Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Imeelezwa kwamba kuna umuhimu wa Tanzania na nchi nyingine za Afrika
kufanya jitihada za kuongeza thamani mazao ya kilimo kama zinataka kufikia
maendeleo endelevu ya kudumu.
Haya yamesemwa na muwakilishi wa shirika la Umoja wa Mataifa
linaloshughulikia Maendeleo ya Viwanda (UNIDO) hapa nchini wakati wa uzinduzi
wa kitabu kinachohusu kilimo kwa ajili ya biashara kwa maendeleo ya Afrika
jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa wiki hii.
Kuna umuhimu wa kuangalia jinsi nchi za Afrika zinavyoweza kuongeza
thamani,” alisema na kuongeza kwamba nchi hizo zinatakiwa kuwa na uwezo wa
kuongeza nusu ya thamani inayoongezwa na nchi zilizoendelea kama kweli zinataka
kuondokana na umaskini.
Kwa mujibu wa kitabu hicho, nchi zilizoendelea huongeza thamani ya
hadi dola 180 kwa tani moja ya mazao wakati nchi zinazoendelea hutumia dola za
Marekani 40 tu kuongeza thamani ya tani moja ya mazao.
Pia, wakati asilimia 98 ya mazao ya kilimo huongezwa thamani katika
nchi zilizoendelea, ni asilimia 30 tu ya mazao ya kilimo huongezwa thamani
katika nchi zinazoendelea.
“Takwimu hizi zinawezakuwa za kukatisha tama zaidi kama tukiangalia
nchi moja moja katika bara la Afrika,” alisema Kalenzi.
Kitabu hicho kilichoandikwa kwa msaada wa UNIDO na kupata mchango wa
Mkurugenzi Mkuu wa shirika hilo kinaangalia jinsi ya kukifanya kilimo kuwa cha
kibiashara zaidi na kuwa chachu ya kufikia maendeleo endelevu Afrika.
Bw. Kalenzi aliisifu Tanzania kwa juhudi inazochukua kuhakikisha
kilimo kinakua na kuwa moja ya mkakati wa kufikia lengo la nchi kuwa taifa
lenye uchumi wa kati ifikapo mwaka 2025.
Hata hivyo alisema ingawa kilimo bado ni mchangiaji mkubwa wa
maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa Tanzania na bara zima la Afrika, bado
hakitafanikiwa kuleta mapinduzi makubwa ya maendeleo kama hapatafanyika mageuzi
makubwa katika sekta hiyo.
“Pamoja na kwamba kilimo kinachangia kwa kiwango kikubwa mapato katika
bara la Afrika, bado kinatumia zana dhaifu,” alisema, na kuongeza kwamba bado
wakulima wengi wanatumia zana zilezile zilizotumiwa na mababu miaka mingi
iliyopita.
Waziri wa Viwanda na Biashara, Abdallah Kigoda alikubaliana
kwamba bila viwanda na kuongeza thamani ya mazao, Afrika haitafikia maendeleo
yanayotazamiwa.
Alisema bara la Afrika sasa halina budi kuachana na kilimo
cha jembe la mkono na kuangalia jinsi ya kufanya kilimo cha kibiashara na
kuvutia uwekezaji katika sekta hiyo.
“Ni lazima Tanzania tuweze kutofautisha kilimo cha kizamani
cha kutumia jembe la mkono na kile cha kibiashara na kuongeza thamani,”
alisema.
Mwisho
No comments:
Post a Comment