Na Mwandishi Wetu, Arusha
Taasisi ya
Sekta Binafsi nchini imesema itaendelea kuimarisha wanachama wake katika ngazi
za kanda kwa kuwapa elimu ya biashara ili kukabiliana na soko la Afrika
Mashariki linaloendelea kukua kwa kasi kwa sasa.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Taasisi hiyo Bw. Godfrey Simbeye aliyasema hayo jijini Arusha muda
mfupi mara baada ya kukutana na wanachama wa kanda ya kaskazini ambapo pamoja
na mambo mengine wametakiwa kuimarisha vyama vyao vya biashara katika ngazi ya
mikoa na wilaya.
“Napenda
tuelewe kuwa wanachama walioko katika kanda ya kaskazini wako mipakani hivyo ni
jukumu letu kutoa elimu ya kibiashara ya jinsi ya wao kuingia katika ushindani
wa soko la Afrika Mashariki,” alisema Simbeye.
Alisisitiza
kuwa kwa sasa kuna programu maalumu ya kutoa elimu ya kuendeleza
wafanyabiashara ijulikanayo kama (Trade Mark East Afrika) inayoangalia fursa
zilizopo katika mikoa ya kanda ya kaskazini ili wafanya biashara wa ukanda huo
waweze kuchangamkia na kunufaika na fursa zilizopo.
Aliongeza
kuwa TPSF kwa kushirikiana na TCCIA katika ngazi ya kanda wameanzisha program
nyingine ya kuendeleza wajasiriamali wadogo waweze kuzalisha na kuuza zaidi.
“Katika
kuhakikisha kuwa wanachama wa TPSF wanakuwa kitu kimoja na kujenga sauti moja
yenye nguvu, wajasiriamali wadogo wanaangaliwa kwa ukaribu hasa kwa kuanzisha program mbalimbali za kuwainua
kiuchumi katika maeneo yao ya biashara waweze kuingia katika kundi la wafanyabiashara
wa kati,” alisisitiza.
Alisema
programu kama hizo ni njia tu ya kuelekea katika kuimarisha uchumi wa nchi
kupitia wafanya biashara wadogo ambao wakiwezeshwa kielimu na kimtaji wataweza
kuwa wafanyabiashara wakubwa hapo baadae.
Akizungumzia
mabaraza ya wilaya na mikoa, Bw. Simbeye aliyataka kufanya kazi kwa ukaribu
zaidi na taasisi hiyo ikiwa ni katika kujenga umoja na nguvu zaidi katika mikoa
na wilaya.
Alisema kwa sasa mabaraza hayo
yamekuwa kimya kutokana na kutokutana mara kwa mara na kujadili mustakabali wa
masuala mbalimbali ya kibiashara katika mikoa na wilaya zao.
“Kikubwa ninachotaka kuwaambia
viongozi katika mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya wafanye mikutano kama
katiba inavyoelekeza, mabaraza haya hajakaa kwa muda mrefu hivyo ni wakati wao
wa kukutana na kujadili matatizo yaliyopo katika maeneo yao,” alisema
Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia umuhimu wa mabaraza hayo kwa uchumi wa taifa Bw.
Simbeye alisema mabaraza ya wilaya na mikoa ni muhimu sana si kwa uchumi wa
mkoa bali kwa taifa na hii ni kutokana na kuhusisha pande zote mbili za sekta
ya umma na binafs katika kukaa na kujadili maendeleo ya wilaya na mkoa kwa
ujumla.
Mkutano
huo wa kuimarisha sauti moja ya taasisi ya sekta binafsi nchini kwa kanda ya
kaskazini umejumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Wanachama
wa taasisi hiyo walijadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali
za kiuchumi katika mikoa ya kanda hiyo pamoja na changamoto mbalimbali
zinazowakabili.
Mwisho
No comments:
Post a Comment