Nyumba bora ni kati ya vitu muhimu
kabisa kwa binadamu tangu enzi na enzi.
Ndio maana jamii na serikali za dunia hii zinajitahidi kupitia programu
mbalimbali kuhakikisha watu wake wanaishi katika makazi bora. Kama moja ya wadau wa sekta binafsi,
Benki ya Afrika Tanzania imekuwa pia ikijitahidi kusaidia juhudi hizi za
serikali na watanzania kwa ujumla kuwa na nyumba bora kwa gharama nafuu. Katika kufanikisha swala hili, hivi
karibuni benki ilinunua hisa toka kampuni ya Tanzania Mortgage Refinance
Company (TMRC) ili kuimarisha mikopo yake ya nyumba kama mwandishi wetu
anavyooelezea…
Malazi, mavazi na chakula ndio vitu
vitatu muhimu kwa binadamu.
Ndio maana jamii na serikali
mbalimbali duniani zimekuwa zikifanya kila liwezekanalo kuhakikisha mahitaji
hayo yanapatikana kwa urahisi na kwa ubora.
Pamoja na kwamba Serikali ya Tanzania
inalishughulikia hili kupitia taasisi zake mbalimbali, pia imeruhusu sekta
binafsi kusaidia katika juhudi hizo.
Benki ya Afrika Tanzania ni moja ya
wadau hao ambao wamedhamiria kusaidia juhudi za kuwawezesha watanzania kuwa na
makazi bora na hivyo kusaidia serikali na kufikia malengo ya milenia.
Chombo hiki cha fedha kimejizatiti
kutoa mikopo ya nyumba ili kuwawezesha watanzania kuwa na nyumba nzuri kwa
makazi ambayo ni muhimu kwa maendeleo ya watu binafsi na taifa kwa ujumla.
Katika juhudi za kuimarisha mikopo yake ya nyumba benki hiyo
imewekeza shilingi bilioni moja na kupata umiliki wa hisa asilimia 9.57 za
Tanzania Mortgage Refinance Company (TMRC) ambapo sasa benki itakuwa na fursa
ya kukopa fedha kutoka kampuni hiyo ili kuendeleza utoaji wa mikopo ya nyumba
kwa mafanikio zaidi.
Akiongea wakati wa uzinduzi wa uwekezaji huo hivi karibuni, Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Afrika Tanzania, Bw. Ammish Owusu-Amoah alisema hatua hiyo
imefikiwa kwa lengo la kuendelea kuboresha huduma ya mikopo kwa wateja wake na
watanzania kwa ujumla.
“Ninayo furaha kutangaza kuwa sasa tutakuwa na nafasi nzuri
ya kuendelea kutoa mikopo ya nyumba kwa vile benki yetu imejiunga na TMRC
ambapo tutakuwa na fursa ya kukopa fedha kwa ajili ya kutoa huduma hii muhimu
ya mikopo kwa wateja wetu na watanzania kwa ujumla,” anasema Bw. Amoah.
TMRC ni kampuni inayotoa mikopo ya nyumba kwa mabenki ambao
ni wanachama wake ili hatimaye benki hizo ziweze kutoa mikopo ya nyumba ya muda
mrefu kwa wateja na watanzania kwa ujumla.
Anasema benki inatoa mikopo ya kununua nyumba, kukarabati
nyumba, kumalizia kujenga na kuweka nyumba kama amana ya kupata fedha kwa ajili
ya shughuli za maendeleo.
Anasema lengo la kufanya hivyo ni kutaka kuwawezesha wateja
wao na watanzania kumiliki nyumba nzuri na kuwa na shughuli mbalimbali za
maendeleo ili kupiga vita hali duni ya vipato miongoni mwao na wakipata
mazingira mazuri ya kuishi itatoa fursa kwa afya zao na kufanya kazi za
kujipatia maendeleo kwa bidii.
“Ni hatua nzuri kuona wadau wengi tunashiriki katika sekta
hii ya mikopo ya nyumba na benki yetu haiko nyuma katika mchakato huu ambao ni
muhimu kwa maendeleo ya wateja wetu na watanzania wote kwa ujumla,” anasema Bw.
Amoah.
Mkopaji atahitajika kurejesha mkopo wa kununua nyumba kwa
muda wa miaka 15 na ule wa kuweka nyumba kama amana ya kupata fedha, kukarabati
nyumba na kumalizia kujenga utalipwa kwa kipindi cha miaka 10.
Ushirika uliopo katika sekta hiyo unasaidia wadau wa TMRC
kuunga mkono juhudi za serikali ya Tanzania kuwa na nyumba bora na kuleta sura
mpya kwa watanzania ambao wanakabiliwa na tatizo la kupata fedha kwa mara moja
na kujenga nyumba za zinazostahili kulingana na mazingira ya sasa.
No comments:
Post a Comment