Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bw. Geofey Simbeye akisisitiza jambo kwa
wanachama wa taasisi hiyo wa kanda ya ziwa katika mkutano maalumu wa
uelimishaji na uhamasishaji wa muundo wa uwakilishi katika kongano ( clusters). Kulia ni Mkurugenzi wa Bodi ya TPSF Bw.
Gideon Kaunda. Mkutano huo ulifanyika
mwishoni mwa wiki jijini Mwanza.
Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya
Sekta Binafsi Tanzania (TPSF) Bw. Geofey Simbeye akizungumza na wanachama wa
taasisi hiyo kutoka kanda ya ziwa katika mkutano maalumu wa uelimishaji na
uhamasishaji wa muundo wa uwakilishi katika kongano( clusters) mwishoni mwa
wiki jijini Mwanza.
Na Mwandishi Wetu, Mwanza
Mchakato wa kuwa na sauti moja, imara
na yenye nguvu nchini kwa sekta binafsi unaendelea vizuri baada ya kuanza
mikutano ya uhamasishaji ya kikanda huku wanachama wa taasisi hiyo wakihimizwa
kuwa kitu kimoja ili kuingia katika ushindani wa soko la Afrika Mashariki.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mtendaji wa
taasisi ya sekta binafsi nchini (TPSF), Bw. Geofrey Simbeye, alisema mchakato
huo ulioanza mwaka 2011 lengo lake ni kuweka mazingira bora na wezeshi kwa
wanachama wake katika kuongeza kasi ya uanzishwaji wa makampuni na viwanda kwa
ajili ya kuongeza ajira na kuinua uchumi wa nchi.
“Pia kuishawishi serikali kuondoa
baadhi ya vikwazo katika ufanyaji biashara ndani na nje ya nchi,” alisema Bw.
Simbeye katika mkutano wa kanda ya ziwa ulioshirikisha wanachama hao jijini
Mwanza mwishoni mwa wiki.
Alisema TPSF inataka wanachama wake wafahamiane
katika ufanyaji biashara hasa katika mikoa iliyopo katika kanda moja pia kujenga
kongano (clusters) imara zitakazoweza kuwaunganisha katika sekta mbalimbali za
kiuchumi.
Aliongeza kuwa mikutano hiyo ya kanda
itahamasisha wawekezaji waliopo katika mikoa husika kuwekeza kutokana na fursa
zilizopo katika mikoa hiyo.
Akizungumzia kanda ya ziwa Mkurugenzi huyo
alisema kanda ya ziwa ni moja ya kanda zenye fursa nyingi za uwekezaji hapa
nchini, hivyo ni changamoto kwa wanachama wa TPSF katika mikoa hiyo kuungana
ili kuisaidia serikali katika kuweka mazingira bora na wezeshi ya kufanya
biashara na uwekezaji.
“Serikali inaitegemea sana sekta
binafsi katika kujenga uchumi wa nchi, kwa hiyo napenda niseme ya kwamba watu
wa kanda ya ziwa wana nafasi kubwa ya kuisaidia serikali katika kutekeleza
jukumu hilo,”aliongeza Mkurugenzi huyo.
Alisisitiza kuwa baada ya mikutano
hiyo ya kanda wanaamini watapata wawakilishi watakaoingia katika bodi ya TPSF
ambao watawakilisha kanda nane zilizoanishwa katika mtindo wa kongano na hivyo kuwa
na sauti moja itakayounganisha wanachama wote nchi nzima.
“Ukishakuwa na sauti moja katika
jambo lolote lile lazima utafanikiwa, tunaomba serikali iweze kuangalia
uwezekano wa kutupunguzia kodi kwa sisi watu wa sekta binafsi,” alisisitiza Bw.
Simbeye.
Aidha Bw. Simbeye aligusia suala la
uwajibikaji kwa wananchama wa taasisi hiyo katika kuchangia mawazo yao ili
kuleta mabadiliko ya kiuchumi si kwa TPSF tu bali na sekta nyingine za kiuchumi.
“Mimi siku zote nimekuwa nikihimiza
viongozi wa vyama vya biashara vya mikoa ambavyo ni wanachama wa TPSF kuwa kitu
kimoja ili serikali iendelee kuiamini sekta yetu katika kuendelea kubadili
uchumi wa nchi hii,” aliongeza.
Mkutano huo wa siku moja uliofanyika
jijini Mwanza ulikuwa na lengo la kuelimisha na kuhamasisha muundo wa
uwakilishi katika kongano (clusters) na kuhusisha mikoa ya Kagera, Mara, Shinyanga, Simiyu, Geita na
Mwanza, ambayo inaunganisha kanda ya ziwa.
Mwisho
No comments:
Post a Comment