Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Chuo Kikuu Mzumbe ni moja ya taasisi za elimu kumi duniani zilizochaguliwa
kuanzisha mradi wa majaribio wa kufundisha kozi zinasosaidia kujenga maadili ya
Kuzuia na Kupambana na rushwa nchini katika ngazi ya shahada ya uzamili.
Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam, Profesa
Andrew Mbwambo alisema hayo jijini Dar es Salaam jana mbele ya waandishi wa
habari.
Kozi hiyo itatolewa chuoni hapo kuanzia mwaka ijao wa masomo
kwa wanafunzi wa shahada ya uzamili ya masomo ya menejimenti na biashara.
“Mradi huu umeanzishwa na Umoja wa Mataifa na kuvichagua vyuo
vya biashara Afrika kuanza kuutekeleza kwa majaribio,” alisema Prof. Mbwambo na
kuzitaja nchi nyingine barani Afrika zitakazoendesha kozi hiyo kuwa ni Afrika
ya Kusini na Nigeria.
Alisema vyuo hivyo vikiweza kutekeleza kwa ufanisi, mradi huo
utasambazwa kenye vyuo vingine Afrika ili kuweza kuwajenga wanafunzi na wasomi
wa taaluma ya biashara kuwa na maadili ya kuzuia na kupambana na rushwa.
Akitoa mfano juu ya swala hilo alisema watu wanasoma taaluma
za biashara hawana bodi za kitaaluma kwa ajili ya kulinda maadili yao ya kazi kama
ilivyo kwa madaktari, wahandisi na wanasheria ambao wana bodi za kitaaluma,
jambo alilosema halitakiwi.
Akielezea zaidi alisema kwa kuanzia, Chuo hicho kimetoa mafunzo
ya kuwajengea uwezo maafisa waandamizi wa jeshi la polisi na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).
Alisema chuo kwa sasa kinajipanga kupata na kuuangalia mtaala
kutoka mpango huo wa Umoja wa Mataifa na kuuingiza katika mtaala wa chuo kwa ajili
ya kufundishia wanafunzi na kuanzisha kozi fupi kwa ajili ya kuwapatia mafunzo watu
mbalimbali katika sekta ya umma na binafsi wakiwemo wabunge.
Alisema kampasi yao ilipata bahati kwa Mkuu wao wa Kozi fupi
na Ushauri ,Profesa Shiv Tripath kushiriki katika kuandaa mtaala huo na chuo
kikawa miongoni mwa vyuo vitatu vilivyo chaguliwa Afrika katika mradi wa
majaribio.
Mmoja wa waanzilishi wa mpango huo ambaye pia ni mhadhiri wa
Chuo Kikuu cha New York, Marekani, Profesa Ronald Berenbeim alisema swala hilo
halikuanzishwa kwa kuangalia rushwa iliyoko Afrika, bali lengo lake ni kutoa
mafunzo ya kujenga maadili dhidi ya rushwa kwa watumishi wa umma na sekta
binafsi.
“Tumekichagua Chuo kikuu Mzumbe Kampasi ya Dar es Salaam kwa
mradi wa majaribio na vyuo vingine vitatu Afrika ili waweze kuingiza katika
mitaala yao swala la vita dhidi ya swala hili la kuzuia na kupambana na rushwa
katika taaluma za biashara,” alisema.
Akiongea wakati wa mafunzo kwa jeshi la polisi, Mkuu wa
Kitengo cha Maadili cha Jeshi la Polisi, Bw.Patrick Byatao alisema mafunzo hayo
yanalenga kuzidi kuwakumbusha juu ya maadili katika kutekeleza majukumu yao
pamoja na kwamba wana miiko ya jeshi.
Alisema mafunzo hayo ni muhimu, na yalikuwa yanawakumbusha baadhi
ya polisi wanaojisahau na kujiingiza katika vitendo vya rushwa kurudi katika
maadili ya jeshi hilo.
No comments:
Post a Comment