The registrar of
Contractors Registration Board (CRB), Eng. Boniface Muhegi addressing participants
of the CRB’s annual consultative meeting that started yesterday in Dar es
Salaam.
Msajili wa bodi ya
makandarasi nchini (CRB), Eng. Boniface Muhegi akihutubia mkutano mkuu wa
majadiliano wa bodi hiyo ulioanza jana jijini Dar es Salaam
The registrar of Contractors Registration Board (CRB), Eng. Boniface Muhegi (centre) following up proceedings during the board’s annual consultative meeting that started yesterday in Dar es Salaam. Others in the picture are the CRB board chairperson, Eng. Consolata Ngimbwa (right) and Tunduru Member of Parliament, Eng. Ram Makani.
Msajili wa bodi ya makandarasi nchini (CRB), Eng. Boniface Muhegi (katikati) akifuatilia jambo wakati wa mkutano mkuu wa majadiliano wa bodi hiyo ulioanza jana jijini Dar es Salaam. Wengine katika picha ni Mwenyekiti wa bodi wa CRB, Eng. Consolata Ngimbwa (kulia) na mbunge wa jimbo la Tunduru, Eng. Ram Makani.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Bodi ya Usajili wa Makandarasi nchini
(CRB) imetoa wito kwa makandarasi nchini kuhakikisha kuwa wanaungana ili
kujenga umoja na nguvu na kupata miradi mikubwa.
Wito huu umetolewa na Mwenyekiti wa
bodi ya CRB, Eng. Consolata Ngimbwa alipokua akiongea wakati wa mkutano mkuu wa mwaka wa majadiliano wa bodi hiyo ulioanza jijini Dar
es Salaam jana.
Alisema kuungana kutasaida
makandarasi wa ndani kuwa na nguvu na pia kuweza kushindana na wale wa nje
ambao wengi wao wana nguvu za mitaji, na utaalamu.
“Tuungane ili na sisi tuweze kupata
sifa za kupata miradi mikubwa,” alisema.
Akifafanua zaidi alisema kuwa
makandarasi wa madaraja ya juu washirikishe wale wa madaraja ya chini ili
waweze kufanya kazi pamoja kwa faida yao wote na kwa faida ya taifa kwa ujumla.
“Makandarasi wa madaraja ya juu
waruhusu ushirika na wale wa madaraja ya chini ili kuleta mafanikio zaidi,”
alisema.
Akiongea awali, msajili wa Bodi hiyo
injinia Boniface Muhegi alisema bodi hiyo imefanikisha mambo mengi tangu
kuanzishwa kwake miaka 15 iliyopita.
Alisema kuwa sekta ya ujenzi Tanzania
imepiga hatua kubwa kwani kulikuwa na makandarasi wapatao 1000 miaka 15
iliyopita kulinganisha na sasa ambapo kuna jumla ya makandarasi 7000.
Ametaja mafanikio mengine kuwa ni kuwa
na ofisi za kanda katika mikoa minne ya Mbeya, Arusha, Mwanza na Dar es Salaam
pamoja na kuongezeka kwa kazi zinazofanywa na makandarasi wazalendo toka
asilimia tano mwaka 1998 hadi asilimia 40 leo huku asilimia 60 ya kazi bado
zikifanywa na wageni.
“Pia pamekua na ongezeko la ubora na
uwingi wa kazi za ukandarasi wa ujenzi,” alisema huku akitolea mfano ongezeko
la minara ya mawasiliano ya simu za mkononi ambayo imetapakaa karibu nchi
nzima, barabara na majengo ya kisasa.
“Pamoja na vikwazo mbalimbali,
tumepiga hatua kubwa,” alisema.
Kwa upande wake, msajili msaidizi,
Utafiti na Maendeleo wa bodi hiyo, Eng. Magesa Bairi alisema bodi itaendelea
kuwezesha makandarasi nchini kwa njia ya mafunzo na pia kutunisha mfuko wa
kusaidia makandarasi hapa nchini.
Eng. Magesa alisema kuwa pamoja na
maendeleo hayo kuna changamoto ambazo zinawakabili kama kujenga uwezo wa
wakandarasi wazalendo kwa viwango vinavyotakiwa, na pia kutofuata kanuni na
sheria mbalimbali kwa upande wa makandarasi.
Mkutano huo wa siku mbili unalenga kuangalia
hasa changamoto na mafanikio katika sekta ya ujenzi Tanzania ndani ya miaka
kumi na tano iliyopita.
Mapendekezo ya mkutano huo
yatapelekwa kwa wadau husika na baadae kufuatilia utekelezaji wake.
Takwimu zinaonyesha kwamba sekta ya
ujenzi inachangia asilimia saba ya pato la taifa huku ukuaji wake kwa mwaka
ikikadiliwa kuwa ni asilimia kumi na moja ikiwa ni sekta ya pili kwa kasi ya
ukuaji huku sekta ya madini ikiongoza.
Asilimia sitini ya bajeti ya
maendeleo nchini inakwenda kwenye sekta ya ujenzi huku asilimia themanini ya
fedha hizo zikienda kwa wanachama wa bodi ya usajili wa mandarasi wa ujenzi.
Inatarajiwa kuwa kesho Waziri wa
Ujenzi, Dkt. John Pombe Magufuli atazungumza na kushiriki mkutano huo.
Mwisho.