Thursday, December 6, 2012

Ole Naiko atunukiwa tuzo, atoa changamoto kuundwa kada ya kati





Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mduara wa Maafisa Watendaji Wakuu Tanzania (CEO Roundtable of Tanzania) umepewa changamoto kusaidia serikali kujenga kada ya watu wa kati hapa nchini.
Wito huo umetolewa na mtaalamu anayetambulika kimataifa wa masuala ya uwekezaji, Bw. Emmanuel Ole Naiko wakati wa chakula cha jioni kilichoandaliwa na umoja huo kumtunukia tuzo ya utumishi uliotukuka serikalini mwishoni mwa wiki jijini Dar es Salaam.
Bw. Naiko anakuwa mtu wa kwanza kutunukiwa tuzo hiyo toka umoja wa maafisa hao.
“Nawaomba mfanye kila linalowezekana kusaidia serikali kujenga kada ya watu wa kati hapa Tanzania,” alisema Bw. Naiko mbele ya maafisa hao na wageni wengine waalikwa.
Mshindi wa tuzo hiyo alimuomba Mwenyekiti wa mduara huo wa Maafisa Watendaji Wakuu, Bw. Ali Mufuruki kutumia uwezo wake na uzoefu alionao katika biashara kusaidia katika kujenga kada ya watu wa kati kiuchumi.
Bw. Naiko alisema kujenga kada hiyo ni lengo la serikali na kwamba hakuna budi kulitekeleza wazo hilo kwa manufaa ya Tanzania kwa ujumla.
Alisema akiwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) anakumbuka rais Jakaya Kikwete mara tu baada ya kuingia madarakani aliipatia TIC kazi ya kuongoza juhudi za kujenga kada hiyo.
“Lengo letu kipindi hicho lilikua kuwaingiza watanzania wenye uwezo mdogo kiuchumi kwenye mfumo wa uchumi rasmi kwa sababu tumerithi taasisi na mifumo inayowaweka wengi nje ya mfumo wa mafanikio,” alisema.
Alisema juhudi hizo zingewezesha watanzania wengi kushiriki kikamilifu katika mfumo wa kitaifa na kimataifa wa kibiashara na hivyo kuwainua.
“Tulichukua changamoto hiyo ya rais na kwa kuanza tuliunda kundi la wajasiriamali 80…bahati mbaya juhudi hizi zilitekwa na mtu mmoja katika moja ya wizara na tukapoteza kabisa mwelekeo,” alisema.
Bw. Naiko alitoa shukrani zake kwa kuteuliwa kupata tuzo hiyo.
 
“Nashukuru sana kwa mapenzi mliyoonyesha kwangu,” alisema.
 
Mtumishi huyo mstaafu alisema si sawa kuwalaumu viongozi waliopita kwa madai kwamba waliiingiza nchi katika mikataba mibovu hasa katika sekta za madini na mafuta.
 
Akielezea zaidi kuhusu hilo alisema watu hao wanasahau kwamba kabla ya mwaka 1998, Tanzania haikuwa hata na mgodi mmoja binafsi uliokuwa unazalisha dhahabu.
 
“Ni baada ya kipindi hicho tu ambapo Tanzania iliweza kuwa mmoja wa wazalishaji wakubwa wa dhahabu Afrika,” alisema.
 
Kwa upande wa mafuta alisema tafiti nyingi zilizofanywa na kampuni za utafiti wa mafuta sasa zinaiweka Tanzania kuwa moja ya wazalishaji wakubwa wa gesi.
 
“Baadhi ya inayoitwa mikataba mibovu ilisainiwa na watu wenye heshima kubwa sana katika nchi yetu na watu hawa wasingeweza kusaini ‘mikataba mibovu’,” alisema.
 
Alisema viongozi hao walifanya hivyo kutokana na mazingira yaliyokuwepo kipindi hicho na walitakiwa kuchagua kati ya kuacha raslimali hizo ardhini au kuzivuna ili nchi ifaidike.
 
“Kulaumu watu hawa kwa madai ya kuingia mikataba mibovu ni sawa na kucheka wazazi na mababu zetu waliotulea na kutukuza katika nyumba za matope,” alisema.
 
Alisema njia Tanzania iliyopitia ni njia inayopitiwa na nchi zote zinazovutia wawekezaji.  Alitoa mfano wa nchi kama Mauritius ambayo leo inatolewa mfano wa mafanikio Afrika kwamba ilipitia njia kama inayopitia nchi hii lakini hakuna mtu anaelaumu viongozi wa nchi hiyo.
 
“Walianza kwa kutegemea miwa kama msingi wa uchumi lakini leo wanategemea teknolojia ya habari na mawasiliano,” alisema.
 
Kwa upande wake, Bw. Mufuruki alisema uamuzi wa kumtunukia Bw. Ole Naiko ulifikiwa na kamati ya uteuzi baada ya kuangalia rekodi yake katika kuendeleza sekta binafsi kwa muda mrefu alipokua mtumishi wa umma.
 
“Tunamshukuru sana hasa kwa vile alisaidia  kwa sera nyingi za kuvutia uwekezaji wa ndani na nje kupitishwa na serikali,” alisema.
Mwisho.


No comments: