Na
Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wizara
ya Mawasiliano, Sayansi na Teknolojia imesema mkakati wa Kilimo Kwanza
unaolenga kufikia mapinduzi ya kijani Tanzania ni moja vipaumbele vyake katika
juhudi za kuchangia maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Hii
ni kwa sababu sekta hiyo ya kilimo inabeba maisha ya watu wengi hapa nchini na
ikiendelezwa vizuri ina uwezo wa kubadilisha maisha ya wananchi wengi katika
nchi hii ambayo ina ardhi kubwa yenye kufaa kwa kilimo.
“Tumejipanga
kutumia fungu la serikali kwa ajili ya utafiti na maendeleo kusaidia tafiti
zitakazosaidia maendeleo ya wananchi na taifa kwa ujumla na Kilimo Kwanza ni
moja ya vipaumbele vyetu,” Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Dkt. Florens Turuka
aliwaambia waandishi wa habari jana.
Kilimo
Kwanza ni mkakati wa serikali unaolenga kutumia kilimo kama daraja la kufikia
mapinduzi ya uchumi hapa nchini kwa kukigeuza kilimo kuwa cha kisasa zaidi kwa
faida ya watanzania na taifa lote kwa ujumla zikihusishwa sekta binafsi na ile
ya umma.
“Tumeamua
kutumia fedha hii ya serikali inayolenga utafiti na maendeleo kusaidia tafiti
zinazolenga kufanikisha Kilimo Kwanza,” alisema Dkt. Turuka.
Aliyataja
baadhi ya maeneo ambayo yanapewa kipaumbele kama utafiti kuhusu pembejeo na
masoko ya mazao.
“Unatakiwa kuwa na soko la uhakika ili
kufanikiwa katika kilimo,” alisema, na kufafanua kwamba unaweza kuwa na mazao
mengi lakini kama huna soko la uhakika inakua haina faida sana.
Alieleza kwamba hii ndio sababu Wizara
yake imeamua kusaidia tafiti zinazolenga kuibua fursa za masoko kwa faida ya
watanzania na wadau wote wanaojihusisha na kilimo.
Aliyataja maeneo mengine yanayolengwa
kama tafiti zinazohusiana na kuimarisha mnyororo ya thamani na kuongeza bidhaa
za kulimo thamani.
Takwimu zinaonyesha kwamba
nchi zilizoendelea hutumia hadi dola za kimarekani 180 kuongeza thamani tani
moja ya mazao wakati nchi zinazoendelea hutumia dola 40 tu kuongeza thamani
katika tani moja ya mazao ya kilimo.
“Eneo hili la kuongeza
thamani mazao ni la muhimu sana kufanyia utafiti zaidi…ndio maana tunalipatia
kipaumbele,” alisema.
Kwa mujibu wa wataalamu,
bado kilimo cha Tanzania kinategemea sana wakulima wadogowadogo na kinachangia
asilimia 50 ya pato la taifa na kuendesha maisha ya asilimia 80 ya wananchi
wote.
Mwisho
No comments:
Post a Comment