Thursday, February 19, 2015

TNBC yahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limewataka wafanyabiashara mkoani Dodoma kutumia fursa ya wafadhili wa Denmark wenye lengo la kuboresha na kutengeneza mazingira rafiki ya ufanyaji biashara ili wapate manufaa zaidi katika kuendeleza biashara zao.

Katibu Mtendaji wa TNBC, Bw. Raymond Mbilinyi alisema baraza limeingia mkataba na ‘Local Investment Climate Reform’ (LIC)  toka Denmark lenye lengo la kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara nchini.

“LIC ni mradi wenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na imeanza na mikoa miwili ya Dodoma na Kigoma hivyo wananchi watumie fursa hii kushirikiana nao ili wawezeshwe katika biashara zao,” alisema Bw. Mbilinyi.

Alisema lengo kuu la LIC ni kutengeneza mahusiano mazuri kati ya sekta za umma na sekta binafsi katika ufanyaji biashara kwani hili ni tatizo kubwa walilobaini katika tafiti zao za awali.

Katibu Mtendaji huyo, amewataka wadau wote kushirikiana na wafadhili hawa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili mikoa yetu ipige hatua katika maendeleo.

No comments: