Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Uendelezaji wa Bonde la Mto Rufiji (RUBADA) imetiliana
saini ya makubaliano ya awali ya uzalishaji nishati ya umeme kupitia mradi wa
Stiegler’s Gorge na Kampuni ya Odebrecht International ya Brazil.
“Leo tunayo furaha kusaini makubaliano ya awali ya kuanza
kutekeleza maradi mkubwa wa Stiegler’s ambao una uwezo wa kuzalisha umeme wa megawati
2100 katika Bonde la Mto Rufiji na Kampuni iliyobobea katika uzalishi nishati
kwa kutumia nguvu ya maji,”alisema Bw. Aloyce Masanja, Mkurugenzi Mkuu wa
RUBADA baada ya tukio hilo jijini Dar es Salaam hivi karibuni.
Alisema makubaliano hayo yanatoa fursa kufanyika upembuzi
yakinifu kupitia ule uliofanywa awali na kampuni ya NORCONSULT ya Norway miaka
ya 1980 na kufanyiwa maboresho na baada
ya miezi sita kampuni hiyo itakabidhi ripoti ya kwanza.
Alisema awamu ya pili itahusisha mkataba wa kibiashara kwa kuangalia maji, teknolojia
itakayotumika, vyanzo vya fedha na utunzaji wa vyanzo vya maji ili kukabiliana
na mabadiliko ya tabia nchi.
Alisema ni lazima suala la mazingira lipewa kipaumbele kwa
sababu mradi wa Stiegler’s upo katika hifadhi ya Selou na bonde hilo pia ni
muhimu kwa kilimo.
Alisema hatua ya tatu itakuwa ni kuanza ujenzi wa mradi
wenyewe na matarajio ni kuanza baada ya miaka miwili kuanzia sasa.
Alisema mradi unatarajia kughalimu fedha za Kimarekani
bilioni mbili ingawa ghara inaweza kubadilika kutokana na teknolojia
itakayotumika.
Alisema Bonde la Mto Rufiji linapita katika mikoa nane na
linakaliwa na watu milioni nane hivyo kukamilika kwa mradi huo kutakuwa na msada
mkubwa katika shughuli za maendeleo.
Mkurugenzi wa Biashara wa Odebrecht, Bw. Fernando Soares alisema
kampuni yao imetia saini kutekeleza maradi huo ili kuzalisha nishati ya umeme
ambayo itachangia kuimarika kwa viwanda na hatimaye kukuza uchumi wa Tanzania.
“Hatua hii tuliyofikia ni muhimu kwa RUBADA na Serikali ya
Tanzania na matarajio ni kuona mradi huu unafanyaka vizuri na kusaidia nchi hii,”alisema
Bw. Soares.
Alisema kwa upande wao wamejidhatiti kutokana na ujuzi
walionao katika kuzalisha nishati ya umeme kupitia nguvu ya maji na wamekuwa wakifanya
kazi hiyo kwa muda mrefu katika mataifa mbalimbali duniani.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi RUBADA, Profesa Raphael
Mwalyosi aliiomba Serikali na wadau wote wa nishati nchini kuunga mkono
jitihada za utelezaji maradi huo mkubwa ambao utaweza kukabili tatizo la umeme
nchini.
“Ninawaomba tusiogope kutekeleza mradi huu, kikubwa ni kuwa
na mipango ya kulinda vyanzo vya maji na Wakuu wa Mikoa ambao mikoa yao ni vyanzo
vya maji yanayoingia katika Bonde la Mto Rufiji wawe makini katika jambo hili,”
alisema.
Balozi wa Brazil nchini Tanzania,Bw.Francisco Luz alisema makubaliano yaliyofanywa na RUBADA na
Kampuni ya Odebrecht yanalenga kuzidi kujenga mahusiano na kuchochea shughuli
za uchumi Tanzania.
Alisema kampuni hiyo ya Brazil ilifika Afrika miaka 30
iliyopita na kufanya kazi katika nchi mbalimbali na nchi Tanzania imejipanga
kutekeleza mradi huo muhimu kwa ufanisi mkubwa.
No comments:
Post a Comment