Monday, December 31, 2012

Bank of Afrika Group kujitanua Afrika Mashariki



Bank of Africa Tanzania Managing Director, Mr. Ammish Owusu-Amoah (standing) addresses Bank of Africa Group Board of Directors meeting that ended in Arusha over the weekend.
Mkurugenzi Mtendaji wa Bank of Africa Tanzania, Bw. Ammish Owusu-Amoah alipokua akihutubia mkutano uliohusisha wakurugenzi wa mtandao wa benki hiyo barani Afrika uliomalizika jijini Arusha mwishoni mwa wiki.



The President, Bank of Africa Group, Mr. Mohamed Bennani addresses Bank of Africa Group Board of Directors meeting that ended in Arusha over the weekend.
Rais wa Bank of Africa Group, Bw. Mohamed Bennani akihutubia mkutano uliohusisha wakurugenzi wa mtandao wa benki hiyo barani Afrika uliomalizika jijini Arusha mwishoni mwa wiki.


Na Mwandishi wetu, Arusha
Mtandao wa mabenki barani Afrika unaojulikana kama Bank of Afrika Group unatarajia kujitanua zaidi katika eneo la Afrika ya Mashariki kuanzia mwakani.
Hayo yamesemwa na Mkurugenzi Mtendaji wa tawi la benki hiyo hapa nchini, Bank of Africa Tanzania, Bw. Ammish Owusu-Amoah alipokua akiongea na waandishi wa habari wakati wa mkutano uliohusisha wakurugenzi wa mtandao wa benki hizo barani Afrika uliomalizika jijini Arusha mwishoni mwa wiki.
“Kwa sasa benki hii inaangalia jinsi ya kujitanua katika ukanda huu ili kuwa pia na matawi katika nchi zilizobaki katika Afrika ya Mashariki,” alisema.
Kwa sasa, katika ukanda huu, benki hiyo kubwa iko katika nchi za Tanzania, Uganda, Kenya na Burundi.
Alipoulizwa ni lini mpango huo utakamilika, alisema: “Kwa vyovyote vile kabla ya mwisho wa mwaka ujao tutakua tumeshaanza kufanya kazi katika nchi zilizobaki.”
Bw. Ammish alisema uamuzi wa kuchagua kufanyia mkutano huo mkubwa Tanzania katika jiji la Arusha ulifikiwa ili kuimarisha uhusiano uliopo kati ya kundi hilo la mabenki na jumuiya ya Afrika ya Mashariki.
“Tulichagua Arusha kuonyesha umuhimu wa eneo hili la Afrika katika ukuaji wa benki yetu,” alisema.
Alielezea kwamba benki hiyo itaendelea kuangalia fursa zilizopo katika ukanda huu pamoja na kusaidia biashara ndogo na za kati kwa masharti nafuu pamoja na kujihusisha zaidi na kutoa michango mbalimbali kwa jamii.
Alisema ni mategemeo ya benki hiyo kujiimarisha zaidi katika Tanzania na kwamba mikakati iliyotokana na mkutano huo itasaidia kufikiwa kwa lengo.
Bw. Ammish alitoa pongezi kwa serikali ya Tanzania kwa ukarimu ulioonyeshwa kwa wajumbe wa mkutano huo na huduma nzuri walizopatiwa.
“Kama nchi, tukiendelea hivi, tutasaidia sana kuvutia mikutano mikubwa na biashara hapa Tanzania…tuendelee na moyo huo,” alisema.
Hii ilikua ni mara ya pili kwa mkutano kama huu kufanyika hapa nchini ambapo kundi hilo pia linafanya kazi kupitia benki yake—Benki ya Afrika Tanzania.
Mkutano wa kwanza uliohusisha wakurugenzi wa benki hiyo kutoka nchi zinazozungumza kiingereza ulifanyika mkoani Dar es Salaam mwezi Machi mwaka huu.
Benki hii inafanya kazi katika nchi 15 zikiwemo Benin, Burkina Faso, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Djibouti, Ghana, Ufaransa, Ivory Coast, Kenya, Madagascar, Mali, Niger, Senegal, Tanzania na Uganda ambapo huzunguka katika kila nchi kwa ajili ya mikutano kama hii.
Mwanahisa mkubwa wa kundi hili ni BMCE Bank ambayo ni benki ya pili binafsi kubwa nchini Morocco.
Tangu ianze shughuli zake hapa nchini mwaka 2007, benki hii imekua ikijitahidi kujitanua kwa kuanzisha huduma mbalimbali ikiwa ni pamoja na kufungua matawi mapya. 
Hadi sasa ina matawi kumi jijini Dar es Salaam pamoja na mengine saba katika mikoa ya Morogoro, Tunduma, Mwanza, Moshi, Mbeya,Mtibwa na Arusha.
Mwisho 



No comments: