Na Mwandishi wetu,
Dar es Salaam
Nafasi ya Tanzania
kuwa kitovu cha huduma za mawasiliano katika Kanda ya Afrika Mashariki, Kati na
Kusini inazidi kuwa kubwa kutokana na kuendelea kuimarika kwa mtandao wa Mkongo
wa Taifa wa Mawasiliano.
Tayari Mkongo huo
umeunganishwa na mikongo ya baharini ya SEACOM na The Eastern Africa Submarine
Cable System (EASSy) na baadaye mkongo wa The East African Marine System (TEAMS).
Akiongea na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki Katibu Mkuu wa
Wizara ya mawasiliano, Sayansi na Teknolojia, Dkt. Florens Turuka alisema
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano umefika makao makuu ya mikoa yote ya Tanzania
Bara na baadhi ya makao makuu ya wilaya.
“Hapa nchini,
kampuni za simu za Airtel, Infinitty, Simbanet, Tigo, TTCL, Vodacom na Zantel
zimeunganishwa katika mkongo huu na zinatoa huduma zake kupitia mkongo huu
katika sehemu mbalimbali,” alisema.
Serikali kupitia
wizara hiyo na Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) tayari imejenga Mkongo wa Taifa
wa Mawasiliano wenye urefu wa kilometa 7,560, ambao unajumuisha kilometa 5,448
mpya zilizojengwa na kilometa 2,112 zilizojengwa na shirika la umeme (TANESCO)
katika njia kuu za umeme.
Akifafanua zaidi
alisema Mkongo huo umetoa fursa ya kuunganisha na mikongo au mifumo mingine ya
mawasiliano ya nchi jirani za Kenya (Namanga, Sirari na Horohoro), Rwanda
(Rusumo), Burundi (Kabanga), Malawi (Kasumulu), Zambia (Tunduma), Uganda
(Mutukula) na Msumbiji (Mtambaswala).
Alisema kampuni za
simu za MTL (Malawi); MTN (Zambia); MTN, RDB, Airtel, KDN, RwandaTel, na BCS
(Rwanda); UCOM na ECONET (Burundi) zimeunganishwa katika Mkongo wa Taifa wa
Mawasiliano.
Dkt. Turuka alisema
kuwa uwepo wa Mkongo huo unawezesha utoaji wa huduma za mawasiliano katika
masuala ya fedha, elimu, afya, kilimo, biashara, utalii kwa njia mtandao.
Serikali imeipa
jukumu Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kuendesha, kuendeleza na kusimamia
huduma zinazotolewa na Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwa ujumla wake.
Alisema kutokana na
mazingira mazuri ya kuendeleza sekta ya mawasiliano, mikongo ya mijini (metro
networks) imeanza kujengwa na sekta binafsi ili kutumia vyema zaidi mkongo wa
taifa wa mawasiliano katika kutoa huduma za mawasiliano.
Akitoa mfano alisema
ujenzi wa metro network ya Dar es Salaam yenye urefu wa kilometa 90 iliyojengwa
na muungano wa kampuni za simu tatu imekamilika na hivi sasa mtandao huo
umeanza kutumika.
Inatarajiwa kuwa
mikongo mingine ya mijini itajengwa katika miji ya Arusha, Mwanza, Dodoma,
Morogoro na Mbeya katika siku zijazo.
Sekta ya mawasiliano imekua ikikua kwa kasi katika miaka ya
hivi karibbuni.
Kwa mujibu wa wizara
hiyo, sekta imeonyesha kukua haraka zaidi kwa wastani wa asilimia 21 kwa miaka
5 mfululizo hadi mwaka 2011 ikilinganishwa na sekta nyingine za uchumi.
Mchango wa sekta
katika Pato Ghafi la Taifa (Gross Domestic Product) umekua kutoka asilimia 1.7
(2005) hadi kufikia asilimia 2.7 (2009).
Matumizi ya simu
hivi sasa ni zaidi ya asilimia 50 ya Watanzania ikilinganishwa na asilimia 3
katika miaka michache iliyopita.
Kwa upande wa
intaneti watumiaji wameongezeka kutoka wastani wa 25,000 kwa mwaka 1999 hadi
kufikia watumiaji zaidi ya 4,800,000 mwaka 2012.
Ends
No comments:
Post a Comment