Thursday, February 19, 2015

TNBC yahamasisha wafanyabiashara kuchangamkia fursa zilizopo



Na Mwandishi Wetu, Dodoma

Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) limewataka wafanyabiashara mkoani Dodoma kutumia fursa ya wafadhili wa Denmark wenye lengo la kuboresha na kutengeneza mazingira rafiki ya ufanyaji biashara ili wapate manufaa zaidi katika kuendeleza biashara zao.

Katibu Mtendaji wa TNBC, Bw. Raymond Mbilinyi alisema baraza limeingia mkataba na ‘Local Investment Climate Reform’ (LIC)  toka Denmark lenye lengo la kutengeneza mazingira wezeshi ya biashara nchini.

“LIC ni mradi wenye lengo la kuboresha mazingira ya biashara na imeanza na mikoa miwili ya Dodoma na Kigoma hivyo wananchi watumie fursa hii kushirikiana nao ili wawezeshwe katika biashara zao,” alisema Bw. Mbilinyi.

Alisema lengo kuu la LIC ni kutengeneza mahusiano mazuri kati ya sekta za umma na sekta binafsi katika ufanyaji biashara kwani hili ni tatizo kubwa walilobaini katika tafiti zao za awali.

Katibu Mtendaji huyo, amewataka wadau wote kushirikiana na wafadhili hawa katika kuboresha mazingira ya biashara na uwekezaji ili mikoa yetu ipige hatua katika maendeleo.

Monday, February 9, 2015

Bendera atoa somo Baraza la Biashara la Manyara



Na Mwandishi wetu, Manyara
Majadiliano ya mara kwa mara ya Baraza la Biashara Mkoa wa Manyara yametajwa kuwa moja ya njia zinazoweza kuibua fursa za biashara na uwekezaji na kuchochea ajira na ukuaji wa uchumi mkoani humo.

Mwenyekiti wa Baraza la Biashara la Mkoa huo, Bw. Joel Bendera ambaye pia ni Mkuu wa Mkoa huo alisema hayo katika mkutano wa tano wa baraza hilo kuwa mikutano hiyo ina nafasi kubwa ya kuibua fursa za biashara.

“Mabaraza haya yamesheheni wajumbe kutoka sekta ya umma na binafsi...yanapokutana yanaibua fursa za biashara na kujenga mtandao miongoni mwao,”alisema.

Mabaraza ya biashara ya mikoa yanafanya kazi chini ya Baraza la Taifa la Biashara (TNBC) na yanaundwa na wajumbe wa sekta ya umma na binafsi katika kuleta majadiliano na kuibua fursa za biashara.

Alisema mkoa huo una fursa nyingi za kibiashara ikiwemo ya Kilimo na madini hivyo wajumbe wana wajibu wa kuzidi kuibua fursa zaidi na kuzitangaza watu wawekeze.

Wednesday, February 4, 2015

Prof Galabawa asisitiza ushirikiano wa wanafunzi na walimu kukuza elimu



 
Mwanzilishi wa Shule ya Sekondari Thomas More Machrina, Profesa Justinian Galabawa akisisitiza jambo jana jijini Dar es Salaam kuhusu baadhi ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuinua kiwango cha ufaulu wa wanafunzi hapa nchini.



Mwanafunzi wa kidato cha kwanza Shule ya Sekondari Thomas More Machrina,Emmanuel Rweyendela akisikiliza kwa makini maelekezo ya mwalimu wa somo la kiingereza katika shule hiyo,Bi.Kulthum Asiimwe jana jijini Dar es Salaam.

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Ushirikiano wa karibu kati ya walimu na wanafunzi na kutumia muda mwingi kufudisha maudhui yaliyomo katika vitabu kulingana na mitaala vimetajwa kama vitu muhimu vitakavyorejesha hadhi ya elimu nchini.

Mwanzilishi wa Shule ya Sekondari Thomas More Machrina, Profesa Justinian Galabawa amesema kuwa mfumo huo ukizingatiwa utaboresha mfumo wa elimu na wanafunzi kufanya vizuri katika masomo yao.

“Tunatakiwa kama taifa turudishe mfumo wa zamani ambao ulilenga maudhui ya masomo na ushirikiano kati ya walimu na wanafunzi,” alisema na kuongeza kusema kuwa muda mwingi utumike katika masomo.

Alisema wasomi wengi wa zamani walifaidika na mfumo huu ambapo walimu walikuwa na ushirikiano mzuri na wanafunzi na muda mwingi ulitumika kufundisha maudhui ya masomo yenyewe.

Shule ya Sekondari ya bweni Thomas More Machrina ambayo ni ya wavulana ilianzishwa 2005 na inatumia mfumo huo wa zamani ambao unaisaidia wanafunzi kufanya vyema katika masomo.

Akiongea jana jijini Dar es Salaam alisema serikali inatakiwa kuiga mbinu zinazotumiwa na shule za binafsi na kutumia mfumo huo ili shule zote za umma ziweze kufanya vizuri.

Wednesday, January 21, 2015

Serikali yapewa changamoto kuchochea ubunifu kwa wanafunzi



Na Mwandishi wetu, Morogoro

Serikali imeshauriwa ipitie upya mitaala yake ya  elimu ili iweze kuendana na ulimwengu wa utandawazi ambao unafanya mwanafunzi kuwa mbunifu zaidi.

Kaimu Mwalimu Mkuu wa Shule ya Awali na Msingi Ndetembia Matemu, Bw. Joshua Kihaka amesema mjini Morogoro hivi karibuni kuwa mitaala ya elimu inatakiwa kuangaliwa upya ili iende sambamba na wakati.

“Wanafunzi wanatakiwa kupata maarifa yatakayowafanya kuwa wabunifu,” alisema.

Alisema pamoja na changamoto hiyo shule ya Ndetembia Matemu inawandaa wanafunzi wakubalike kitaifa na kimataifa kulingana na ulimwengu wa sayansi na teknolojia.

Alifafanua kuwa shule hiyo inayofundisha kwa lugha ya kiingereza pia inafundisha somo la Teknolojia ya Habari na Mawaslianino (TEHAMA) ambalo linawafanya watoto kwenda na wakati.

Alisema changamoto za kielimu zilizopo nchini lazima zitatuliwe na serikali kupitia Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, walimu na wazazi.