Tuesday, May 21, 2013

Kusini Pemba wapewa somo kuhusu majadiliano kwa manufaa ya wote


Na Mwandishi Wetu ,Pemba

Mkuu wa Mkoa wa Kusini Pemba Bw. Juma Kasim Tindwa amewataka wananchi wa kisiwani humo kuwa wabunifu katika shughuli zao za kila siku ili kuweza kubadilisha hali ya maisha ya sasa waliyonayo na kuweza kuingia katika ushindani wa kimaendeleo.
Alitoa kauli hiyo Kiswani pemba jana wakati akifungua majadiliano ya ushirikiano kwa manufaa ya wote (smart partnership dialogue) ikiwa ni mwendelezo wa majadiliano yanayofanyika katika kanda mbalimbali hapa nchini.
“Watu wa kisiwani pemba lazima tubadilike kwa sasa, tuondoe ule uzamani tulionao, majadiliano haya yanamaana kubwa sana kwetu, ni lazima tuzingatie yale yatakayozungumzwa na watoa mada ili tukitoka hapa tuwe na mtazamo tofauti katika katika vichwa vyetu” alisema Bw. Juma Kasim.
Alisisitiza kuwa kutokana na kauli mbiu ya majadiliano haya kuwa ni matumizi ya teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu, nilazima watu wabadilike kwa kila nukta ya kazi zao wanazofanya, waweke ubunifu zaidi ya kukaa na kushikilia yale ya zamani.
“Ndugu zangu kauli mbiu hii sio ya kitoto hata kidogo (matumizi ya teknolojia katika kuleta maendeleo endelevu ya kijamii na kiuchumi barani afrika kwa nja shirikishi) lazima tushirikiane kwa manufaa ya wote ili kufikia malengo yetu na kuinua uchumi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla”, alisisitiza Mkuu wa Mkoa kusini Pemba.
Aliongea kuwa maendeleo hayaji kwa kukwamishana bali kwa kusaidiana na kushirikiana, hivyo dhana ya ushirikiano kwa manufaa ya wote ni dhana shirikishi kwa kila mmoja wetu aliyepo hapa.
“Jirani yako akifanikiwa basi sisi sote tumefanikiwa, huu ni mtaji mkubwa sana katika kuleta maendeleo katika dunia ya leo haiwezekani wewe ufanikiwe na jirani yako anaishi katika dimbwi la umasikini, katika zama hizi tuyazike mawazo hayo tushirikiane”,alisisitiza.
Alisema Baraza la Biashara la Zanzibar (zbc) liko bega kwa bega na Baraza la Taifa la Biashara katika kuhakikisha majadiliano haya yanaleta tija na nguvu ya pamoja katika kuleta maendeleo ya wananchi wa Tanzania Bara na Tanania Visiwani.
“Baraza la Biashara la Zanzibar limekuwa mstari wa mbele kuteeleza yale yote yanayolenga katika kuleta maendeleo ya nchi kwa pande zote mbili na ndio mana tumekuwa na mawasiliano ya karibu katika kila hatua na kuhakikisha serikali inasonga mbele katika mipango yake”, aliongeza Juma Kasim Tindwa.
Lazima tuheshimu kauli ya kiongozi wetu Rais Jakaya Mrisho Kikwete, yeye ndio alizindua majadiliaano haya tarehe 28 mei mwaka 2013 na ndio chanzo cha majadiliano haya ya nchi nzima kufanyika sasa na yatakuwa ni mwendelezo katika kila mwaka.
“Ndugu zangu majadiliano haya yatakuwa endelevu na kila mwaka tutakuwa tunaulizana wapi tumefikia katika yale tulioyajadili katika mikutano yetu iliyotangulia, ni lazima kila mtu atimize wajibu wake ipasavyo kwa yale aliyopangiwa” alisema.
Aidha aliwataka wakazi wa mkoa wa kusini Pemba na maeneo yote kisiwani humo kuwa na mtazamo hasi katika kuleta mabadiliko ya kiuchumi na kijamii, nah ii ni kuacha tofauti zao za kimawazo na kimtazamo katika yale wanayoyatekeleza kila siku wawapo katioka majukumu yao ya kawaida.
Kwa upande wake Mkuu wa Fedha na Utawala wa Baraza la Taifa la Biashara (TNBC), Bi. Oliva Vegulla alisifu ushiriki na michango mbalilimbali kutoka kwa washiriki wote katika mkutano huo.
“Ushiriki umekuwa mzuri na ni matarajio yetu kuwa mambo mengi yalijadiliwa hapa yataingizwa kwenye mkutano wa kitaifa utakaofanyika mapema mwezi ujao,” Bi. Vegulla alisema.
TNBC ndiyo waliopewa dhamana ya kuratibu majadiliano hayo ya kikanda  nay a kitaifa pia.
Majadiliano ya ushirikiano kwa manufaa ya wote (smart partnership dialogue) hutoa fursa kwa viongozi wa serikali katika ngazi husika na kukutana na jumuiya mbalimbali za wananchi kujadili ili kupata mawazo kutoka ngazi ya chini kwenda juu na wala sio viongozi kutoa maagizo kutoka juu kwenda chini.

 mwisho

No comments: