Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
Waziri Mkuu Mizengo Pinda ametoa
Changamoto kwa taasisi mbalimbali hasa za serikali nchini kuwaamini na
kuwatumia watafiti wa ndani badala ya kukimbilia kutumia wale wa nje ambao
amesema mara nyingi huwa na gharama kubwa.
Waziri Mkuu alisema hayo wakati alipokuwa
akizindua rasmi Chuo Kikuu Mzumbe, Kampasi ya Dar es Salaam na pamoja na jengo
la ghorofa tano la kampasi hiyo juzi jioni jijini Dar es Salaam.
Akizungumza katika hafla hiyo baada ya
uzinduzi huo, Bw. Pinda alisema kuna tabia imejengeka kwa taasisi na idara za
serikali kukimbilia watafiti wa nje pale mahitaji yanapojitokeza na kuwaacha wa
ndani.
“Huu mtindo haufai...watafiti wetu wa
ndani wana uwezo na wanajua mazingira ya nchi yetu vizuri...tuwasadie kwa
kuwapa kazi,” alisema, na kuongeza kuwa serikali inaamini kuwa watafiti hao
wanaweza kufanya kazi kwa viwango vinavyokubalika kitaifa na kimataifa.
Alisema watafiti hao wakitumika vizuri
watakuwana uwezo wa kutoa majibu yanayolingana na mazingira ya nchi na hivyo
kupata suluhisho la changamoto mbalimbali za maendeleo.
Akitoa mfano wa Mzumbe alisema chuo hicho
kilichodumu kwa takriban miaka 60 sasa kimetoa mchango mkubwa wa wataalam na
kujijengea uwezo katika nyanja mbalimbali ambao unaweza kuwa faida kwa nchi
kuliko ilivyo sasa kama kitatumiwa vizuri.
“Tumieni uwezo wa chuo hiki katika tafiti
zenu,” Bw. Pinda aliwaambia baadhi ya maafisa waandamizi wa serikali
walioandamana nae katika hafla hiyo.
Alisisitiza kuwa katika maswala ambayo
vyuo kama hicho vina uwezo nayo hakuna sababu ya kutafuta wataalamu kutoka nje
ya nchi.
“Tabia ya kuchua watalaamu kutoka nje ya
nchi kwa maswala ambayo wataalamu wetu wana uwezo nayo haiingii akilini,”
alisema Pinda.
Aidha alitoa ushauri kwa chuo
hicho kuanzisha kozi fupi amabazo zitasaidia kutoa elimu kwa viongozi wakiwemo
mawaziri, wabunge, makatibu wakuu, wakuu wa mikoa, wilaya na wengine kupata
weledi wa uongozi.
“Kuna matatizo mengi yanajitokeza hivi
sasa na ukiyaangalia unakuta kuwa baadhi ya mambo yanahitaji tu weledi wa mbinu
kidogo za uongozi,” alisema Bw. Pinda.
Alisema Chuo hicho kilipoanzishwa wakati
wa ukoloni na baada ya uhuru kilikuwa kinatayarisha watu kuwa viongozi na
kwamba pamoja na kuwa sasa masomo hayo yanatolewa katika programu za masomo ya
chuo hicho, bado ipo haja ya kuanzisha kozi hizo fupi kwa ajili ya viongozi
ambao hawakupata mafunzo hayo.
Alisifu uongozi wa chuo hicho kwa kupanua
wigo wa elimu kwa watanzania kwa kuanzisha kampasi za Mbeya na Dar es Salaam na
pia kwa kupanua miundombuni na udahili wa wanafunzi.
Alisema uamuzi wa chuo hicho kutaka kuanza
kutoa mafunzo katika ngazi ya uzamili kuwezesha wahitimu kusimamia miradi
mikubwa katika sekta za madini, gesi na mafuta ni mzuri na wenye manufaa kwa
nchi.
“Kinachotakiwa sasa ni kwa chuo hiki
kujenga mahusiano na nchi zenye uzoefu katika sekta hizi ili mjue zaidi undani
wake na mboreshe kozi mtakazotoa,” alisema.
Alisema pamoja na kwamba uwiano wa
wanawake na wanaume katika udahili wa wanafunzi si mbaya, bado juhudi
zinatakiwa katika kuongeza idadi ya wanawake.
Naye Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu Mzumbe,
Profesa Joseph Kuzilwa alisema chuo chake kimejenga jingo hilo kutokana na
mahitaji makubwa ya watu wanaotaka kusoma katika kampasi ya Dar es
Salaam.
“Jengo hili litasaidia kuboresha huduma
zetu kwa wanafunzi na pia kurahisisha kazi ya waalimu wetu,” alisema, na
kuongeza kuwa sasa chuo kitaokoa zaidi ya shilingi milioni 300 kwa mwaka
zilizokuwa zikitumika katika kukodisha kumbi za mihadhara.
Jengo hilo lina maktaba ya kisasa
iliyochukua ghorofa mbili za jengo, ofisi ya Makamu Mkuu wa Chuo pamoja na ya Mkuu
wa Kampasi, kumbi tatu za mihadhara zenye uwezo wa kuchukua wanafunzi 132 kila
mmoja pamoja na ukumbi wa mikutano.
Alisema chuo kina mipango ya kuongeza
ujenzi wa miundombinu na rasilimali watu ili kuzidi kupanua wigo wa elimu kwa
watanzania katika sehemu mbalimbali nchini katika juhudi za kuunga mkono nia ya
serikali ya kupanua fursa za elimu kwa wananchi.
Kampasi ya Dar es Salaam ilianzishwa mwaka
2005 ikiwa na wanachuo 146 na programu mbili za uzamili.
Katika mwaka wa masomo wa 2013/2014,
kampasi hiyo ilidahili wanafunzi 1052 ambao kati yao 504 ni wanawake na 548 ni
wanaume wanaosoma shahada za uzamili katika programu zaidi ya 10.
Kukua kwa kampasi hiyo kumechangia kwa
kiasi kikubwa kukua kwa Chuo Kikuu Mzumbe ambayo idadi yake kwa sasa ni zaidi
ya wanachuo 8,000.
Mwisho.