Wednesday, March 13, 2013

Uhusiano wa wazazi, watoto muhimu kwa maendeleo shuleni



Mkuu wa Shule ya Ndetembia Matemu iliyo katika eneo la Kihonda katika Manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro, Ms. Christina Gumbo akisisitiza jambo wakati akielezea maendeleo ya elimu katika shule yake pamoja na maoni yake jinsi ya kuimarisha sekta hiyo hapa nchini jana mjini Morogoro.

The Head Teacher of Ndetembia Matemu primary school in Kihonda, Morogoro region, Ms. Christina Gumbo stresses something when talking to journalists yesterday in Morogoro on matters related to education development in the country.

Na Mwandishi wetu, Morogoro

Wakati wadau wa elimu nchini wakilalamikia kushuka kwa kiwango cha elimu na ufaulu mdogo katika mitihani ya kitaifa, wazazi na walezi wametakiwa kuwa karibu na watoto wao ili kuleta mabadiliko haraka katika sekta hiyo muhimu kwa maendeleo.

Mwalimu Mkuu wa Shule ya Ndetembia Matemu iliyopo katika eneo la Kihonda katika manispaa ya Morogoro Mkoani Morogoro, Bi. Christina Gumbo alitoa wito huo kwa waandishi wa habari wakati akitoa maoni yake kuhusiana na maendeleo ya elimu katika shule yake na hapa nchini kwa ujumla.

“Sekta binafsi inatakiwa ijikite zaidi katika kuwekeza zaidi kwenye elimu, lakini na wazazi wahimize watoto wao kukazania elimu kwa kuwa ndio itakayowasaidia kubadilisha hali ya uchumi katika nchi,” alisema Mwalimu Gumbo.

Aliongeza kuwa msingi bora wa kumlea mototo unaanzia nyambani, hivyo ni vema wazazi wakawakumbusha kila mara watoto umuhimu wa elimu na mustakabali wa maisha yao ya baadae ili waweze kuzingatia kile wanachopewa na walimu wawapo masomoni.

“Mwalimu ni mzazi wa pili awapo shuleni, sisi pia tunafundisha kama wazazi tofauti ni kwamba hapa shuleni masomo na nidhamu ndio yanazingatiwa kwa umakini wa hali ya juu,” alisisitiza mkuu huyo wa shule.

Akizungumzia lengo la kuanzishwa kwa shule hiyo alisema wameitikia sera ya serikali ya kuwekeza katika elimu kutokana na uhaba uliopo wa shule za msingi na sekondari katika katika halmashauri na manispaa mbalimbali hapa nchini.

“Siku zote serikali imekuwa ikihimiza wadau mbalimbali kujenga shule bora na zenye kiwango ili kuongeza fursa za masomo hapa nchini,” alisema.

Matokeo ya kidato cha nne ya hivi karibuni yamelalamikiwa sana na wadau mbalimbali hapa nchini wakidai ni kutokana na nidhamu isiyoridhisha miongoni mwa wanafunzi, wazazi kutokua karibu na watoto miongoni mwa sababu nyingine.

Shule hiyo iliyoanzishwa mwaka 2010 ina wanafunzi 177 kuanzia chekechea hadi darasa la nne.

“Ni lengo letu kutayarisha wanafunzi watakaokua na uwezo na kufanya vyema katika masomo yao,” alisema.

Mwisho

No comments: