Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya
Serengeti (SBL), Bw. Evans Mlelwa akisisitiza jambo jana kwa maafisa wa polisi
(hawako pichani) waliofanya ziara kwenye kiwanda hicho jana jijini Dar es
Salaam. Kushoto ni Naibu Kamishna wa
Polisi, Bohari Kuu (DCP) Adrian Magayane aliyeongoza ujumbe huo.
Naibu Kamishna wa Polisi, Bohari Kuu (DCP) Adrian
Magayane (wa tatu kushoto) akisikiliza maelezo ya Meneja Mkuu wa Upikaji Pombe
wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL),Bw. Donan Ritte (kushoto) wakati wa ziara
ya maafisa wa polisi katika kiwanda hicho jana jijini Dar es Salaam kujionea
shughuli za kiwanda hicho. Wa kwanza
kulia ni Inspeta Msaidizi wa polisi, Simpohanus Chacha na wa pili kutoka kulia
ni Inspeta, Milliton Masanja.
Na Mwandishi wetu, Dar es Salaam
Serikali imeshauriwa kutoongeza tena ushuru wa bidhaa za
pombe aina ya bia na vinywaji vikali tena ili kuwezesha viwanda kukua na kuweza
kutumia zaidi malighafi za ndani katika uzalishaji.
Akiongea na waandishi wa habari jana jijini Dar es Salaam,
Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Kampuni ya Bia ya Serengeti (SBL), Bw. Evans
Mlelwa amesema ongezeko la kila mara la ushuru wa bidhaa hizo unazuia ukuaji wa
viwanda na hivyo kurudisha nyuma maendeleo ya uchumi.
Bw. Mlelwa alikua akiongea katika kiwanda cha kampuni hiyo
baada ya ziara ya ujirani mwema ya kikundi cha maafisa wa polisi kutoka katika
bwalo la polisi barabara ya Kilwa.
Ugeni huo wa polisi uliongozwa na Naibu Kamishna wa Polisi wa
Bohari Kuu (DCP) Adrian Magayane.
Akielezea zaidi, Bw. Mlelwa alisema ongezeko la kila mara la
kodi hiyo kila inaposomwa bajeti ya nchi husababisha ongezeko la bei kwa
walaji.
“Mara baada ya ongezeko la kodi tu, wazalishaji nao huongeza
bei ya bidhaa zao na hali hii huleta athari kwa upande wa mauzo,” alisema.
Alifafanua kuwa kutokana na kushuka kwa mauzo
kunakosababishwa na kuongezeka kwa gharama, viwanda kama SBL vinapata
changamoto kufikia malengo yake ya kutumia malighafi za ndani na hivyo kuleta athari
kwa wakulima ambao wangefaidika kwa kuuza mazao yao.