Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Ndug; Jakaya Mrisho Kikwete
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Rais Jakaya Kikwete ametoa wito kwa
taasisi za fedha nchini kutenga fedha kwa ajili ya kutoa mikopo kwa wakulima
ili kilimo Tanzania na katika nchi za Afrika kiweze kuwa cha kisasa na kutoa
mazao ya kutosha ya chakula na biashara.
Rais Kikwete alisema hayo jana jijini
Dar es Salaam wakati akihutubia kongamano kubwa la kikanda la kilimo la
muungano wa umoja wa vyama vya kilimo kusini mwa Afrika (SACAU) jana jijini Dar
es Salaam.
“Taasisi za fedha hazina budi kuchukua
jukumu hilo katika nchi zetu badala ya kutegemea tu serikali zetu,” alisema na
kuongeza kuwa kwa kufanya hivyo kilimo kitapata msukumo mpya na kusaidia
kuondoa umasikini.
Kongamano hilo lililoangalia kwa undani
swala la jinsi ya kuhudumia kifedha kilimo cha Afrika lilitayarishwa na Baraza
la Kilimo na Mifugo Tanzania (ACT) kwa kushirikiana na SACAU.
Alisema Kilimo ni uti wa mgongo kwa
nchi za Afrika ikiwemo Tanzania hivyo kuna kila sababu ya kuhakikisha wakulima
wadogo na wakubwa wanawezeshwa ili kupata zana za kisasa kama matrekta,
pembejeo bora na madawa.
Alisitiza kuwa miundombinu ya
umwagiliaji inatakiwa kujengwa ili kukabili mabadiliko ya tabia nchi badala ya
kutegemea mvua ambazo siyo ya uhakika.
“Serikali ya Tanzania imejiwekea
mkakati wa kukuza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) kwa
ajili ya kukuza kilimo kidogo na kikubwa,” aliongeza.
Ukanda huo wa kilimo unaundwa na mikoa
ikiwemo ya Iringa, Ruvuma, Mbeya na Rukwa ambayo ni wazalishaji wakubwa wa
mazao ya mahindi, mpunga na mazao mengine hapa Tanzania.
Alisema ukanda huo ukifanikiwa dhana
hiyo itaenezwa katika kanda nyingine katika kuendeleza kilimo kama pamba na
kahawa.
Naye Mwenyekiti wa bodi ya ACT, Bw.
Salum Shamte alisema hakuna mbadala wa kilimo kama kweli Tanzania na Afrika
inataka kweli kufikia maendeleo endelevu.
Alisema sekta ya kilimo ikipata mikopo
ya muda mrefu na riba nafuu inaweza kuwa ya kisasa na kusaidia kupata chakula
cha kutosha na kubadilisha maisha ya watu wa Afrika wakiwemo watanzania.
Mkurugenzi Mtendaji wa Miyombo Golden
Resource Company, Bw. Freddy Swai aliyekua mmoja wa washiriki katika mkutano
huo alisema shughuli za ufugaji nyuki ni moja ya kazi muhimu katika biashara
lakini kinahitaji kuwezeshwa.
“Warina asali tunayo fursa nzuri ya
kuendelea lakini tunashindwa kuendelea sababu hatuna uwezo wa kutosha,”
alisema.
Washiriki zaidi ya 200 kutoka nchi 14
za kusini mwa Afrika pamoja na wawakilishi wa vyama vya wakulima kutoka maeneo
mengine ya Afrika walishiriki kongamano hilo lilomalizika jana.
Pamoja na mambo mengine, mkutano huo
uliangalia ushirikiano kati ya SADC/COMESA/EAC katika maswala ya kilimo.
Pia mkutano huo uliangalia makisio ya
mahitaji ya bidhaa za kilimo duniani na kuona fursa na tishio lake kwa
wakulima.
Pia washiriki hao walizungumzia kama
mfumo wa kifedha uliopo sasa unaweza au hauwezi kuendeleza sekta ya kilimo
katika siku zijazo.
Mwisho
No comments:
Post a Comment