Thursday, March 13, 2014

Mabasi machache kuanza kutoa huduma kabla ya awamu ya kwaza kuisha -DART

Kaimu Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART Agency), Bi. Asteria Mlambo akisisitiza jambo kwa waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam alipokuwa akiongelea utaratibu utakaotumika kupata watoa huduma wa mradi huo utakapoanza.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wakala wa Mradi wa Mabasi yaendayo aaraka (DART) umesema kabla ya utekelezaji wa awamu ya kwanza ya mradi kukamilika, mwaka huu kutakuwa na mabasi machache ambayo yataanza kutoa huduma ya usafiri kutoka Kimara hadi Kivukoni.

Kaimu Mtendaji Mkuu wa (DART), Bi. Asteria Mlambo aliwambia waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hivi karibu kuwa utekelezaji wa awamu ya kwanza unaendelea vizuri na kabla ya kukamirika hapo mwakani,kutakuwa na mabasi machache yataanza kufanya kazi mwaka huu.

“Mradi huu wa mabasi haya unatarajia kukamilika mwaka ujao lakini juhudi zinafanyika kuhakikisha mwaka huu yanapatikana mabasi machache kuanza kutoa huduma,”alisema Bi. Mlambo.

Alisema utekelezaji wa mradi huu umegawanyika katika awamu sita katika jij la Dar-es-salaam ambapo kwa sasa wapo katika awamu ya kwanza na inaendelea vizuri.

“Katika awamu hii ya kwanza wakandarasi wapo katika mafungu makuu sita, ambapo fungu la kwanza ni ujenzi wa barabara unaofanywa na kampuni ya strabag ya ujerumani kuanzia Kimara hadi Kivukoni,” alisema.

Fungu la pili ni kituo kikuu cha mabasi cha Ubungo ambako kunaajengwa  maegesho na karakana ya mabasi kwa ajili ya kufanyia mabasi matengnezo.

Bi. Mlambo alisema fungu la tatu ni ujenzi wa kituo cha maegesho eneo la jangwani ambacho pia kutajengwa makao makuu ya mradi kwa ajili ya maswala ya kiutawala.

Alisema fungu la nne ni eneo la kivukoni ambako ujenzi wake umefikia asilimia 90, fungu la tano ni ujenzi kituo kikuu eneo la Kariakoo Gerezani Quarter na fungu la sita ni vituo vidogo ambavyo vitashusha na kupakia abiria
“Vituo hivi vidogo vitawaunganisha abiria kutoka maeneo wanayoishi na mfumo wa mabasi haya,”alisema  mtendaji mkuu huyo na kuongeza kuwa maendeleo ya ujenzi wa mradi yanaridhisha.

Akifafanua zaidi alisema mpaka hivi sasa utekelezaji wa mradi huo upo katika kiwango cha 55% ya ujenzi wa miundombinu unasimamiwa na Wakala wa Usimamiaji wa Barabara nchini (TANROADS).
“Kampuni ya ushauri ya Rebel Group kutoka Uholanzi ambayo ilishanda zabuni itasaidia kupata watoa huduma baada ya kutangazwa tenda hiyo hapo mwezi mei, mwaka huu,” alisema.

Alisema katika utekelezaji mradi huo wakala ulikutana na changamoto mbalimbali ikiwemo ya kuwepo kwa huduma mbalimbali zilizokuwa zinaendeshwa kando ya barabara ambapo wakala ulilazimika kuingia gharama kuviondosha.

Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka ambao upo chini ya Ofisi ya Waziri Mkuu Serikali za Mitaa na Tawala za mikoa (TAMISEMI) unatekeleza maradi wa mabasi hayo ili kutatua kero ya msongamano wa magari katika jiji la Dar es Salaam.


Mwisho.

EPZA yatoa msaada Polisi Dar es Salaam

Mkurugenzi wa Fedha na Utawala wa  Mamlaka ya ukanda maalumu wa uwekezaji (EPZA), Bw. Desidery Kalimwenjuma (kushoto) akimkabidhi Mkuu wa  polisi wilaya ya kimara, SP Cosmas Papalika (katikati) moja ya vifaa vitakavyotumika kwa ajili ya ukarabati wa kituo kidogo cha polisi cha Mwongozo kilichopo Makuburi Kibangu jijini Dar es Salaam jana.  Wengine ni afisa wa polisi, Ali Rashidi (kulia), Mkuu wa kituo cha hicho, John Haule (wa pili kulia) na Mkuu wa kitengo cha manunuzi kutoka EPZA Bw. Joseph Matara (wa pili kushoto).
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Mamlaka ya Ukanda Maalumu wa Uwekezaji (EPZA) imetoa msaada wa vifaa vya ujenzi vyenye thamani ya Tshs 1,500,000 kwa Kituo cha Polisi Mwongozo, Makuburi Kibangu kwa ajili ya kukifanyia ukarabati.

Akikabidhi msaada huo Mkurugenzi wa Utawala na Fedha wa Mamlaka hiyo, Bw. Desidery Kalimwenjuma alisema msaada huo unalenga kukiboresha kituo hicho ambacho kipo karibu na mamlaka yao.

“Tunatambua suala la usalama katika maeneo ya uzalishaji,” alisema jana jijini Dar es Salaam na kuongeza kuwa hali hiyo iliwasukuma kutoa msaada wa vifaa vya ujenzi ili waweze kukarabati jengo hilo la kituo.

Alisema misaada ambayo mamlaka imetoa kwa kituo hicho ni pamoja na milango, , rangi za maji na za mafuta.

“Eneo la mamlaka yetu ni eneo maalumu la uwekezaji na linahitaji usalama zaidi,”aliongeza kusema Bw. Kalimwenjuma.

Alisema msaada huo pia ni sehemu ya kujenga mahusiano mena kati ya mamlaka, jeshi la polisi kupitia kituo hicho na serikali ya mtaa ya Makuburi Kibangu.

Alisema mamlaka inaahidi kuzidi kutoa misaada ya vifaa kama ilivyofanya kwa ajili ya kuboresha jengo la kituo hicho ambalo linahitaji matengenezo.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Kipolisi ya Kimara, SP Cosmas Papalika aliipongeza mamlaka hiyo kwa kutoa msaada huo. “Kiujumla hali ya usalama katika eneo hili ni nzuri, hakuna matukio ya kihalifu kama ilivyo kuwa huko nyuma,” alisema na kufafanua kuwa hilo linatokana na na ushirikiano unaotolewa na jamii katika eneo hilo.

Alisema kituo hicho na vile vyote katika  wilaya yake vinahitaji ushiriki wa jamii katika kuhakikisha vinaboreshwa zaidi na kutoa huduma nzuri.
Mwenyekiti wa Serikali ya Mtaa ya  Makuburi Kibangu, Bw. Moshi Kaftanyi liishukuru  mamlaka hiyo kwa kuitikia wito wa kusaidia kituo hicho cha polisi ambacho kipo katika mtaa wake.

“Kituo hiki kilikuwa kimechakaa, na tukaamua kuiomba mamlaka  isaidie ili kuweza kufanya marekebisho,” alisema na kuongeza kuwa moyo huo unatakiwa kuigwa na taasisi mbalimbali na jamii pia.

Alisema usalama mahali pa kazi na makazi ni muhimu sana, hivyo kunakila sababu ya kuhakikisha jamii na taasisi zinasaidia vituo vya polisi.


Mwisho.

Wednesday, March 5, 2014

DART yawatoa hofu watu wanaotaka kuomba zabuni za kutoa huduma

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Wakala wa Mradi wa Mabasi Yaendayo Haraka (DART Agency) umewataka watu wanaotaka kuomba tenda za kutoa huduma katika mradi huo wa mabasi kuondoa wasiwasi kwa kuwa zabuni hizo zitatangazwa kwa uwazi.
Kaimu Mtendaji Mkuu wa wakala huo, Bi. Asteria Mlambo aliwaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam kuwa watu waondoe wasiwasi kwa vile zabuni hizo zitatangazwa kwa mujibu wa sheria na taratibu.
“Huduma zinazotarajiwa kutangazwa ni pamoja na watu wenye uwezo  wa kuwekeza katika mabasi, uwezo wa kukatisha tiketi, kukusanya nauli, na nyingine,”alisema Bi. Mlambo.
Alisema huduma hizo hazijatangazwa hivyo watu waondoe wasiwasi kwa vile zabuni zitawekwa wazi na kila mmoja mwenye sifa ataomba.
Pia alisema hadi sasa hakuna mtu ambaye tayari ameshateuliwa, hivyo watu waondoe dhana hiyo kwa vile taratibu zote zitafanyika kwa uwazi na bila kificho.
“Kuna baadhi ya watu wanawasiwasi hasa wamiliki wa daladala kuwa wamewekwa pembeni...hii si kweli,” alisema.
Alisema katika kufanikisha hilo, mwezi Mei mwaka huu wakala unatarajia kufanya mkutano kuwawezesha watanzania na watu kutoka mataifa mbalimbali kujionea fursa zilizopo kutokana na mradi huo.
Alisema tayari wakala umeshapata mtaalamu ambaye ni Kampuni ya Rebel Group  ambaye atafanya mchakato wote wa kupata watoa huduma hao katika mfumo huo mpya wa mabasi.
Mtaalamu huyo alisaini mkataba na wakala Januari 15 mwaka huu na wamesha andaa utaratibu wa namna ya kupata watoa huduma hao.
Kwa mujibi wa afisa huyo, mfumo wa mabasi haya unatarajia kukamilika mwaka 2015 na kuanza kutoa huduma zake kama ilivyopangwa.
Aidha aliwataka wananchi kuhakikisha wanafuata sheria katika matumizi ya miundombinu ya mradi huo ili iweze kudumu kwa muda mrefu na kuchangia shughuli za maendeleo.
Vilevile wakala unahitaji ushirikiano kutoka mamlaka za Serikali za mitaa za jiji la Dar es Salaam hasa katika suala zima la utunzaji miundombinu vikiwemo vituo katika eneo la mradi.
Kwa muda mrefu pamekuwa na msongamano mkubwa wa magari na serikali inategemea kuwa mradi huo utasaidia kupunguza msongamano na foleni hizo.


Mwisho  

Dk. Turuka awataka wadau kujenga mazingira mazuri ya biashara nchini

Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam

Wadau wanaoshughulika moja kwa moja na mchakato wa usajili wa makampuni hapa nchini wametakiwa kufanya kazi kwa karibu zaidi ili kuimarisha kiwango cha Tanzania kimataifa katika kujenga mazingira ya biashara.

Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Dk. Florens Turuka amewaambia waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam wakati wa mkutano wa CEO Roundtable kuwa mamlaka hizo zinatakiwa kutekeleza mradi unaojulikana kama Tanzania Investment Window Project kabla ya mwezi Mei mwaka huu ili faida za ubunifu wake ziweze kuunganishwa katika viwango vya mwaka kesho vinavyohusiana na jinsi nchi zinavyoimarisha mazingira ya biashara.

Mradi huo unaofadhiliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Maendeleo (UNDP) na mpango wa ONE UN, unalenga kuwezesha makampuni ya ndani na ya nje kujisajili kwa urahisi zaidi na kwa muda mfupi.

Kituo cha Uwekezaji nchini (TIC) kwa msaada wa kiufundi toka shirika la umoja wa mataifa linalohusika na biashara na maendeleo (UNCTAD) kiko katika juhudi kuhakikisha kuwa taratibu za usajili wa makampuni unarahisishwa kupitia mtandao.       

Mpango huo uliasisiwa na Waziri Mkuu Mizengo Pinda mwezi wa Kumi mwaka jana nchini China.

Mpango huo utaruhusu wawekezaji kusajili makampuni, kupata vibali vya uwekezaji, vibali vya kazi na huduma nyingine kupitia njia ya mtandao.

Dk. Turuka alitaja baadhi ya taasisi zinazotakiwa kufanya kazi kwa karibu kama Wakala wa Usajili wa Makampuni (Brela), Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Wizara ya Biashara, Mamlaka ya Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA), Jiji la Dar es Salaam na TIC.

“Mamlaka hizi ziteue wawakilishi wa ngazi za juu kabisa watakaofuatilia kwa haraka utekelezaji wa mradi huu,” alisema, huku akipendekeza kikosi kazi hicho kukutana kila mwezi kuhakikisha kila kitu kinakwenda sawa.
Alisema kuwa mradi huo unachukuliwa kwa umakini mkubwa na Waziri Mkuu Pinda ambaye ametaka kuelezwa kila wakati maendeleo yake hadi pale utakapotekelezwa.

Pia alitoa shukrani zake kwa wadau wote waliowezesha mradi kufikia hatua iliyofikiwa hadi sasa kwa kipindi cha mwaka uliopita hasa kuhusiana na taarifa zinazohusu taratibu za uwekezaji.

Alisema hadi sasa taratibu 30 ziko wazi na zinaweza kufikiwa kirahisi kupitia mtandao wa TIC katika lugha zaidi ya 70.

Alisema taarifa hizo zinazopatikana kwa sasa zimeonyesha mafanikio makubwa kwa kuwa sasa kila wiki zaidi ya wafanyabiashara 1000 duniani kote wanatembelea mtandao huo na idadi ikiongezeka.

Akifafanua zaidi alisema sekta binafsi inataka kurahisishiwa mambo na kuwa hilo katika dunia ya leo linaweza kufanikishwa kwa kutumia mtandao.

“Mradi huu unaweza kufanikisha malengo hayo,” alisema.

Mwisho