Na Mwandishi wetu, Mbeya
Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kimesema wajasiriamali nchini
wanatakiwa kuongeza nguvu zaidi katika kuendelea biashara kwa kuwa biashara zao
ni nguzo ya uchumi wa nchi.
Mratibu wa Mafunzo ya Ujasiriamali wa kituo hicho, Bw.Patrick
Chove ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo ya ujasiriamali alisema hayo mkoani
Mbeya kuwa wajasiriamali wana nafasi kubwa ya kuendeleza nchi.
Alisema hayo wakati wa mafunzo ya wajasiriamali katika mkoa huo yaliyotolewa
na TIC kwa kushirikiana na Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na Maendeleo
(UNCTAD) chini ya programu ya Business Linkages ya kituo hicho.
“Taifa linatambua mchango wa wajasiriamali ndiyo maana kumekuwa na
jitihada nyingi za uwekaji mazingira bora ya biashara,”na kuongeza kusema kuwa
ombi kubwa kwao ni kufuata maadili ya kufanya biashara.
Alisema kwa kutambua umuhimu wa wajasiriamali,TIC inazidi
kuendeleza kutoa mafunzo kwa kundi hilo kwa kuwajengea uwezo wa kufanya
biashara na wafanyabiashara wa makampuni makubwa.
“Tulianza kutoa mafunzo haya Jijini Dar es Salaam yakaenda Moshi
na sasa yameingia Kanda ya Nyanda za Juu Kusini na Mkoa wa Mbeya umekuwa wa
kwanza,”alisema Bw.Chove.
Kanda ya Nyanda za Juu Kusini inajumuisha mikoa ya Ruvuma, Iringa,
Rukwa, Katavi na Mbeya yenyewe ambapo ofisi ya kanda ya TIC ndiyo inayoratibu
mafunzo hayo katika eneo hilo.
Alieleza kuwa matarajio ya mafunzo hayo ni kuwafikia wajasiriamali
wote katika kanda hiyo ili waweze kupata mbinu za biashara na kutoa mchango wao
kwa taifa.
Alisema katika mafunzo hayo,
wajasiriamali wanafundishwa tabia za kuwa mfanyabiashara ili waweze
kuwa kama wafanyabiashara wengine duniani maana tabia zao zinafanana.
Mshauri kutoka Shirika la Umoja wa Mataifa la Biashara na
Maendeleo (UNCTAD), Benedict Lema ambaye pia ni mwezeshaji wa mafunzo ya
ujasiriamali alisema kampuni kubwa zinashindwa kufanya biashara na
wajasiriamali hapa nchini kwa kuwa baadhi siyo waaminifu.
“Badala ya kununua malighafi za wajasilimali wa hapa,
wafanyabiashara wakubwa wanaagiza nje ya nchi,” alisema Bw. Lema, na kuongeza
kuwa hali hii haifai kwa maendeleo yao.
Alisema ni muhimu kwa wafanyabiashara wa ndani kujitahidi kuwa
waaminifu na kujituma ili kufikia viwango vya kimataifa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment