Na Mwandishi Wetu, Dodoma
Serikali imeanza mchakato wa kumiliki
Kampuni ya Mawasiliano Tanzania (TTCL) kwa asilimia 100 ikiwa ni
njia mojawapo ya kufanya mageuzi ya kibiashara na kuliendesha shirika hilo
kisayansi zaidi ya ilivyo sasa.
Naibu Waziri wa Mawasiliano, Sayansi
na Teknolojia Mh. Januari Makamba aliyasema hayo mkoani Dodoma mwanzoni mwa
wiki hii wakati akielezea mikakati mbalimbali inayotaka kuchukuliwa na serikali
ili kuweza kulimiliki shirika hilo kwa asilimia 100 badala ya 65 za sasa.
Kwa sasa TTCL inamilikiwa kwa ubia,
serikali ikiwa na asilimia 65 wakati 35 zinamilikiwa na kampuni ya simu za
mikononi ya Airtel.
“Mazungumzo tayari yameshaanza na
dhamira yetu ni kununua aslimia 35 ya hisa zinazomilikiwa na wenzetu ili
serikali iweze kumiliki asilimia 100,” alisema Mh. Makamba.
Alisema katika kufanya mipango ya
kwenda mbele kimaendeleo kupitia shirika hili ni lazima kufanya mchakato wa
kulimiliki kwa asilimia 100 ili serikali iweze kufanya mageuzi kwa utashi wake
kadiri inavyofaa.
Alifafanua kwamba hatua hii ni
Kutokana na changamoto zilizopo za kimuundo, kiungozi na ndio maana serikali
imechukua hatua za kinidhamu miongoni mwa baadhi ya watendaji waliobainika
kutumia madaraka yao vibaya ikiwa ni pamoja na kufanya ubadhirifu na hivyo
kulisababishia shirika hasara.
“Hii ni moja ya hatua muhimu katika
kuelekea kufanya mageuzi katika shirika hili kongwe hapa nchini,” alisema.
Alizitaja changamoto nyingine kuwa ni
matatizo ya mtaji, na kusema kuwa ni lazima yashughulikiwe ikiwa ni pamoja na
kwenda na teknolojia mpya na kulifanya shirika lijiwekeze kibiashara zaidi ya
ilivyo sasa.
“Naamini katika kufanya mageuzi
makubwa bodi itachukua nafasi yake kwa maana ya uongozi wa shirika katika
kurekebisha mambo na mapungufu yaliyopo, kwa maana ya kuweka uongozi mpya
utakaoleta mabadiliko ili kulibadilisha liwe shirika kubwa la kisasa
linalotengeneza faida,” alisisitiza.
Alisema kutokana na historia yake
huko nyuma kampuni hii ilipaswa kuwa ndio kampuni inayoongoza kimapato na pia
kwa kutoa huduma nchi nzima kutokana na kuwa ipo kila wilaya katika nchi,
lakini kutokana na changamoto mbalimbali imekuwa ni tofauti na matarajio
yaliyowekwa wakati huo.
Alisisitiza kuwa wakati sasa umefika
kwa shirika kuwa katika mtazamo wa kuwekeza kibiashara zaidi na ushindani.
“Shirika hili kongwe limeendelea
kubaki kama lilivyo na serikali imeliona hilo, kinachohitajika ni kuwekeza
katika rasilimali fedha na watu ili kukabiliana na ushindani wa kibiashara
uliopo sasa,” aliongeza.
Alisema
mbali na changamoto zote hizo lakini TTCL imefanikiwa kuunganisha Ofisi za
Serikali, mashirika mbalimbali, Taasisi za kifedha, utangazaji na Taasisi za
elimu na hivyo kuboresha matumizi ya huduma za mtandao wa mawasiliano kupitia
Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano katika utoaji wa huduma mbalimbali kwa wananchi.
“Kwa
mfano huduma za video conferencing zinawezesha kuendesha mafunzo au mikutano
kwa wahusika na hivyo kuongeza ushiriki, na kupunguza gharama,” alisema.
Akisikiliza kero za wafanyakazi wa
kampuni hiyo hivi karibuni, waziri Makamba aliiagiza bodi ya Wakurugenzi ya
TTCL kumtumia Mkaguzi Mkuu wa Serikali (CAG) kufanya ukaguzi wa mahesabu ili
kuthibitisha tuhuma za ubadhirifu wa fedha za kampuni hiyo ili hatua za
kisheria wakibainika.
Baadhi ya malalamiko yaliyotolewa na
wafanyakazi hao ni pamoja na uongozi na bodi dhaifu katika ufuatiliaji mambo,
ubadhirifu wa fedha za kampuni pamoja na uhamisho wa wafanyakazi usofuata
taratibu.
Mwisho
No comments:
Post a Comment