Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Rasilimali watu iliyo bora imetajwa kama moja ya siri za
mafanikio ya Benki ya Afrika Tanzania.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo, Bw. Ammish
owusu-Amoah wakati wa sherehe ya mwaka ya wafanyakazi wa benki hiyo
iliyohusisha pia familia zao hivi karibuni jijini Dar es Salaam.
“Tunatambua na kujali watu wetu, mafanikio ya benki yetu
yamechangiwa sana na utendaji kazi bora wanaouonyesha,” alisema Bw. Amoah.
Alisema sherehe hizo zinahusisha wanafamilia kwa kuwa wana
mchango mkubwa sana katika kuwaongezea ari na kuwapatia moyo wafanyakazi wa
benki katika utendaji wao wa kila siku.
“Ninawahamasisha kufanya kazi kwa bidii zaidi kwa faida yetu
sote na kwa faida ya taifa zima kwa ujumla,” alisema.
Sherehe hizo pia zilishuhudiwa kutolewa tuzo kwa wafanyakazi
mbalimbali baada ya kufanya vyema katika nafasi zao za kazi.
Mmoja wapo alikuwa Bi. Sophia Mwema aliyetangazwa kuwa
mfanyakazi bora idara ya Rasilimali Watu na Utawala.
“Nina furaha kubwa…sikutegemea,” alisema Bi. Mwema, na
kuongeza kwamba hii itamfanya kuongeza bidii zaidi.
Mwingine aliyetambuliwa alikuwa, Bw. Masumbuko Humuli aliyekuwa
mfanyakazi bora kutoka idara ya Fedha na Uhasibu ambaye kwa upande wake alitoa
wito kwa wafanyakazi wenzake kushirikiana zaidi ili kuifanya benki hiyo
kufanikiwa zaidi katika wakati huu wa ushindani mkubwa.
Benki ya Afrika Tanzania imekuwa ikijitahidi kujitanua na
kuimarisha huduma zake katika miaka ya hivi karibuni.
Tangu ianzishwe hapa nchini mwaka 2007, imeshafanikiwa
kufungua matawi kumi mkoani Dar es Salaam na sita nje ya mkoa huo yakiwepo ya Morogoro,
Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya and Arusha.
Benki hii ni moja ya mtandao wa kibenki unaofanya kazi katika nchi 15 ambazo
ni pamoja na Benin, Burkina Faso, Ghana, Ivory Coast,
Mali, Niger na Senegal. Nyingine
ni Burundi, Djibouti, Kenya, Madagascar, Tanzania na Uganda.
Pia ina tawi katika nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya
Kongo.
No comments:
Post a Comment