Thursday, July 26, 2012

TIC yawakikishia ushirikiano wawekezaji


Na Mwandishi wetu, Bagamoyo

Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kimeimwagia sifa kampuni ya Agro EcoEnergy Tanzania Limited kwa maendeleo mazuri yanayolenga kutekelezwa kwa uwekezaji mkubwa wa kilimo cha umwagiliaji cha zao la miwa katika bonde la Mto Ruvu wilayani Bagamoyo mkoani Pwani.
Kwa sababu hiyo, TIC imesema kwamba iko tayari kuisaidia kampuni hiyo na wawekezaji wengine watakao onekana kufanya vyema katika miradi yao kwa faida ya pande zote mbili. 
Mara uzalishaji wa mradi huu unaotarajiwa kuanza mwaka 2014 utakapoanza inatarajiwa kuongeza uzalishaji wa bidhaa za sukari, nishati ya umeme na mafuta aina ya ethanol ambayo yana uwezo wa kuendesha magari.
Sifa hizo zilitolewa na Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa TIC, Bw. Raymond Mbilinyi alipofanya ziara ya kuangalia maendeleo ya mradi huo mkubwa wa kilimo cha kisasa cha miwa jana wilayani Bagamoyo.
“Inatarajiwa kwamba mradi huu utazalisha  sukari tani 150,000 kwa mwaka, mafuta ya ethanol pamoja na Megawati 30 za umeme,” alisema.
Kati ya Megawati hizo, 15MW zitatumika kwa ajili ya uzalishaji katika kampuni hiyo na zilizobaki zitatumika kwa ajili ya wakaazi wa jirani.
Alisema jukumu la serikali ni kuhakisha inatoa msaada kwa mradi huo kwa vile ni silimia 60 tu ya sukari inayotumika inazalishwa  hapa nchini wakati asilimia 40 inatoka nje.
Alisema mradi huo ukianza kuzalisha kwa mafanikio utasaidia kupunguza mfumuko wa bei  kwa vile bidhaa hiyo ni moja inayochangia mfumuko wa bei mara pale inapokuwa adimu.
Akifafanua zaidi alisema kati ya bidhaa zinazo changia kuwepo mfumuko wa bei ni sukari na mchele na serikali imeliaona hili na kuwa inajitahidi kukuza uwekezaji katika eneo hilo.
“Tunapenda kasi ya uzalishaji iendelee kuwa kubwa na serikali itahakikisha vikwazo vyote vinatatuliwa ili kuhakikisha malengo ya uwekezaji yanatimia kwa ajili ya maendeleo ya nchi,” alisema. Bw. Mbilinyi.
Alisema kufanikiwa kwa mardi huo kutaleta mafanikio makubwa katika uchumi wa nchi kwa kuwa wakulima zaidi ya 300 watapata ajira na kupata mahitaji mbalimbali.
Mwenyekiti Mtendaji wa kampuni hiyo, Bw. Per Carstedt alisema wamekuja kuwekeza katika mradi mkubwa wa kilimo cha kisasa cha umwagiliaji cha zao la miwa kwa ajili ya soko la ndani la nchi.
“Hii itasaidia kupunguza kuagiza nje ya nchi bidhaa mbalimbali kama mafuta na sukari,” alisema na kuongeza kwamba hii itasaidia kutoa mchango kwa maendeleo kwa kiwango kikubwa.
Alisema zao la miwa linachukuwa miezi 12 kukua tangu kupanda na hadi kuvuna na kwamba wanatarajia kuzalisha aina tano za miwa.
Mwisho

No comments: