Monday, December 22, 2014

Watanzania washauriwa kujenga tabia ya kununua hisa

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wito umetolewa kwa Watazania kujenga tabia ya kununua hisa katika kampuni ikiwemo ya kampuni Uwekezaji ya TCCIA kwa maendeleo yao na taifa zima kwa ujumla.

Wito huo ulitolewa na wakala wa uuzaji Hisa wa kampuni ya Rasilimali Limited, Bw. Arphaxad Masambu ambaye pia ni mjumbe wa kampui ya TCCIA alipokua akitoa semina kwa wanahisa wa kampuni hiyo hivi karibuni jijini humo.

Mtaalamu huyo alisema wakati umefika wa watanzania kuelewa maana ya hisa na kuanza kuzinunua.

“Tunatakiwa kubadilika kwa sababu swala hili limekuwa kama geni kwetu, sasa wakati umefika wa kuchukua hatua na kupenda kujifunza ili hisa zitusaidie baadaye,”alisema.

Akifafanua zaidi alisema kuwa na hisa katika kampuni ni ukombozi mkubwa katika maisha sababu fedha zinakuwa katika mazingira salama na zinaongezeka.

Alisema kampuni ya hisa kazi yake ni kukusanya mtaji ambao unatokana na hisa walizonunua watu na kwenda kuwekeza katika makampuni na mashirika yanayojiendesha kwa faida.


“Kampuni ya hisa inaendeshwa kwa mujibu wa sheria za nchi, hivyo watanzania wasisite kununua hisa katika kampuni zinazofanya vizuri,”alisema.

Wateja wa Zantel, Tigo kufaidika na huduma mpya ya kutuma, kupokea fedha

Mkurugenzi wa Huduma za Fedha Zantel, Bw. Hashim Mukudi (wa pili kushoto) akipongezana na Mkuu wa kitengo cha Huduma za Fedha wa kampuni ya Tigo, Bw. Andrew Hodgson  wakati wa uzinduzi rasmi wa huduma mpya ya kutuma na kupokea pesa miongoni mwa wateja wa mitandao hiyo hapa nchini jana visiwani Zanzibar.  Kulia ni Meneja Chapa wa Tigo, Bw. William Mpinga na kushoto ni Bi. Shinuna Kasim ambae ni Mkurugenzi wa Miradi wa Zantel.
Na Mwandishi wetu, Zanzibar

Kampuni za simu za mkononi za ZANTEL na Tigo zamezindua rasmi huduma za kutumiana pesa miongoni mwa wateja wake Tanzania.

Mbali na huduma hiyo ya kutumiana pesa miongoni mwa wateja wa mitandao hiyo, wateja wa EzyPesa na TigoPesa sasa wataweza kutuma na kupokea pesa kwa marafiki na ndugu walio katika mitandao hiyo popote pale nchini.

Kutekelezwa kwa mpango huo kunazifanya ZANTEL na Tigo kuwa viongozi wa huduma kama hiyo Duniani. 

Uzinduzi wa huduma hiyo umefanyika visiwani Zanzibar jana na kushuhudiwa na maafisa wa juu wa kamuni hizo.  Haya ni matokeo ya makubaliano yaliyotangazwa mwanzoni mwa mwaka huu na EzyPesa, TigoPesa na Airtel Money.  

Kwa mujibu wa maafisa hao, hapatakuwa na gharama za ziada mteja anapotuma pesa kwa mtandao mwingine isipokuwa gharama zinakuwa sawa na zile anapotuma kwenye mtandao wake.

Pia, wateja wanaopokea pesa kutoka mtandao mwingine wanaweza kutoa pesa kwa wakala wa mtandao wao na hapatakuwa tena na ulazima wa mteja kutafuta wakala wa mtandao wa mtu aliyemtumia pesa.


Akizungumza wakati wa uzinduzi huo, Mkurugenzi wa Biashara wa Zantel, Mohamed Mussa, alisema Zantel inaendelea kutimiza ahadi ya kuwarahisishia huduma za fedha wateja wake kwa kufanya kazi pamoja na Tigopesa.

Tumedhamiria kuwapa wakazi Dar, elimu bora---Mzumbe

Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstaafu, Barnabas Samatta (wa pili kushoto) wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho kampasi ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine ni Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Josephat Itika (kushoto); Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Daniel Mkude (wa pili kulia) na Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Utawala na Fedha, Profesa Faustin Kamuzora (kulia).
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstaafu, Barnabas Samatta (wa pili kulia) wakati wa mahafali ya 13 ya chuo hicho kampasi ya Dar es Salaam mwishoni mwa wiki.  Wengine ni Kaimu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Profesa Josephat Itika (kulia); Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Daniel Mkude (kushoto) na Naibu Makamu Mkuu wa chuo hicho, Utawala na Fedha, Profesa Faustin Kamuzora (wa pili kushoto nyuma).
 Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam kimeendelea kupata mafanikio ambapo kwa sasa kinaendesha programu 11 za shahada ya uzamili huku mbili kati yake zikiendeshwa kwa ushirikiano na chuo Kikuu cha Bradford cha Uingereza ukilinganisha na programu mbili zilizokwepo wakati kampasi ikianzishwa mwaka 2005.

Kaimu Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe, Profesa Josephati Itika alisema katika mahafali ya 13 yaliyofanyika mwishoni mwa wiki iliyopita Kampasi ya Dar es Salaam kuwa hatua hiyo ni fursa nzuri hasa kwa wakaazi wafanyakazi wa jiji hilo ambao wana kiu ya kujiendeleza kielimu.

Katika mahafali hayo yaliyofanyika katika kampasi hiyo, wahitimu mbalimbali walitunukiwa shahada zao na Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstafu, Barnabas Samatta.

“Chuo kimepata mafanikio makubwa na kinazidi kupanua programu zake ili kukidhi mahitaji ya wakazi wa jiji la Dar es Salaam wanaopenda kuendelea na masomo,”alisema.


Alisema programu hizo zimewezesha watanzania waishio  Dar es Salaam kujiendeleza kielimu huku wakiwa wanafanyakazi.