Wednesday, January 30, 2013

Sheria itakayoongoza maendeleo sekta binafsi yatakiwa


 The Chairperson of the Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Ms. Esther Mkwizu talks to Mr. Aloys Mwamanga (centre) and the TPSF Board Member, Mr. Salum Shamte (right) during the TPSF extra ordinary general meeting held in Dar es Salaam yesterday.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Esther Mkwizu akiongea na Bw. Aloys Mwamanga (kati) na mjumbe wa bodi ya TPSF, Bw. Salum Shamte (kulia) wakati wa mkutano mkuu maalumu wa Taasisi hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam. 



The Chairperson of the Tanzania Private Sector Foundation (TPSF), Ms. Esther Mkwizu (left) with the Foundation’s Executive Director, Mr. Godfrey Simbeye (centre) and a TPSF Board Member, Mr. Salum Shamte (right) during the TPSF extra ordinary general meeting held in Dar es Salaam yesterday.
Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Esther Mkwizu (kushoto) akiwa pamoja na Mkurugenzi Mtendaji wa taasisi hiyo, Bw. Godfrey Simbeye (kati) pamoja na mjumbe wa bodi ya TPSF, Bw. Salum Shamte (kulia) wakati wa mkutano mkuu maalumu wa Taasisi hiyo uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Hatua ya kuundwa kwa sheria itakayoongoza ustawi, umoja na ushirikiano wa sekta binafsi Tanzania imetajwa kama muhimu na ya haraka kwa maendeleo ya uchumi hapa nchini.
Pendekezo hili liko kati ya mapendekezo saba yaliyotolewa katika mkutano mkuu maalumu wa wanachama wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) uliofanyika jana jijini Dar es Salaam.
Akiwasilisha mapendekezo hayo mbele ya wajumbe wa mkutano huo, Mwenyekiti wa kikundi kazi wa kamati ndogo ya wajumbe wa kamati iliyochaguliwa kuangalia jinsi ya kuimarisha sekta binafsi hapa nchini, Bw. Salum Shamte alisema jambo hilo ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta hiyo hapa nchini.
“Tunapendekeza kuwepo na sheria ya kuendeleza sekta binafsi hapa nchini,” alisema, na kuongeza kuwa jambo hili lifanywe haraka ili kufikia malengo ya taasisi hiyo.
Mapendekezo mengine yaliyotolewa na kamati hiyo ndogo ni pamoja na kupitiwa upya kwa malengo matatu ya awali ya taasisi hiyo kuyafanya kuwa nane yakijumuisha maswala ya majukumu ya kijamii (CSR), usalama na maendeleo ya mazingira pamoja na kuhusishwa kwa wadau toka ushirika wa sekta binafsi na ya umma (PPP).
Pia mapendekezo mengine ni kugawanya wanachama wa taasisi hiyo katika makongano kumi (clusters) ili kuimarisha ushiriki wao katika taasisi hiyo.  Makundi ya kongani hizo ni pamoja na kilimo, uzalishaji, sekta ya madini, viwanda na nishati, utalii na maliasili, benki na huduma za kifedha, huduma, biashara, sekta binafsi za Zanzibar, vyama vya biashara mikoani na wajasiriamali wanawake.
“Hata hivyo makongano haya yanaweza kubadilika kadiri tunavyoendea na uchumi wa nchi unavyobadilika,” alisema Bw. Shamte, na kuongeza kuwa hilo likitokea basi namba ya makongano hayo inaweza kuongezeka na mfumo wake kubadilika.
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, wawakilishi wa makongano haya kumi ndio wataunda bodi ya TPSF, nafasi moja ikiwekwa kwa Mwenyekiti anaemaliza muda wake.  Mwenyekiti na Makamu Mweneyekiti wa taasisi hiyo watatokana na wajumbe hao kumi. 
Kwa mujibu wa mapendekezo hayo, makundi maalum kama wanawake, vijana na walemavu watapewa upendeleo maalum katika muundo mpya wa TPSF.
“Kuna umuhimu wa kuangalia jinsi TPSF itakavyojenga uwigo wa kupata mapato zaidi ili kuimarisha sekta hii muhimu hapa nchini,” alisema Bw. Shamte akiongeza pendekezo lingine ya kamati yake.
Wajumbe wengine wa kikosi kazi cha kamati hiyo ndogo iliyoshughulikia mapendekezo haya walikuwa ni Bw. Felix Mosha, Bw. Ali Mufuruki, Bw. Aloys Mwamanga na Dkt. Gideon Kaunda.
Kwa ujumla, wajumbe wa mkutano huo waliotoka nchi nzima walipitisha mapendekezo ya kikosi kazi cha kamati hiyo ndogo. 
Ilikubalika kwamba marekebisho madogo yaliyochangiwa na wajumbe wa mkutano huo yatazingatiwa.
katika miaka ya hivi karibuni, mchango wa sekta binafsi katika kuendesha uchumi wa nchi umekuwa ukitambulika na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na serikali.
Mwisho 

No comments: