Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akimsikiliza Kaimu
Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova (kushoto)
wakati wa mkutano wa maswala ya usalama na uwekezaji mwishoni mwa wiki jijini
Dar es Salaam.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi (kulia) akimsikiliza Kaimu
Kamishna wa Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova (katikati)
wakati wa mkutano wa maswala ya usalama na uwekezaji mwishoni mwa wiki jijini
Dar es Salaam. Kushoto ni Mwakilishi
Mkuu wa maswala ya uchumi na biashara wa China nchini Tanzania, Bw. Lin
Zhiyong.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imesema itahakikisha
inaimarisha uhusiano wake na wawekezaji toka China kwa manufaa ya nchi zote
mbili.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa Kituo cha
Uwekezaji Tanzania (TIC), Bw. Raymond Mbilinyi amesema katika mkutano wa
maswala ya usalama na uwekezaji mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam kuwa
serikali itatumia uwekezaji na biashara baina ya nchi hizo kama moja ya njia za
kuimarisha uhusiano wa muda mrefu kati ya mataifa hayo.
Mkutano huo uliolenga wawekezaji wa
Kichina wanaoishi Dar es Salaam ulihudhuriwa na maafisa mbalimbali wa serikali
kutoka polisi, TIC, uhamiaji na idara ya kazi.
“Maeneo haya ya uwekezaji na biashara
yana uwezo wa kuimarisha uhusiano wetu kwa kiwango kikubwa,” alisema.
Mkutano huo uliandaliwa kwa
ushirikiano kati ya Kituo cha Biashara cha China nchini Tanzania (CBCT) na TIC
kwa lengo la kuimarisha ushirikiano kati ya CBCT na idara mbalimbali za
serikali ya Tanzania.
Bw. Mbilinyi alimshukuru Rais Jakaya
Kikwete kwa juhudi zake katika kuimarisha uhusiano na nchi hiyo ambayo ni
miongoni mwa zenye uchumi mkubwa kabisa duniani na kuwataka wawekezaji hao
kulenga sekta zinazozalisha ajira kwa wingi kama vile uzalishaji na ujenzi.
“Tunapenda kusisitiza ushirikiano na
wawekezaji wa ndani ili kuleta mafanikio makubwa zaidi,” alisema Bw. Mbilinyi
na kuongeza kuwa kama wawekezaji hao watafuata sheria na taratibu za nchi
watafanikiwa katika malengo yao.
Mwenyekiti wa CBCT, Bw. Janson Huang
alisema siku zote nchi ya China itaheshimu uhusiano wa siku nyingi kati ya
pande hizo na kwamba wataonyesha kwa vitendo heshima hiyo kwa kuajiri
wafanyakazi wazalendo katika kampuni zao hapa nchini na kujihusisha katika
kutoa misaada mbalimbali ya kiutu hapa nchini.
Bw. Huang alisema kuwa usalama ni
swala muhimu sana katika kuendesha biashara na akapendekeza kuanzishwa kwa
kituo cha ushirikiano kati ya polisi na jumuia ya wachina hapa nchini
kushughulikia maswala ya kiusalama ya kila siku yanayowahusu.
Pia alitoa ombi kwa serikali ya
Tanzania kuangalia jinsi ya kurahisisha taratibu nzima za kutoa vibali
mbalimbali kwa wawekezaji hao ili kuimarisha zaidi ushirikiano.
Kwa upande wake, Kaimu Kamishna wa
Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Bw. Suleiman Kova alisema kwamba kikosi
chake kiko tayari kulinda wawekezaji na mali zao ili kuhakikisha mazingira ya
uwekezaji yanaboreka zaidi na hivyo kukuza uchumi wa nchi.
Hata hivyo, alitoa angalizo kuwa ni
lazima wawekezaji hao kufuata sheria na taratibu za nchi na kwamba kamwe wasiwe
chanzo cha matatizo.
“Tutazidi kushirikiana na idara
nyingine za serikali kuhakikisha kuwa wawekezaji wanakua salama,” alisema.
Uhusiano
kati ya Tanzania na China ni wa kihistoria na uliasisiwa na viongozi,
Mwenyekiti Mao Zedong wa China na Rais Julius Nyerere na kudumu zaidi ya miaka
hamsini hadi sasa.
China
imekua ikijihusisha na miradi mbalimbali hapa nchini.
Takwimu
zinaonyesha kuwa uwekezaji wa China hapa nchini umekua thabiti katika miaka ya
hivi karibuni, nchi hiyo ikiwekeza miradi yenye thamani ya zaidi USD bilioni
moja kupitia kampuni zaidi ya 300 na kutengeneza ajira zaidi ya 80,000 kwa
watanzania.
Hivi
karibuni, nchi hiyo iliipatia Tanzania mkopo wa dola za kimarekani 1.01 bilioni
kugharamia ujenzi wa bomba la gesi lenye urefu wa kilometa 522 kutoka Mtwara
hadi Dar es Salaam kwa riba ya asilimia 3 tu.
Mradi
huo unatarajiwa kumaliza tatizo sugu la umeme hapa nchini na hivyo kuimarisha
uchumi.
Mwisho
No comments:
Post a Comment