Thursday, February 28, 2013

Pinda ahamasisha wafanyabiashara kutumia barcode ya Tanzania


Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa wito kwa wafanyabiashara  watanzania kuanza kutumia alama ya kiambishi anuani (Barcodes) ya hapa nchini kwa faida yao na ustawi wa taifa kwa ujumla.
Waziri Mkuu alitoa wito huo jana jijini Dar es Salaam wakati akizindua Mpango mkakati wa miaka mitano 2013/2017 wa GSI (TZ) National Ltd.
 GSI (TZ) National Ltd ndio inayohusika na mfumo wa kimataifa wa utambuzi na bidhaa kwa kutumia nembo za mstari (Barcodes).
“Nchi yetu imeingia katika mfumo huu ambao utasaidia kuimarisha ushindani wetu katika soko la ndani na nje,” alisema.
Tanzania ilifanikiwa kuingia katika mfumo huo baada ya kutimiza mashari ya kuwa mawanachama wa Global Standard One (GS1) yenye makao makuu yake nchini Ubelgiji.
Alama ya kiambishi anuani au barcode husaidia kutambulisha bidhaa husika katika soko na kwa muda mrefu Tanzania imekuwa ikitumia alama za nchi nyingine katika bidhaa zake.
Hata hivyo, kuanzia mwezi Agosti 2011, Tanzania kupitia GS1 (TZ) National Ltd ilifanikiwa kuanza kutoka alama hiyo, hatua inayotegemewa kuongeza kuaminika kwa bidhaa za hapa nchini kitaifa na kimataifa na hivyo kuchochea kukua kwa uchumi wa wafanyabiashara pamoja na nchi. 
Namba ya utambulisho ya alama ya kiambishi anuani ya Tanzania ni 620.
Waziri Mkuu Pinda alisema ni muhimu kwa wafanyabiashara wote sasa kuingia katika mfumo huo kwani utawawezesha kuingia kwa ufanisi zaidi na kushindana katika masoko ya kimataifa.
“Natoa wito kwa wafanyabiashara ambao bado hawajaingia na wale wanaoendelea kutumia nembo za barcodes za mataifa mengine kuacha kufanya hivyo kwa vile taifa lina nembo yake,”alisema.
Aliitaka GSI (TZ) National Ltd kutumia mpango mkakati wake wa miaka mitano kujitangaza kwa nguvu zote ili wajasiriamali na wafanyabiashara wote waweze kuingia katika mfumo huo wa kimataifa kwa vile una faida kubwa kwao.
“Ni jambo la kujivunia kuwa wazalishaji 370 wameingia katika mfumo wa kuwa na barcodes na jumla ya bidhaa 6,000 zilizopo sokoni nazo zina alama hii hadi sasa,”alisema Bw. Pinda.
Alifafanua kwamba serikali ya awamu ya nne ilifanya juhudi kubwa kupata alama hiyo ya utambulisho ili kama moja ya juhudi za kuimarisha sekta binafsi na wajasiriamali hapa nchini.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Bi. Esther Mkwizu alisema Tanzania imefanikiwa kufika hapo kutokana na juhudi za pamoja kati ya serikali na sekta binafsi na sasa bidhaa za Tanzania zina utambulisho.
“Ili kuleta mafanikio zaidi ya mfumo huu, serikali inahitajika kuweka sera bora ya kuuendeleza na isaidie wafabiashara wote kujiunga na mfumo huo ili kuchochea uzalishaji katika sekta za viwanda na kilimo,” alisema.
Alisisitiza kuwa wale walio na alama hiyo tayari wanahitajika kuwa mabalozi wazuri katika matumizi yake ili kuhamasisha wale ambao hawajaingia katika mfumo huo
Makamu Mwenyekiti wa GSI (TZ) National Ltd, Bw. Yakub Hasham alisema Tanzania imefanya mapinduzi makubwa ya kuwa na alama yake ambayo itasaidia kuzitambulisha bidhaa zahapa nchini katika masoko mbalimbali.
Mwisho

No comments: