Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mtumishi wa muda mrefu serikalini na
mtaalamu anayetambulika kitaifa na kimataifa wa maswala ya uwekezaji, Emmanuel
Ole Naiko ameteuliwa kuwa balozi wa heshima wa Botswana nchini Tanzania
atakaekua na makao yake jijini Dar es Salaam.
Akitangazwa na waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Kimataifa, Bw. Bernard Membe jana jijini Dar es Salaam, Bw.
Naiko aliishukuru serikali ya Botswana chini ya uongozi wa Rais Ian Khama na
Waziri wa mambo ya nje na mahusiano ya kimataifa Bw. Phandu T.C Skelemani kwa
kumteua kuwa mwakilishi wao hapa Tanzania.
“Naamini ni Mwenyezi Mungu
aliyewaongoza na mimi napenda kuwahakikishia kwamba sinta waangusha.
Nitawawakilisha kwa ukamilifu wote ulio ndani ya uwezo wangu,” alisema Bw.
Naiko.
Bw. Naiko alimshukuru waziri Membe kwa
kukubali kumkabidhi dhamana hiyo kubwa.
“Wewe ni ndugu na rafiki yangu wa muda
mrefu naamini uliona ni vyema ukanipa heshima hii wewe mwenyewe,” alisema.
Alisema Botswana ina vivutio vingi vya
uwekezaji kama Tanzania na kuwa Watanzania na jumuiya ya Afrika Mashariki
wanakaribishwa kuwekeza katika nchi hiyo.
“Nadhani wakati umefika Botswana nayo
kupata wawekezaji kutoka Tanzania kama wao walivyowekeza Mlimani City,”
alisema.
Nchi ya Botswana imepakana na nchi za
Afrika ya Kusini, Zimbabwe, Namibia na Zambia. Ina ukubwa wa Sq km 58,2000,
wakazi Milioni 2.
Ni nchi iliyo na amani na utulivu toka
uhuru na ina kiwango kidogo sana cha rushwa barani Afrika.
Nchi hiyo imedhamiria kuongoza katika
sekta za fedha, madini hasa Uranium, shaba na usafirishaji wa almasi, na Copper
na pia kuendeleza uwekezaji katika sekta ya utalii kwani Botswana ina mbuga
nyingi za wanyama na hasa Vistoria Falls ambayo iko mpakani na Zimbabwe na
Zambia katika mji wa Kasane.
Bw. Naiko alisema ni vyema Tanzania
nayo ikaanzisha ubalozi wa heshiama Botswana kwani kuna watanzania kati ya 2000
– 4000 ambao wanafanya kazi katika sekta za teknolojia, vyuo vikuu, afya ma
makampuni binafsi.
“Watanzania walioko huko wameanzisha
chama chao na mimi nilikutana nao niliopokuwa TIC,” alisema.
Kodi ya mapato katika nchi hiyo ni
asilimia 22; VAT ni asilimia 12 na pia kuna msamaha wa kodi kwa wawekezaji ni
kati ya miaka mitano mpaka 10.
Mwisho
No comments:
Post a Comment