting yesterday in Dar es Salaam where a Private Sector Led Working
Group on Construction Permits was established.
On the right is a Policy Analyst from TPSF, Mr. Adam Gahhu.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Godfrey Simbeye (kushoto) akiongea wakati wa
mkutano jana jijini Dar es laam ambapo kikosi kazi kinachoongozwa na sekta
binafsi kushughulikia maswala ya vibali vya ujenzi kiliundwa. Kulia ni mchambuzi wa sera toka TPSF, Bw.
Adam Gahhu.
Na
Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Suluhisho
la matatizo ya kupata vibali vya ujenzi kwa wakati unaotakiwa limepata nguvu
zaidi baada ya kuundwa kwa kikosi kazi kwa upande wa sekta binafsi kushughulikia
swala hilo.
Kikosi kazi
hicho kilichoundwa na Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) kinataka
kusaidia wawekezaji wa ndani, nje na wananchi wengine kwa ujumla kuweza kupata
vibali vya ujenzi kwa wakati unaotakiwa na wenye tija pale wanapotaka kutekeleza
miradi mbalimbali ya ujenzi hapa nchini.
Mkurugenzi
Mtendaji wa TPSF, Bw. Godfrey Simbeye amesema wakati wa uzinduzi wa kikosi kazi
hicho jana jijini Dar es Salaam kwamba hatua hiyo ni kuunga mkono mkakati
maalum wa serikali za kuboresha mazingira ya uwekezaji hapa nchini.
“Vibali vya
ujenzi ni moja ya vigezo vinavyozingatiwa kimataifa katika kutathmini mazingira
ya uwekezaji,” alisema, na kuongeza kuwa sekta binafsi ina nafasi kubwa na
muhimu katika kuboresha upatikanaji wa vibali hivyo.
Bw. Simbeye
alisema kwamba kikosi kazi hicho kitafanya kazi hiyo na kuainisha matatizo na
kutoa mapendekezo ya kitaalamu ambayo baadae yatawasilishwa serikalini kwa
utekelezaji.
“Katika
kutekeleza hili, timu hii itafanya kazi pamoja na wadau mbalimbali toka sekta
ya umma na binafsi,” alisema.
Upatikanaji
wa vibali vya ujenzi ni moja ya mambo yanayoelezwa kuathiri mazingira ya
uwekezaji hapa nchini kutokana na mchakato mgumu wa kuvipata.
Kwa mujibu
wa ripoti ya Benki ya Dunia, Doing Business 2013, taratibu, muda na gharama
zinazotakiwa kupata vibali vya ujenzi bado ni ngumu kwa hapa Tanzania na hivyo
kuathiri mazingira ya uwekezaji.
Kwa mujibu
wa ripoti hiyo, mtu akitafuta vibali vinavyotakiwa ili aweze kutekeleza mradi
wa ujenzi anatakiwa kupitia taratibu zipatazo 19, na siku 206.
Duniani,
Tanzania ni ya 174 kati ya nchi 185 zilizofanyiwa utafiti duniani kuangalia
urahisi wa kupata vibali vya ujenzi.
Kwa upande
wake, Mwenyekiti wa kikosi kazi hicho, Bw. Clement Mworia alisema timu yake
itafanya kazi na serikali kuhakikisha kuwa taratibu nzima za upatikanaji wa
vibali vya ujenzi zinakua rahisi na zenye ufanisi.
“Tutafanya
kazi na serikali na wadau wengine kuhakikisha kuwa mapendekezo yetu yanakua
yenye nguvu na yanatoa suluhisho kwa changamoto hii,” alisema.
Nae msahuri
wa kikosi kazi hicho toka Taasisi ya Uongozi na Maendeleo ya Ujasiriamali, Dkt.
Donath Olomi alisema ucheleweshwaji kupatikana kwa vibali vya ujenzi kunaathiri
swala zima la ajira na mapato ya serikali kwa kiwango kikubwa.
“Ni lazima
changamoto hizi zifanyiwe kazi kwa haraka,” alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment