Sunday, March 10, 2013

PASS kufufua miradi ya umwagiliaji nchini, kusaidia wakulima wadogo



Mjumbe wa Bodi ya wadhamini ya Asasi ya Kusaidia Uwekezaji Kwenye Kilimo (PASS Trust), Bw. Salum Diwani (kushoto) akibadilishana mawazo na Mkurugenzi Mtendaji wa Asasi hiyo Bw. Iddy Lujina muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha bodi hiyo mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.




Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Asasi ya Kusaidia Uwekezaji Kwenye Kilimo (PASS) imetenga shilingi bilioni 4 kwa ajili ya kutoa huduma mpya ya mikopo ya Karadha ili kusaidia kufufua miradi ya umwagiliaji na wakulima wadogo wadogo hapa nchini kwa mwaka huu.
Kwa kuanzia, mikopo hiyo ya karadha itaanza kusaidia juhudi za kufufua mradi wa umwagiliaji Moshi katika mazao ya mpunga na mahindi kwa kutoa Tshs 400 milioni mwezi ujao ili kupata matrekata na vifaa vya kuvunia mazao.
Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini PASS, Profesa Andrew Temu aliwaambia hayo waandishi wa habari mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam mara baada ya kikao cha bodi ya wakurugenzi wa asasi hiyo.
“Kikao chetu cha bodi kimeamua kuanzisha mikopo ya karadha ambayo imeanza na ukanda wa kaskazini wa nchi ambapo kupitia fedha hiyo mradi huo utapata matrekta nane na vivunio sita,” alisema.
“Huu ni mfumo wa karadha ambapo wakulima baada ya kurejesha mikopo yao vifaa hivyo vitakuwa vya kwao,” alisema na kuongeza kuwa mikopo hiyo ya vifaa vya kilimo itasaidia sana pia na wakulima wadogo wanaoishi katika na pembezoni mwa mashamba hayo makubwa ya umwagiliaji maana wao hawana uwezo wa kupata vifaa hivyo.
Alisema awamu ya pili itahusisha kiasi cha Tshs 800 milioni katika kanda hiyo.
Alisema baada ya ukanda huo asasi hiyo italenga pia kanda nyingine kama vile mradi wa umwagiliaji wa Dakawa, Morogoro kwa kilimo cha mpunga; Mradi wa umwagiliaji Madibira, Iringa na maeneo mengine.
Alisema asasi yao sasa itafanya kazi pia na benki za kijamii ikiwemo ya Kilimanjaro Community Bank LTD, Pride na nyingine mkoani Arusha ili kuwafikia kwa karibu wakulima wadogo.  
Pia asasi hiyo inashirikiana na benki nyingine kama CRDB, Exim Bank, TIB, NMB na NBC.
Alisema asasi yao inaunga mkono juhudi za serikali na mkakati wake wa kuendeleza kilimo katika ukanda wa kusini mwa Tanzania (SAGCOT) na kusema kwamba ili mpango huu uweze kufanikiwa kwa kiwango cha juu, unahitaji huduma za kibenki.
Mkurugenzi Mtendaji wa PASS, Bw. Iddy Lujina alisema kilimo cha Tanzania bado kipo chini na kinahitaji huduma za kibenki kufikia kilimo cha kisasa.
“Tumeshakamilisha kufanya maboresho kwenye tawi la Moshi na tunatarajia kufungua tawi la Mtwara ili lihudumie Lindi na Mtwara kwa ajili ya kusogeza huduma kwa jamii,” alisema na kuongeza kuwa kwa  sasa wanatafuta eneo kufungua tawi Kigoma ili kuhudumia pia mkoa wa Tabora.
Alisema baada ya kufungua matawi hayo watakuwa na tawi la Mwanza, Moshi, Morogoro, Dar es Salaam, Mbeya, Mtwara na Kigoma kwa lengo la kusaidia upatakanaji wa huduma za mikopo katika kilimo katika kanda zote hapa nchini.
Kupitia huduma zake, mwaka 2011 PASS ilisaidia wakulima 11,000 kupata mikopo yenye thamani ya Tshs 22 bilioni kutoka kwenye benki mbalimbali na mikopo hiyo ilipanda hadi kufikia Tshs 30 bilioni mwaka jana.

Hadi sasa, taasisi hiyo ina matawi katika mikoa ya Morogoro, Mbeya, Dar es Salaam, Mwanza, Moshi na Mtwara.

Katika miaka kumi iliyopita, PASS imeweza kusaidia wakulima zaidi ya 100,000 kupata mikopo na katika mpango wake mpya wa miaka mitano inatarajia kusaidia wakulima zaidi ya 300,000 kuweza kupata mikopo yenye thamani ya Tshs 290 bilioni.

Mwisho 

No comments: