Monday, December 10, 2012

Wahitimu Mzumbe watakiwa kutumia elimu yao kwa manufaa ya nchi




Mkuu  wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstafu Barnabas Samatta akiongoza maandamano ya chuo kuashiria kufungua maahafali ya 11 ya Chuo hicho akiwana Makamu Mkuu wa Chuo hicho,Profesa Joseph Kulizwa na Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho Profesa Daniel Mkude.
Mzumbe University Chancellor, Rt. Judge Barnabas Samatta (center) during the varsity’s 11 graduation ceremony in Morogoro this Friday.  Others in the picture are the varsity’s Vice Chancellor, Prof. Joseph Kuzilwa (left) and the Chairman of Mzumbe University Council, Prof. Daniel Mkude.  



Mkuu  wa Chuo Kikuu Mzumbe, Jaji Mstafu Barnabas Samatta akimtunuku shahada ya uzamivu (PhD),Balozi wa Tanzania Nchini Ubelgiji, Diodorus Kamala katika Mahafali ya 11 ya Chuo Kikuu Mzumbe Kampasi Kuu Morogoro Ijumaa.
Mzumbe University Chancellor, Rt. Judge Barnabas Samatta conferring a Doctorate Degree (Phd) to the Tanzania Ambassador to Belgium, Amb. Diodorus Kamala during a 11 graduation ceremony held at the varsity’s main campus in Morogoro this Friday.


Na Mwandishi wetu, Morogoro
Chuo kikuu Mzumbe kimewaasa wahitimu wake kuitumia vizuri taaluma waliyoipata chuoni hapo kusaidia kusukuma gurudumu la maendeleo ya taifa na jamii zao.
Ushauri huo umetolewa wakati wa sherehe za mahafali ya 11 ya chuo hicho mjini Morogoro mwishoni mwa wiki ambapo wahitimu mbalimbali walitunukiwa astashahada, stashahada,shahada ya kwanza, shahada ya uzamili na uzamivu na Mkuu wa Chuo hicho, Jaji Mstafu, Barnabas Samatta.
Makamu Mkuu wa Chuo hicho, Profesa Joseph Kuzilwa alisema wahitimu hao hawanabudi kuzitumia taaluma zao na kuwa kioo cha shughuli za maendeleo sehemu za kazi na katika jamii.
“Tunawataka mkayatumie maarifa mliyoyapata hapa kupitia masomo yenu mliyofuzu kwa kuajiriwa, na kujiajiri kwa lengo la kulisaidia taifa kimaendeleo,” alisema.
Aliwasifu wahitimu hao kwa kufanya vizuri katika masomo yao na hivyo kustahili kutunukiwa vyeti hivyo na kuongeza kusema wanawake wamefanya vizuri zaidi.
Hata hivyo, alieleza kuwa chuo kinakabiliwa na uchakavu na upungufu wa miundombinu ya madarasa,hostel za wanafunzi,ofisi za wahadhiri na hivyo kusababisha kuendesha shughulizake katika mazingira magumu.
Aliomba serikali na wadau mbalimbali kuzidi kuongeza misaada kwa chuo kwa lengo la kutimiza mahitaji hayo ili kukidhi ongezeko la udahili wa wanafunzi na kuongeza programu za masomo.
Chuo kimeendelea kuajiri wanataaluma wapya na kupelekea kuwa na wahadhiri 150 mwaka 2002 hadi kufikia 304 mwaka huu.
Mwenyekiti wa Baraza la Chuo hicho, Profesa Daniel Mkude alisema chuo hicho kimeendelea kutoa elimu za taaluma mbalimbali ikiwemo ya elimu ili kupunguza tatizo la uhaba wa walimu shule za sekondari na vyuo vya ualimu nchini.
Aliwataka wahitimu hao kuthamini maisha yao kwa kujihadhari na janga la ukimwi na madawa ya kulevya ili taifa lisipoteze nguvu kazi.
Aliongeza kusema kuwa wahitimu hao wanatakiwa kuwa mabalozi wa kukomesha vitendo viovu kama wizi, unyang’anyi,mauaji ya vikongwe,maalbino,ubakaji, ukahaba, kukomesha rushwa na mimba za utotoni.
Naye Balozi wa Tanzania nchini Ubelgiji, Bw. Diodorus Kamala ambaye alitunukiwa shahada ya uzamivu na chuo hicho aliwaasa vijana kuwa elimu ndiyo njia pekee ya kufikia malengo yao kimaisha na kulisaidia taifa kimaendeleo.
Alisema yeye pamoja na majukumu aliyonayo kitaifa na ya kwake binafsi ameweza kupanga muda na kuendelea na masomo na kufuzu.
Chuo Kikuu Mzumbe kina kampasi tatu ikiwemo Kampasi Kuu ya Morogoro, Dares Salaam na Mbeya. Pia ina vituo katika mikoa ya Mwanza na Tanga.
Katika mahafali ya mwaka huu, Kampasi Kuu ya Mzumbe Morogoro ilitoa wahitimu 716, Kampasi ya Mbeya 314 na Kampasi ya Dar es Salaam itakua na wahitimu 1,019.
Kati ya wahitimu hao, wahitimu 291 wlitunukiwa vyeti, 94 diploma, 1,143 shahada ya kwanza, 1515 shahada ya uzamili na wawili shahada ya uzamivu.
Balozi Kamala alikua ni miongoni mwa waliotunukiwa shahada ya uzamivu baada ya kufanya utafiti wa masuala ya ushirikiano wa biashara Afrika Mashariki.
Wihitimu wanaume walikuwa 1,170 na wanawake 1,279.
Mwisho. 

No comments: