Afisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha
Tanzania (FSDT), Bw. Sosthenes Kewe akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari
jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongelea awamu ya tatu ya shindano la
mfuko wa ubunifu wa bidhaa za kifedha unaolenga kusaidia wajasiriamali. Wengine ni washindi waliopita wa shindano
hilo; Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Go Finance Limited, Bw. Geoffrey Ndosi
(kushoto) na Mkurugenzi Mkuu Mtendaji wa Problem Solved Limited, Bw. Eric
Mutta.
Na Mwandishi
wetu, Dar es Salaam
Wadau wa sekta
ya fedha na wabunifu nchini wametakiwa kuchangamkia awamu ya tatu ya shindano
la mfuko wa ubunifu wa bidhaa za kifedha unaolenga kusaidia wajasiriamali
wadogo na wa kati.
Shindano hilo
linaendeshwa na Mfuko wa Kuendeleza Sekta ya Fedha Tanzania (FSDT) ambao
ulianzishwa mwaka 2004 kuchochea ukuaji wa sekta ya fedha Tanzania hasa
kuwezesha watu wengi zaidi na biashara kuweza kufikia huduma za kifedha.
Akiongea na
waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Afisa Mtendaji Mkuu wa FSDT, Bw.
Sosthenes Kewe alisema shindano hilo lililofunguliwa mwanzoni mwa mwezi Desemba
mwaka jana linalenga kuvutia mawazo ya aina ya miradi na ubunifu utakaosaidia
kuja na bidhaa na huduma mpya kusaidia wajasiriamali hapa nchini.
“Hakuna
mabadiliko yanayoweza kutokea kama mambo yatafanyika vile vile katika mazingira
yanayobadilika kwa kasi,” alisema.
Alisema huu ni
wakati wa kwa wadau wa sekta ya fedha na wabunifu kuja na mambo mapya ambayo
yatasaidia kuendeleza sekta ya wajasiriamali hapa nchini.
Alisema ingawa
umuhimu wa sekta ya wajasiriamali katika kujenga uchumi, kukuza ajira na
kuondoa umaskini unajulikana; bado sekta hiyo ina changamoto kubwa kufikia
huduma za kifedha.
“Pamoja na
umuhimu wao, bado changamoto ya huduma za fedha kwa wajasiriamali hapa nchini
ni kubwa sana,” alisema Bw. Kewe.
Kwa mara ya
kwanza shindano hilo lilianza mwezi Juni 2011 ambapo katika awamu hiyo kampuni
19 ziliomba; wakati kampuni 13 zilijitokeza katika awamu ya pili ya shindano
hilo.
Mshindi wa
kwanza, Go Finance Limited, alishinda ruzuku ya dola za kimarekani 153,000
Januari 2012 na ametengeneza mfumo wa kiteknolojia ambao umerahisisha kutoa
mikopo kwa wajasiriamali bila kukumbana na masharti magumu katika uendeshaji wa
biashara zao.
Afisa Mkuu
Mtendaji wa Go Finance Limited, Bw. Geoffrey Ndosi alisema ruzuku hiyo
imesaidia kampuni yao kukua kibiashara, kuongeza ajira pamoja na kusaidia
wajasiriamali.
“Ninawahamasisha
wadau wa sekta hii kuchangamkia fursa ya shindano hili ili waweze kuleta
mabadiliko yanayotakiwa,” alisema.
Mshindi
mwingine wa awamu ya pili ya shindano hilo ambaye ni kampuni ya Problem Solved
Limited, alijishindia ruzuku ya dola za kimarekani laki 328 (Tshs 525 milioni)
baada ya kuelezea jinsi anavyoweza kutengeneza mfumo wa kompyuta utakaosaidia
wajasiriamali kutunza kumbukumbu za hesabu zao za biashara kwa urahisi.
Afisa Mtendaji
Mkuu wa Problem Solved Limited, Bw. Eric Mutta alisema ruzuku aliyopata
itasaidia kuleta tofauti kubwa kwa wajasiriamali hapa nchini na hivyo
kuendeleza uchumi wa nchi.
Ruzuku hiyo ya
FSDT inatolewa baada ya kushindanisha watu waliyoomba kuanzia dola 100,000 na
dola 500,000 kulingana na aina ya mradi. FSDT hutoa asilimia 50 ya
fedha zilizoombwa kusaidia gharama za kuanzisha bidhaa au huduma zikilenga
kuinua wajasiriamali.
Mwisho