Wajasiriamali wa Mkoa wa Mbeya wameshauriwa kuwa wabunifu
katika biashara zao ili kuwaongezea vipato vya kutosha na kutoa ajira kwa
watanzania.
Akifungua Mafunzo ya wiki moja ya wajasiriamali hao, Mkuu wa
Mkoa wa Mbeya, Bw. Abbas Kandoro aliwataka kujenga tabia hiyo katika biashara zao.
“Ubunifu katika biashara ni jambo la msingi sana, ni lazima
lizingatiwe,” alisema na kuongeza kuwa katika kufanikisha hilo wanatakiwa
kuondoa uoga wa kuthubutu kufanya ubunifu.
Alisema wajasiriamali hao wanatakiwa kuyatumia vizuri mafunzo
hayo wanayopatiwa na Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kwa kushirikiana na
Shirika la Kimataifa la Biashara na Maendeleo (UNCTAD) ili kupata mbinu mpya za
biashara.
Bw. Kandoro alisema wajasiriamali hao wanahitajika pia
kuvitumia vyombo vya fedha kupata mikopo na kujenga tabia ya kuirudisha kwa
wakati ili waweze kukopa tena kwa ajili ya kukuza biashara zao.
Alisisitiza kuwa mfunzo hayo yanalenga kuwaunganisha na makampuni
makubwa kwa ajili ya kupata ujuzi, hivyo wana wajibu wa kuhakikisha wanaheshimu
mikataba watakayoingia na kujiepusha na tabia ya ubabaishaji katika mahusiano
hayo.
Alisema serikali itaendelea kuwajengea misingi mizuri ya
kufanya biashara zao ili wote waweze kukua zaidi na kusaidia kutoa ajira na
kukuza uchumi wa nchi.
Meneja wa Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC),Kanda ya Nyanda za
Juu Kusini, Bw. Daudi Riganda alisema mafunzo hayo yamejumuisha wajasiriamali
30 kutoka Mkoa wa Mbeya.
“Mafunzo haya yanatolewa
kwa mara ya kwanza katika kanda hii na yameanza kwa wajasiliamali wa Mkoa wa
Mbeya,” alisema na kuongeza kuwa matarajio ni kuwafikia wajasilimali wote
katika kanda yao yenye mikoa ya Ruvuma, Iringa Katavi, Rukwa na Mbeya.
TIC kwa kushirikiana na UNCTAD wanaendesha mafunzo hayo
kuwajengea uwezo wajasiriamali hao kwa kuwaunganisha na makampuni makubwa
kufanya biashara kwa ufanisi.
Mshauri wa programu hiyo kutoka UNCTAD, Bw.Benedict Lema ambaye
pia ni mwezeshaji wa program hiyo, alisema mafunzo hayo yanalenga kuwawezesha
wajasilimali kufanya biashara na kampuni kubwa kwa kuwasambazia bidhaa
mbalimbali ili waweze kukua na kuongeza vipato vyao.
Naye mmoja wa wajasiriamali hao, ambaye ni Mkurugenzi wa
Kampuni ya Asaky’s Investment, Bi.Sophia Abdallah alisema wao kama wajasiriamali
wapo tayari kuyapokea mafunzo ili waweze kupata ujuzi wa kibiashara.
“Tunayofuraha kubwa kwa ujuzi tunaopatiwa hapa… tutaweza
kundeleza zaidi biashara zetu kwa manufaa yetu, jamii na taifa kwa ujumla,”alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment