Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali ya Tanzania kwa kushirikiana na Idara ya
Forodha na Ulinzi wa Mipaka ya Marekani imezindua programu ya uimarishaji
ulinzi katika bandari ya Dar es Salaam na uwanja wa Ndege wa Kumbukumbu ya
Mwalimu Nyerere kwa kutumia mbwa maalumu kubaini dawa za kulevya na pembe za
ndovu.
Wizara zinazohusika na programu hiyo hapa nchini ni
pamoja na Wizara ya Uchukuzi, Wizara ya Mambo ya Ndani na Wizara ya Maliasili
na Utalii.
Akizungumza katika uzinduzi huo jana jijini Dar es
Salaam, Waziri wa Maliasili na Utalii, Bw. Lazaro Nyalandu alisema programu
hiyo inalenga kuimarisha ulinzi katika maeneo hayo kwa kuanzia ili kupambana na
wasafirishaji wa madawa ya kulevya na pembe za ndovu.
“Tumedhamiria kupambana na wahalifu hawa hadi mwisho,”
alisema.
Chini ya mpango huo, polisi wa Tanzania watapatiwa
mafunzo nchini marekani ya kutumia mbwa maalumu kwa ajili ya kuanza kutumia
mbwa hao maalum katika maeneo hayo ifikkapo mwezi Septemba mwaka huu.
Waziri alisema dhamira ya serikali ni kuwa na ulinzi
wa namna hiyo katika mipaka yote ya nchi kuhakikisha taifa linakuwa salama
kutokana na uharibifu unaofanywa na watu wasio na mapenzi mema na taifa lao.
No comments:
Post a Comment