Thursday, February 19, 2015

Serikali yashauriwa kutoongeza ushuru wa vinywaji

 Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Bw. Evans Mlelwa akisisitiza jambo jana kwa maafisa wa polisi (hawako pichani) waliofanya ziara kwenye kiwanda hicho jana jijini Dar es Salaam.  Kushoto ni Naibu Kamishna wa Polisi, Bohari Kuu (DCP) Adrian Magayane aliyeongoza ujumbe huo.
Naibu Kamishna wa Polisi, Bohari Kuu (DCP) Adrian Magayane (wa tatu kushoto) akisikiliza maelezo ya Meneja Mkuu wa Upikaji Pombe wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL),Bw. Donan Ritte (kushoto) wakati wa ziara ya maafisa wa polisi katika kiwanda hicho jana jijini Dar es Salaam kujionea shughuli za kiwanda hicho.  Wa kwanza kulia ni Inspeta Msaidizi wa polisi, Simpohanus Chacha na wa pili kutoka kulia ni Inspeta, Milliton Masanja.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imeshauriwa kutoongeza tena ushuru wa bidhaa za pombe aina ya bia na vinywaji vikali tena ili kuwezesha viwanda kukua na kuweza kutumia zaidi malighafi za ndani katika uzalishaji.

Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Bw. Evans Mlelwa amesema ongezeko la kila mara la ushuru wa bidhaa hizo unazuia ukuaji wa viwanda na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya uchumi.

Bw. Mlelwa alikua akiongea katika kiwanda cha kampuni hiyo baada ya ziara ya ujirani mwema ya kikundi cha maafisa wa polisi kutoka katika bwalo la polisi barabara ya Kilwa.

Ugeni huo wa polisi uliongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi wa Bohari Kuu (DCP) Adrian Magayane.

Akielezea zaidi, Bw. Mlelwa alisema ongezeko la kila mara la kodi hiyo kila inaposomwa bajeti ya nchi husababisha ongezeko la bei kwa walaji.

“Mara baada ya ongezeko la kodi tu, wazalishaji nao huongeza bei ya bidhaa zao na hali hii huleta athari kwa upande wa mauzo,” alisema.


Alifafanua kuwa kutokana na kushuka kwa mauzo kunakosababishwa na kuongezeka kwa gharama, viwanda kama SBL vinapata changamoto kufikia malengo yake ya kutumia malighafi za ndani na hivyo kuleta athari kwa wakulima ambao wangefaidika kwa kuuza mazao yao.

No comments: