Wednesday, April 3, 2013

RUBADA, wadau wajadili ripoti ya Stieglers Gorge




Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) Bw. Aloyce Masanja akiwaonyesha wadau kutoka katika taasisi na Idara mbalimbali za serikali ripoti ya awali iliyotayarishwa na Kampuni ya  Odebretch International ya Brazili ikiwa ni hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maji wa Stierglers Gorge, ripoti hiyo imewasilishwa kwa wadau hao ili kuijadili na  kuangalia kama moja ya hatua za utekelezaji mradi huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam. 



Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) Bw. Aloyce Masanja akiwaonyesha wadau kutoka katika taasisi na Idara mbalimbali za serikali ripoti ya awali iliyotayarishwa na Kampuni ya  Odebretch International ya Brazili ikiwa ni hatua ya awali ya utekelezaji wa mradi mkubwa wa uzalishaji umeme wa maji wa Stierglers Gorge, ripoti hiyo imewasilishwa kwa wadau hao ili kuijadili na  kuangalia kama moja ya hatua za utekelezaji mradi huo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.  Kulia ni Mwenyekiti wa Bodi ya wakurugenzi wa Mamlaka hiyo, Profesa Raphael Mwalyosi.




Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Mamlaka ya Uendelezaji Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imekutana na wadau mbalimbali toka idara na taasisi za serikali kujadili ripoti ya awali ya ujenzi wa mradi wa Stieglers Gorge.

Hatua hiyo muhimu imefikiwa kama moja ya michakato kuelekea utekelezaji wa mradi huo ambao utatekelezwa kwa ushirikiano kati ya RUBADA na Kampuni ya Odebretch International ya Brazil.

“Tumejadili kwa mafanikio makubwa ripoti hii ya awali na mwelekeo ni mzuri,” alisema Mkurugenzi Mkuu wa RUBADA, Bw. Aloyce  Masanja mbele ya waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam mara baada ya mkutano huo.

Ripoti husika ilitayarishwa na kampuni hiyo ya Brazil na kukabidhiwa kwa ungozi wa RUBADA miezi michache iliyopita.

Ripoti hiyo inatoa picha kamili ya mwelekeo wa utekelezaji wa mradi huo mkubwa unaotarajiwa kuzalisha 2100MW za umeme mara utakapokamilika.

Ripoti na mapendekezo hayo imegusa maswala kama maji, teknolojia itakayotumika, vyanzo vya fedha na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi.

Bonde la Mto Rufiji linapita katika mikoa nane na linakaliwa na watu milioni nane hivyo kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na msaada mkubwa katika shughuli za maendeleo.

Bw. Masanja aliwaambia waandishi wa habari kuwa hatua ya kujadili ripoti hiyo ilikua ya muhimu sana kuelekea utekelezaji wake maana utahusisha wadau mbalimbali.
“Kimsingi wajumbe hao wa mkutano walikubaliana kuhusiana na umuhimu wa kutekelezwa kwa mradi huo,” alisema.

Kwa mujibu wa Bw. Masanja, awamu ya pili ya mradi huo itaanza  April, 2013 kwa kuanza kufanya tathmini ya upembuzi yakinifu ya kimazingira ili kuchukua tahadhari kulinda mazingira, viumbe na shuhghuli za kilimo cha umwagiliaji.

Pia awamu hiyo itaangalia namna ya ujenzi wa mbiundombinu mbalimbali itakavyokuwa ikiwemo ya nguzo za umeme, na barabara kutoka katika eneo la mradi hadi Chalinze mkoa wa Pwani.

Alisema awamu hiyo itakamilika Juni 2014 baada ya kukamilisha upembuzi huo yakinifu na kupata vibali mbalimbali vya kuanzisha mradi huo vikiwemo vya matumizi ya maji kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Nishati na Maji (EWURA) na Shirika la Umoja wa Mataifa linaloshughulikia elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO) kwa sababu mradi upo katika hifadhi ya Selous.

Alisema ujenzi unatarajia kugharimu dola za Kimarekani bilioni 2.3 ambapo ghrama halisi za mradi mzima ni dola za kimarekani bilioni 3.6.

“Umeme huu ni muhimu katika uzalishaji viwandani na migodini  sababu ni rahisi ambapo uniti moja itauzwa dola ya kimarekani senti nne ,” na kuongeza kusema tayari masoko yako wazi na ni mengi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi RUBADA, Profesa Raphael Mwalyosi alisema mradi huo ni wa mseto na unatarajia kuzalisha nishati ya umeme na pia utachochea kilimo cha umwagiliaji Rufiji chini, maji ya kunywa na utalii katika hifadhi ya Selous.

“Mafanikio ya mradi huo unahitaji ushirikiano mkubwa wa kutunza vyanzo vya maji kutoka TANESCO, DAWASA, Wizara ya maji, Wizara ya Kilimo na Chakula na RUBADA,”alisema Profesa Mwalyosi.

Alisema umeme wa maji ni muhimu na ni uwekezaji endelevu ukilinganisha na umeme wa vyanzo vingine pamoja na kwamba kuna changamoto ya mabadiliko ya tabia nchi,hivyo kuna kila sababu ya mradi huo kukamilishwa.
Alisema viongozi na wadau mbalimbali wanahitajika kuunga mkono ujenzi wa mardi sababu utasaidia kukua kwa uchumi wa nchi na ustawi wa jamii.

Wadau walioshiriki kujadili ripoti hiyo walitoka Wizara ya Nishati na Madini, Maliasili na Utalii, Wizara ya Maji, Wizara ya Kilimo, Chakula na Ushirika, EWURA, Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, RUBADA na taasisi mbalimbali.

Mwisho 

No comments: