Wednesday, March 27, 2013

TPSF yapania kujenga uwezo kwa wanachama wake




Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (tpsf), Godfrey Simbeye ikisisitiza jambo wakati wa mkutano maalumu wa kuwajengea uwezo wanachama wa taasisi hiyo katika kanda ya kaskazini, juu ya umuhimu wa kongano (clusters) na jinsi ya kuimarisha mabaraza yao ya biashara ya wilaya na mikoa ili kuwa na sauti moja yenye nguvu kwa taasisi hiyo, mkutano huo ulifanyika jijini Arusha jana na kujumuisha mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha.



Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Nchini (tpsf), Godfrey Simbeye ikisisitiza jambo wakati wa mkutano maalumu wa kuwajengea uwezo wanachama wa taasisi hiyo katika kanda ya kaskazini ,juu ya umuhimu wa kongano (clusters) na jinsi ya kuimarisha mabaraza yao ya biashara ya wilaya na mkoa ili kuwa na sauti moja yenye nguvu kwa taasisi hiyo, (kushoto) ni Mkurugenzi wa Bodi ya taasisi hiyo DKT. Gidion Kaunda. Mkutano huo ulifanyika jijini Arusha jana na kujumuisha mikoa ya Manyara, Kilimanjaro na Arusha.

Na Mwandishi Wetu, Arusha
Taasisi ya Sekta Binafsi nchini imesema itaendelea kuimarisha wanachama wake katika ngazi za kanda kwa kuwapa elimu ya biashara ili kukabiliana na soko la Afrika Mashariki linaloendelea kukua kwa kasi kwa sasa.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi hiyo Bw. Godfrey Simbeye aliyasema hayo jijini Arusha muda mfupi mara baada ya kukutana na wanachama wa kanda ya kaskazini ambapo pamoja na mambo mengine wametakiwa kuimarisha vyama vyao vya biashara katika ngazi ya mikoa na wilaya.
“Napenda tuelewe kuwa wanachama walioko katika kanda ya kaskazini wako mipakani hivyo ni jukumu letu kutoa elimu ya kibiashara ya jinsi ya wao kuingia katika ushindani wa soko la Afrika Mashariki,” alisema Simbeye.
Alisisitiza kuwa kwa sasa kuna programu maalumu ya kutoa elimu ya kuendeleza wafanyabiashara ijulikanayo kama (Trade Mark East Afrika) inayoangalia fursa zilizopo katika mikoa ya kanda ya kaskazini ili wafanya biashara wa ukanda huo waweze kuchangamkia na kunufaika na fursa zilizopo.
Aliongeza kuwa TPSF kwa kushirikiana na TCCIA katika ngazi ya kanda wameanzisha program nyingine ya kuendeleza wajasiriamali wadogo waweze kuzalisha na kuuza zaidi.
“Katika kuhakikisha kuwa wanachama wa TPSF wanakuwa kitu kimoja na kujenga sauti moja yenye nguvu, wajasiriamali wadogo wanaangaliwa kwa ukaribu hasa kwa kuanzisha  program mbalimbali za kuwainua kiuchumi katika maeneo yao ya biashara waweze kuingia katika kundi la wafanyabiashara wa kati,” alisisitiza.
Alisema programu kama hizo ni njia tu ya kuelekea katika kuimarisha uchumi wa nchi kupitia wafanya biashara wadogo ambao wakiwezeshwa kielimu na kimtaji wataweza kuwa wafanyabiashara wakubwa hapo baadae.
Akizungumzia mabaraza ya wilaya na mikoa, Bw. Simbeye aliyataka kufanya kazi kwa ukaribu zaidi na taasisi hiyo ikiwa ni katika kujenga umoja na nguvu zaidi katika mikoa na wilaya.
Alisema kwa sasa mabaraza hayo yamekuwa kimya kutokana na kutokutana mara kwa mara na kujadili mustakabali wa masuala mbalimbali ya kibiashara katika mikoa na wilaya zao.
“Kikubwa ninachotaka kuwaambia viongozi katika mabaraza ya biashara ya mikoa na wilaya wafanye mikutano kama katiba inavyoelekeza, mabaraza haya hajakaa kwa muda mrefu hivyo ni wakati wao wa kukutana na kujadili matatizo yaliyopo katika maeneo yao,” alisema Mkurugenzi huyo.
Akizungumzia umuhimu wa mabaraza hayo kwa uchumi wa taifa Bw. Simbeye alisema mabaraza ya wilaya na mikoa ni muhimu sana si kwa uchumi wa mkoa bali kwa taifa na hii ni kutokana na kuhusisha pande zote mbili za sekta ya umma na binafs katika kukaa na kujadili maendeleo ya wilaya na mkoa kwa ujumla.
Mkutano huo wa kuimarisha sauti moja ya taasisi ya sekta binafsi nchini kwa kanda ya kaskazini umejumuisha mikoa ya Arusha, Manyara na Kilimanjaro.
Wanachama wa taasisi hiyo walijadili mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na fursa mbalimbali za kiuchumi katika mikoa ya kanda hiyo pamoja na changamoto mbalimbali zinazowakabili.
Mwisho


No comments: